BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini
pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) imewaengua zaidi ya wanafunzi
3074 walioomba vyuo na mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2012/13.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
taasisi hizo kupitia mitandao yao (website) Agosti 10 na 12, 2012 zaidi
ya wanafunzi 3074 wameenguliwa katika maombi yao kwa kuwa na dosari
mbalimbali.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Bodi ya
Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) pekee imeorodhesha zaidi ya wanafunzi
2,649 ambao imebaini kuwa na mapungufu kadhaa katika maombi yao ya
kupewa mikopo ya vyuo.
Miongoni mwa makosa ama dosari ambazo
bodi imezibaini kwa walioenguliwa kwa sasa ni pamoja kukosekana kwa
vyeti vya kuzaliwa kwa muombaji, sahihi ya mdhamini/muombaji, kukosekana
kwa picha ndogo ya muombaji/mdhamini, kukosekana kwa sahihi za viongozi
wa Serikali za mitaa/vijiji kwa waombaji na nyaraka nyingine muhimu kwa
waombaji.
Kwa upande wake TCU imewaengua jumla ya waombaji 425 kwa dosari na makosa mbalimbali, ambayo imeyabainisha katika taarifa yake.
Miongoni mwa dosari ambazo zimetajwa na
TCU kwa wanafunzi hao ni pamoja na baadhi yao kukosea namba za vyeti
vya masomo kwa vidato vya nne na tano (O’ level na A’ level Index
number), miaka ya kumaliza masomo (year of completion), mawasiliano
sahihi kwa muombaji (Contact information e.g. Mobile phone number, email
address and postal address) pamoja na uchaguzi wa masomo (Programme
selected).
Waweza kuingia katika linki hii hapo chini na kuona majina ya waliobainika kuwa na dosari anuai katika maombi yao kwa TCU http://www.tcu.go.tz
Pia waweza kutembelea linki zifuatazo
na kushuhudia majina ya waliobainika kuwa na dosari hizo katika maombi
yao kwa bodi ya mikopo;-http://www.heslb.go.tz
Hata hivyo taasisi hizo mbili zimetoa
muda kwa walioenguliwa sasa kutokana na dosari hizo kurekebisha na
kutuma tena maombi yao kupitia mitandao kwa mujibu wa maelekezo
waliyotoa.
No comments:
Post a Comment