Baadhi ya
vigogo waliowahi kuliongoza Jiji la Dar es Salaam akiwemo Charles Keenja
ni miongoni mwa wanaodaiwa kuuziwa eneo la mradi wa Shirika la
Maendeleo la Jiji la Dar es Salaam (DDC) na Manispaa ya Kinondoni.
Meneja
Mkuu wa DDC, Rwandiko Manumbu, alisema hayo jana wakati Kamati ya Fedha
na Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilipofanya ziara ya
kuangalia miradi ya shirika hilo na kutembelea shamba la Malolo lenye
ekari 5000, Mabwepande.
Alisema aliyekuwa Naibu Meya wa jiji la Dar es Salaam, Ahmed Mwilima,
alidai kuuziwa eneo katika sehemu hiyo bila kujua kama ni mali ya DDC.
Katika ziara ya kuzungukia eneo hilo, Manumbu alisema kuna baadhi ya
viongozi na wananchi wa kawaida wameuziwa zaidi ya hati 70 zilizotolewa
na Manispaa ya Kinondoni huku ikijua kuwa shamba hilo ni mali ya DDC.
Hata hivyo, Manumbu hakuwa tayari kumzungumzia suala la Keenja na Mwilima walivyouziwa viwanja hivyo.
"Viongozi hao sitaki kuwazungumzia ila wenyewe hawana neno kwani suala
hilo wanalitambua na kwamba wanatusikiliza sisi tutakachoamua kwani
walivyouziwa hawakujua kama ni shamba la DDC."
Manumbu alisema kwa sasa Manispaa ya Kinondoni inatakiwa kutengua hati
zilizotolewa na kuwatafutia wananchi hao viwanja katika maeneo mengine.
Alisema tangu mwaka 1984 wana hati miliki ya shamba hilo ambapo kwa sasa
wamekuwa na mvutano na Manispaa ya Kinondoni kwa kipindi cha miaka
mitano ili kubadilishia eneo hilo liwe la makazi.
Alisema suala hilo lilifika mpaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi ambapo ilibaini kuwa Manispaa ya Kinondoni ilitoa hati juu ya
hati jambo ambalo wizara iliwataka DDC kukutana kwa pamoja na Manispaa
hiyo ili kulijadili suala hilo na kulimaliza.
Alisema baada ya kupatiwa kibali cha kulibadilisha shamba hilo kuwa
makazi ya watu, Januari mwaka huu wamefanya jitihada mbalimbali za
kutaka kukutana na Manispaa ya Kinondoni ili kukizungumzia suala hilo na
matokeo yake imekuwa ikiwakwepa hadi sasa.
Manumbu alisema wanachotaka kukifanya sasa ni suala hilo kulikabidhi katika Halmashauri ya jiji ili kuanza kuvipima viwanja.
Alisema katika shamba hilo wanatarajia kupata mradi wa viwanja 3800 na
zoezi hilo lilitarajiwa kuanza mapema lakini tatizo ni Manispaa ya
Kinondoni kugoma kutoa ushirikiano na kusababisha ucheleweshaji wa zoezi
hilo.
Aidha, alisema ameshindwa kuielewa Manispaa ya Kinondoni kwa kitendo cha
kubomoa nyumba za wavamizi katika eneo hilo huku zingine za wavamizi
hao zikiachwa.
"Katika shamba letu kuna baadhi ya nyumba zimebomolewa lakini
nimeshindwa kuwaelewa ni kwa nini wameacha baadhi ya nyumba wakati wote
wale ni wavamizi walitakiwa wabomolewe nyumba zote na sio kuziacha,"
alisema.
Hata hivyo, alisema kuna tetesi kuwa watu hao walibomolewa kwa kuwa eneo hilo ni la watu wakubwa.
Akizungumzia DDC ya Mwenge, alisema kwa sasa wapo katika mchakato wa
kulibomoa jengo hilo kwa ajili ya kuanzisha mradi mkubwa wa jengo la
ghorofa saba kwa ajili ya biashara.
Alisema jengo hilo litagharaimu Dola za Marekani milioni 21 na litakamilika kwa kipindi cha miaka miwili.
Alisema muwekezaji ameshapatikana na ujenzi utakapokamilika watachukua
asilimia 65 na jiji litachukua asilimia 35 kwa kipindi cha mika 14.
Aliongeza kuwa mradi wa DDC Magomeni wenye ekari mbili umepangwa kujenga
jengo jingine kwa ajili ya shughuli za kibiashara na Benki ya
Rasilimali (TIB ) itawafadhili kwa mkopo wenye asilimia 80 hadi 100.
Alisema suala hilo bado lipo katika mazungumzo na tayari wameshatangaza tenda kwa watu 10.
Manumbu alisema dhumuni la kufanya mabadiliko hayo katika miradi hiyo ni
kutaka kuongeza kipato cha uchumi kuwa katika hali nzuri.
Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Chaurembo Abdallah, alisema kwa
pamoja katika kamati hiyo wamekubaliana kuunda kamati itakayosaidiana na
DDC katika zoezi la ugawaji wa viwanja.
Alisema kwa sasa wanashughulikia wavamizi kwa kuwapa notisi ili watu wa mipango miji waanze kazi ya upimaji.
Naye Mwenyekiti wa DDC ambaye pia ni Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas
Mtemvu, alisema kwa kuwa wameshabadilisha shamba hilo wataharikisha
zoezi hilo ili viwanja vipimwe na kutolewa kwa wananchi.
Alisema waliovamia wajiandae kuondoka na kwamba lengo kubwa ni kuboresha miradi ya DDC ili uchumi uweze kukua.
Kwa upande wao wananchi ambao wanadaiwa kuvamia maeneo hayo walieleza
kuwa wamekuwa wakifuata taratibu zote kwa kushirikiana na serikali za
mtaa katika kupata maeneo hayo.
Mmoja wa wakazi hao Sinandugu, alisema uongozi wa serikali za mtaa unahusika na zoezi la ugawaji viwanja.
Chanzo: nipashe
No comments:
Post a Comment