Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, September 5, 2012

HUYU NDIE ASKARI POLISI ALIYEVYATUA BOMU NA KUMUUA MWANDISHI WA HABARI DAUD MWANGOSI...!

DAKIKA  CHACHE  KABLA  YA  KIFO  CHA  DAVID  MWANGOSI

ASKARI polisi aliyefyatu bomu lililomlipua na kumuua kinyama mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, David Mwangosi (40), amejulikana.

Tayari mazishi ya masalia ya mwili wa Mwangosi yamefanyika jana katika Kijiji cha Busoka, Kata ya Itete, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, huku ndugu, waandishi wa habari, wachungaji na wananchi wengine wakililaumu Jeshi la Polisi kwa mauaji hayo, na kwa kushindwa kuwachukulia hatua askari polisi waliosababisha kifo hicho na jina baya la jeshi hilo.

Picha zilizopigwa kwenye tukio la mauaji hayo, zinaonyesha askari wakiwa wamemzingira na kumpiga Mwangosi, baadhi yao wakiwa na virungu, na wengine bastola. Mmoja miongoni mwao, ameshikilia bunduki na kuielekeza tumboni.
Kutoka mazikoni, habari zinasema kuwa haikuwa kazi ndogo kuzuia vilio na simanzi zilizoonyeshwa na umati mkubwa wa waombolezaji waliofika kushuhudia mwili wa marehemu Mwangosi ulioharibiwa vibaya ukionyeshwa baada ya Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Busoka, Mathayo Mwantemanie kuongoza ibada ya mazishi.
Kifo cha mwandishi huyo ambacho kimevuta hisia za wananchi wengi ndani na nje ya nchi, hususani wakazi wa Wilaya ya Rungwe, kilimgusa kila mmoja akiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na wizara maalum, Profesa Mark Mwandosya na mkewe, Lucy Mwandosya waliofika nyumbani kwa marehemu.
Profesa Mwandosya alieleza jinsi msiba wa Mwangosi ulivyomgusa, kumuumiza moyo na kumfanya ashindwe kujizuia kutoa machozi kwani tayari alishapoteza wazazi wake wote wawili miaka michache iliyopita.
“Ni vigumu sana kwangu kuzungumzia hali hii, Mwangosi ameniuma sana, nimezunguka naye sana, nimefanya naye kazi kwa karibu sana, nimepotelewa na kijana wangu, mtoto wangu, mwenzangu katika kazi, kila nilipokuwa naye alinipiga sana maswali na mengi yalikuwa ya msingi,” alisema Profesa Mwandosya.
Kwa upande wake, Dk. Slaa ambaye alikuwa kwenye msafara wa kusafirisha mwili wa marehemu, alieleza mazingira ya kifo hicho na kusema msiba hauna itikadi, dini wala rangi, na kubeza kauli za ubaguzi dhidi ya msiba wa mwanahabari huyo.
Alisema CHADEMA itahakikisha haki ya Mwangosi haipotei na kuongeza kuwa binadamu si kuku, kwani damu yake lazima ipiganiwe kwa haki na kueleza jinsi chama hicho kinavyoshtushwa na vitendo vinavyofanywa na serikali dhidi ya vyombo vya habari, hususani kulifungia gazeti la MwanaHALISI na sasa wameamua kupoteza maisha ya mwanahabari huyo.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Kilutheri, Dk. Steven Kimondo na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Idara ya Thiolojia, aliuliza umati huo baada ya kusema kuwa Jeshi la Polisi linahusika na mauaji ya Mwangosi.
“Akili yangu inakataa kusema uongo kuwa Jeshi la Polisi halihusiki na tukio la kifo hiki, vitendo hivi vya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia vinajenga chuki kwa wananchi dhidi ya serikali yao na kwamba lazima uchunguzi ueleze ukweli kuwa marehemu hajafa kifo cha Mungu isipokuwa binadamu wamehusika,” alisema Dk. Kimondo.
Dk. Slaa alitoa ubani wa sh milioni 2, Mbeya Press Club (sh 700,000), Iringa Press Club (sh 1,750,000), MISA-Tan (sh 500,000), huku Profesa Mwandosya akiahidi kumsomesha mtoto mkubwa wa marehemu ambaye yupo kidato cha nne na wadogo zake, na alitoa ubani wa sh 500,000.

No comments:

Post a Comment