Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, September 16, 2012

UAMSHO WALIPUKA TENA ZANZIBAR...!

Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa

Vurugu  kubwa zimezuka mjini hapa na kusababisha majengo likiwemo tawi la CCM kuchomwa moto, zinazodaiwa kufanywa na wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho eneo la Rahaleo.
Vurugu hizo zimetokea majira ya saa 1 usiku juzi wakati wafuasi hao walipofanya maandamano  wakitoka kwenye mhadhara uliyofanyika katika Msikiti wa Msumbiji Magomeni Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na kituo cha umeme kunusurika kuwaka moto.
Alisema  baada ya wafuasi hao kufika katika eneo hilo wakiwa na silaha za kienyeji yakiwemo mapanga na mawe, walianza kuwashambulia watu waliokuwa wamekaa nje ya jengo moja la ghorofa  kwa mawe.
Alisema  tawi la CCM maarufu kama Maskani Kachororo, lilivunjwa vioo vya madirisha kwa mawe na kuchoma mali kadhaa zilizokuwemo ndani.
Kamanda Mussa, alisema watu hao walifanya mkusanyiko na maadamano hayo kinyume na sheria na mtu mmoja amekamatwa kuhusiana na vurugu hizo ambapo anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Alisema wafuasi hao wamekuwa na tabia ya kufanya mihadhara yao msikitini na wanapomaliza hurejea kwa maandamano kinyume na sheria.
Alisema Jeshi la Polisi limekuwa likichukua hatua mbali mbali ikiwemo kuwaelimisha viongozi wa Uamsho kupitia Ofisi ya Mufti kuacha tabia hiyo bila ya mafanikio.
Hata hivyo, alisema watu waliohusika na tukio hilo wanaendelea kusakwa na polisi ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Msemaji wa Kachorora, Rajabu Omar Bakary, alisema wakiwa wamepumzika nje ya Tawi la CCM Kachorora, waliona kundi la watu wakitokea barabara ya Kijangwani na walipofika eneo hilo walianza kurusha mawe.
Alisema baada ya kuona hali imekuwa mbaya walikimbilia ndani na kufunga mlango huku wakiomba msaada kutoka polisi kwa kupiga simu.
Alisema wakati wakiwa ndani walichungulia nje na kuona watu hao wakimwaga mafuta ya petroli katika jengo la ghala la kuhifadhia samani za nyumba na kuchoma moto pamoja na bendera ya Chama cha Mapinduzi.
"Wakati tukiwa ndani tuliamua kutokea nyuma kupitia dirishani baada ya kuona wanamwaga mafuta ya petroli na kuwasha moto,” alisema Bakary.
Alisema baada ya kuona tukio hilo walipiga simu  Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kufuatia moto huo  kuwaka karibu na trasfoma ya umeme na walifanikiwa kuuzima kabla ya kuleta madhara.
Alisema hilo ni shambulio la  pili kutokea katika Maskani ya Kachorora na Kisonge kutupiwa mawe na wafuasi wa Uamsho.
Akizungumza na NIPASHE baada ya kukagua eneo hilo, Katibu Mwenezi wa CCM Taifa Nape Nauye, alisema wakati umefika kwa  Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara Zanzibar (JUMIKI) kufutwa na mrajisi wa serikali Zanzibar.
Alisema kwamba kikundi cha Uamsho  kina hatarisha amani na umoja wa kitaifa tangu kuvamia shughuli za kisiasa Zanzibar.
Alisema kwamba Uamsho imeacha kufanya majukumu yake ya kuwajenga waumini kiroho na badala yake kinafanya kazi za kisiasa bila ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Uamsho wana hatarisha amani na Umoja wa kitaifa wanafanya kazi ya siasa badala ya kufanya kazi ya dini,” alisema Nape.
Akizungumza na NIPASHE Katibu Mkuu wa Uamsho, Abdalla Said Ali, alikanusha Jumuiya yake kuhusika na shambulio hilo na kutaka kuudwe tume huru ya uchunguzi.
Alisema tume hiyo ifanye kazi ya kuchunguza tukio hilo pamoja na matukio mengine yaliyotokea nyuma na kuhusishwa na Uamsho.
 ‘Uamsho tumegeuzwa sawa na kitambaa cha mkononi kila uchafu tunafutiwa sisi lakini hatuhusiki na tukio hilo,” alisema kiongozi huyo.
Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja Kanali mstaafu Mahamoud Mzee alisema kitendo kilichofanywa na wafuasi wa Uamsho hakikubaliki mbele ya sheria.
Alisema Zanzibar inaweza kuingia katika vurugu kubwa kama wananchi wataamua kuchukua sheria mkononi kupambana na watu wanaofanya vurugu.
Kanali Mahmoud  alisema  serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kulinda amani na umoja wa kitaifa ikiwemo kuwasaka na kuwachukulia hatua watu waliohusika na kitendo hicho.
Jumuiya ya Uamsho imekuwa ikifanya kampeni katika misikiti za kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano na kuugwa mkono na baadhi ya Viongozi wa chama na Serikali Zanzibar.
Mwezi Mei mwaka huu Jumuiya hiyo pia ilihusishwa na vurugu za ku choma makanisa na baa, visiwani humo.


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment