Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, October 25, 2012

Ewura, TRA watoa suluhusho uhaba wa mafuta..!

Kufuatia uhaba wa mafuta ya petroli na dizeli kuikumba baadhi ya mikoa kuanzia juzi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekubali kurekebisha utaratibu wa kuyatumia mafuta yaliyopo kwa ajili ya kusafirishwa nje na kuwakopesha wauzaji wa jumla wa kampuni zinazotoa huduma ya nishati hiyo hapa nchini.

Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao cha pamoja kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam, kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), TRA na baadhi ya kampuni zinazotoa huduma hiyo katika kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo.

Awali, Ewura walikuwa na kikao cha pamoja na baadhi ya kampuni za mafuta kwa lengo la kukutana na TRA ili iruhusu nishati hiyo ikopwe na kutumika ndani ya nchi na kwamba, meli nyingine zikileta yaweze kulipwa.

Akizungumza na NIPASHE baada ya kikao hicho cha kwanza kumalizika, Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema: “Tutaiomba TRA iyakopeshe makapuni hayo mafuta yanayotakiwa kuuzwa nje. Wanachukua yale mafuta, wanayatumia na kuyarudisha,” alisema Kaguo na kuongeza:

“Lengo la kwenda TRA ni kuwaomba warekebishe utaratibu wa kuyatumia mafuta yaliyopo kwa ajili ya kwenda nje ili wayauzie makapuni hayo na baadaye watayarudisha hadi hali itakapokaa sawa.”

Baadhi ya kampuni zilizoambatana na Mgurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, kwenda kuonana na TRA ili kushughulikia suala hilo ni Gapco, Oryx, Gusta na OMC.


Katika mahojiano maalum na NIPASHE kwa njia ya simu baada ya kikao hicho cha pili kumalizika, Kaguo alisema TRA wamekubaliana na ombi hilo, lakini bila kutoa ufafanuzi ni lini wataanza kuyatoa.

Alisema mafuta yote ya kusafirishwa nje yapo mikononi mwa TRA jambo lililowafanya waende huko ili waruhusu nishati hiyo ikopwe na kutumika ndani ya nchi na kwamba meli zingine zikileta yaweze kulipwa.

Mikoa, ambayo imeripotiwa kukumbwa na uhaba wa nishati hizo, ni Iringa, Njombe na Ruvuma, huku baadhi ya vituo vya mafuta katika maeneo hayo vikiishiwa kabisa mojawapo ya nishati hizo na vingine vyenye akiba kidogo vikishuhudiwa kuwa na misururu mirefu ya magari yakihitaji mafuta.

Tahadhari pia imetolewa kwa waishio maeneo ya mbali kutoka jijini Dar es Salaam, kwa kuchelewa kufikiwa na na nishati hiyo kwa muda mwafaka kutokana na umbali.

Kuhusiana na kupandishwa kiholela kwa bei ya nishati hizo iwapo bado hali hiyo haitatengemaa, alisema kampuni itakayokwenda kinyume cha sheria na taratibu za mamlaka hiyo inayotoa bei elekezi za nishati hizo, itapigwa faini ya Sh. milioni 7.

Kaguo alisema tatizo hilo lilichangiwa na kuharibika kwa boti zinazoingiza mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam kutoka nchi za jirani, Septemba.

No comments:

Post a Comment