WABUNGE WAZALENDO ONENNI UFISADI MWINGINE KUPITIA GPSA...!
Waheshimiwa Wabunge na hasa Wabunge Wazalendo,
Salaam na poleni na majukumu ya kujenga taifa letu.
UTANGULIZI:
Kama kichwa cha habari hii kinavyosomeka, leo hii nimeamua kuwaeleza japo kwa ufupi kuhusu ufisadi mwingine unaoweza kuliangamiza taifa hili kupitia manunuzi ya umma ya bidhaa zinazoitwa "common use items".
Kama mnavyofahamu, kwa takriban miaka miwili sasa idara za serikali na mashirika ya umma yanalazimika kununua bidhaa mbalimbali kwa wazabuni waliopitishwa na Wakala wa Serikali wa Huduma za Manunuzi (GOVERNMENT PROCUREMENT SERVICES AGENCY - GPSA).
Utaratibu huu ni mpya na ni utekelezaji wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya 2004 ambayo imefanyiwa marekebisho hivi karibuni kuruhusu ununuzi wa bidhaa za mitumba kama vile ndege, meli, gari moshi, n.k.
Chini ya utaratibu huu mpya, Idara za Serikali na Mashirika ya Umma yanalazimika kupeleka mahitaji yao ya mwaka ya bidhaa mbalimbali kwa GPSA ili iendeshwe zabuni kwa nchi nzima ya kupata wazabuni wa kusambaza bidhaa.
Baada ya zabuni kuendeshwa, makampuni huteuliwa kutoa huduma ya usambazaji bidhaa mbalimbali na kwa bei iliyopitishwa na GPSA.
Makampuni hayo huingia mikataba na GPSA unaofahamika kama FRAMEWORK CONTRACT unaobainisha pamoja na mambo mengine bei za bidhaa (unit cost) na mahali pa kufikisha bidhaa hizo (delivery point).
UFISADI UNAVYOFANYIKA:
Katika mwaka huu wa fedha (2012/2013) idara za serikali na mashirika ya umma yametumiwa orodha ya makampuni ambayo yamepitishwa na GPSA kwa ajili ya usambazaji wa bidhaa mbalimbali na bei zake.
Kisheria, idara za serikali na mashirika ya umma hayaruhusiwi kununua bidhaa hizo nje ya makampuni hayo labda kama bidhaa inayohitajika haipo kwenye orodha ya GPSA. Kinachoshangaza na kusikitisha ni mambo mawili yafuatayo:-
Kwanza, makampuni mengi ni ya mifukoni (brief case companies).
Hayana ofisi na yale yenye ofisi hayauzi bidhaa zilizopo kwenye orodha ya GPSA. Kwa mfano, kampuni moja inaweza kuwa kwenye orodha ya makapuni yanayouza bidhaa za ujenzi (building materials) lakini ukienda ofisini kwake utakutana na ubao wa hiyo kampuni umeegeshwa kwenye duka linalouza vifaa vya kuandikia (stationery).
Ukihitaji bidhaa za ujenzi, mwenye kampuni atakutaka umpatie orodha ya bidhaa unazotaka halafu ataondoka kwenda kwenye maduka ya bidhaa za ujenzi kununua kwa bei ya chini na kisha kukuuzia kwa bei ya juu iliyopo kwenye Mkataba wa GPSA. Jambo hilo hufanyika waziwazi bila kificho.
Nachojiuliza ni je, kampuni hiyo ilipata kazi na kuingia Mkataba na GPSA kwa vigezo vipi ikiwa hata ofisi tu haipo? Kama huu siyo ufisadi ni nini!? Kwa nini watu tusifikiri kwamba kampuni hizo ni za wakubwa.
Pili, bei za bidhaa zilizopitishwa na GPSA ni kubwa kubwa kubwa kupita kiasi. Hata kama Mkataba ni wa mwaka mzima, lakini bado bei ni kubwa sana na Idara za Serikali na Mashirika ya Umma yanalazimika kununua bidhaa kwa bei hizo hata kama zinaumiza.
Kwa mfano, mimi binafsi nililazimika kununua bidhaa fulani kwa bei ya Sh. 80,000 wakati ambapo mwenye kampuni niliongozana nae na nikashuhudia akinunua bidhaa hiyohiyo kwa bei ya Sh. 45,000. Duka jingine lilikuwa linauza bidhaa hiyo hiyo kwa Sh. 45,500. Ilibidi nitumie Sh. 1,600,000 kwa kununua bidhaa 20 badala ya kutumia Sh. 900,000 kwa kununua bidhaa hiyo hiyo kwa idadi inayofanana. Hii ina maana kwamba endapo ningeshindanisha maduka zaidi ya matatu tofauti, kama ulivyokuwa utaratibu wa zamani, ningeweza kupata bei ya ushindani chini ya Sh. 45,000.
Ndugu zangu waheshimiwa wabunge, inawezekana lengo la utaratibu huu lilikuwa ni kupunguza mlolongo mrefu wa mchakato wa manunuzi ambao idara za serikali na mashirika ya umma yanalazimika kufuata wakati wa ununuzi wa bidhaa.
Pamoja na lengo hilo zuri, nataka niwahakikishie kwamba utaratibu huu tayari umetumiwa vibaya na wakubwa na athari zake zipo wazi.
Badala ya kuleta nafuu kwa wananchi. utaratibu wa "common use items" umeleta gharama na mzigo mkubwa kwa walipa kodi kwani bidhaa sasa zinanunuliwa mara mbili na hata zaidi ya bei ya kawaida.
Hivi kweli inaingia akilini kwa kisingizio cha mkataba wa mwaka mzima eti kitu kinachouzwa kwa bei ya kawaida ya Sh. 45,000 kiuzwe kwa Sh. 80,000 na mbaya zaidi kampuni yenyewe iliyopewa zabuni hiyo haina hata ofisi na haijihusishi kabisa na uuzaji wa bidhaa hiyo!!!
Kwa akili ya kawaida, kinachoonekana hapa huu ni Mradi wa wakubwa. Wameshinikiza utaratibu huu utumike kwa malengo ya kuingiza kampuni zao za brief case.
OMBI KWA WAHESHIMIWA WABUNGE:
Waheshimiwa wabunge, ninyi ndiyo sauti ya wananchi. Nimewaeleza jambo hili kwa lengo moja tu la kuwaomba mpige kelele na ikiwezekana iundwe tume itakayopitia orodha ya makampuni yaliyopitishwa na GPSA kwa mwaka huu wa fedha na kuona kama kweli ni makampuni halali yanayojohusisha na bidhaa husika na kama yana ofisi.
Wakati wa zoezi hilo, tume ipitie hata bei ili ione uhalali wa bei ili ibainishe namna fedha za umma zinavyotumika vibaya.
chanzo: JF
No comments:
Post a Comment