Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Saturday, October 6, 2012

RAISI AKERWA NA UPOTOSHAJI KUHUSU UKWELI WA MIRADI ENEO LA SERENGETI

Rais Jakaya Mrisho Kikwete

Rais  Jakaya Kikwete amesema anashangazwa na jitihada za upotoshaji wa makusudi wa ukweli kuhusu miradi ya maendeleo inayobuniwa na kuanzishwa na Serikali yake.

Amesema upotoshaji huo wa makusudi hautaifanya Serikali yake kubadilisha maamuzi yake kuhusu miradi ya maendeleo ya wananchi ama kuacha kubuni miradi mipya zaidi.

Rais Kikwete aliyasema hayo juzi wakati alipohojiwa na mwandishi wa habari mwandamizi wa Gazeti maarufu la Canada la Globe and Mail, Michael Posner  yaliyofanyika kwenye makazi rasmi ya Gavana Jenerali wa Canada, Jumba la Rideau, mjini Ottawa, Canada.

Rais Kikwete amezungumzia masuala mbali mbali yakiwemo jitihada za Serikali kuendeleza kilimo na mipango ya kujenga barabara kupitia Loliondo.

“Kamwe hatujapata kuwa na mipango ya kujenga barabara ya lami kukatisha Mbunga ya Serengeti. Huu ni upotoshaji wa kushangaza. Najua ni upotoshaji wa makusudi hata kama sijui unaanzia wapi. Tumesema na kusema tena kuwa tunalo jukumu la maendeleo kwa wananchi wote wakiwemo wa Loliondo na Mugumu ambao tumesema kuwa tutawajengea barabara ya lami.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Tunajenga barabara za lami zenye jumla ya kilomita 11,000 kwa sasa ili kuunganisha nchi nzima. Hivyo, wananchi wa Loliondo na Mugumu watakuwa sehemu ya maendeleo haya makubwa ya barabara.

Hakuna mtu atakayepisha barabara ya lami ndani ya Serengeti. Kwa hakika, kwa upande wa Loliondo, barabara ya lami itaishia kiasi cha kilomita 80 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.”

Alipoulizwa  kwa nini Serikali yake haionyeshi uchangamfu mkubwa kuhusu ujenzi wa barabara ya lami kupitia Kusini mwa Serengeti badala ya barabara hiyo kupita Kaskazini ndani ya Mbunga, kama inavyopendekezwa na baadhi ya wafadhili, Rais alijibu:

“Tunakaribisha sana wazo na ujenzi wa barabara Kusini mwa Serengeti, lakini barabara hiyo haitakuwa jibu la matatizo ya usafiri kwa wakazi wa Kaskazini. Barabara ya Kusini itahudumia watu wa Kusini na wala siyo watu wa Kaskazini.”

Kuhusu suala jingine ambalo linachochewa kwa njia nyingi na kwa kila namna kuwa Serikali inapora ardhi ya wakulima wadogo na kuitoa kwa wakulima wadogo ili kufanikisha mageuzi ya kilimo nchini, Rais alisema:

“Huu ni upotoshaji mwingine wa mipango yetu ya maendeleo. Sijui upumbavu huu unatoka wapi? Tunchofanya sisi chini ya mipango yetu ya kuleta mageuzi katika kilimo cha Tanzania ni kumsaidia mkulima mdogo kwa kulinda na kuiendeleza ardhi yake ili kumwokoa na njaa, kumpunguzia umasikini na kuongeza usalama wake wa chakula. Hakuna mkulima mdogo ambaye atanyang’anywa ardhi yake katika mipango yetu ili apewe mkulima mkubwa.”

Hata hivyo, Rais Kikwete amemwambia mwandishi huyo kuwa upotoshaji huo hautaifanya Serikali yake kuogopa na kushindwa kutelekeza majukumu yake ya maendeleo kwa wananchi kama ilivyoahidi kwenye Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu.

No comments:

Post a Comment