Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Rais Jakaya Kikwete, amezindua mradi wa uwekaji wa anuani za makazi na postikodi mkoa wa Dar es Salaam na kuwaagiza viongozi na watendaji wa Jiji, kuipa majina mitaa ambayo haina majina.
Aidha alisisitiza kuwa zoezi hilo lifanywe bila kisingizio cha fedha kwani kazi hiyo haihitaji pesa na kuwaonya wasije wakaikuza kuwa kazi ngumu inayohitaji kuandaliwa bajeti maalumu.
Aliwaambia mameya, madiwani, maofisa wa mipango miji, ardhi, mabaraza na viongozi wa mitaa kuanza zoezi hilo kwa kutoa majina kwa mitaa ambayo haina.
Anuani za makazi zinamaanisha kuipa mitaa majina na kuweka vibao vya kuitambulisha barabarani, kutoa namba za utambuzi kwa majengo na kuyapa majina majengo marefu.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jana, Rais alisema mitaa mingi ya jiji haina majina kutokana na watendaji kutokutimiza wajibu ipasavyo.
Rais alikumbusha kuwa baada ya Uhuru mitaa ilipewa majina mfano Ilala majina ya mikoa yalitumika mathalani Mtaa wa Arusha, Lindi wakati majina ya wanasiasa maarufu kama Samora, Toure, Luthuli, Nkurumah, Indira Ghadhi yanatumiwa katikati ya jiji.
Alishangazwa na watendaji wa sasa kushindwa kuipa mitaa majina na kuhoji inakuwaje maofisa wa mipango miji na wa ardhi wapime viwanja, waweke miundo mbinu lakini wasiipe mitaa majina?
Alisema maeneo ya Mbezi Beach na Tegeta yamepimwa lakini mitaa yake haina majina.
Katika hotuba yake aliagiza watendaji kuachana na majina ya kizamani mfano Mburahati Barafu na kubuni mapya yenye maana na kuongeza; “ondoeni majina ya kienyeji kama Kwa Dikwazu ambayo maana yake ni kwenye mti wa mkwaju”.
Rais aliwapa viongozi hao jukumu jingine la kutunga sheria za kulinda miundombinu yote inayotumika kwenye anuani za makazi mfano vibao vya majina ya mitaa na masanduku ya posta yatakayowekwa maeneo ya makazi.
“Usalama wa mali za watu ni lazima katika masanduku yenu ya posta,” alisema na kuwaagiza wadau wa mradi huo kutengeneza masanduku imara kuzuia mali za wateja kuibwa.
Aliwataka wadau hao kutoa elimu kwa wananchi ili wajue masuala ya anuani za makazi na wawe sehemu ya mradi huo.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Profesa John Mkoma, alisema zoezi la kutoa anuani za makazi ambazo zitahusisha pia postikodi ambazo ni namba zinazotambulisha na kutofautisha eneo moja na jingine lilianza tangu mwaka jana.
Postikodi hizo zimegawanywa hadi ngazi za kata na kuongeza kuwa zoezi la kugawa posti kodi hizo kwa nchi nzima limekamilika .
Profesa Mkoma alieleza faida za anuani za makazi kuwa ni pamoja na kurahisisha usambazaji huduma, ufanyaji biashara, maeneo kufikika kwa urahisi, kuimarisha ulinzi na usalama pia inaweza kusaidia kujua idadi kamili ya wakazi wa eneo husika.
Dar es Salaam ni mkoa wa tatu kutekeleza zoezi hilo baada ya Dodoma na Arusha.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment