Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, October 3, 2012

IMF yaiasa serikali gesi, mafuta vinufaishe wananchi

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeiasa Serikali ya Tanzania kutoa kipaumbele kwenye maandalizi ya mifumo ya udhibiti na kisera kwa ajili ya kuratibu mapato yatokanayo na kupatikana kwa gesi na mafuta, ili rasilimali hiyo iwanufaishe wananchi pamoja na kukuza uchumi.

Ushauri huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Paolo Mauro, kiongozi wa ujumbe wa timu ya maofisa wa IMF  waliokuwa nchini,  kwa lengo la kufanya majadiliano ya Tathmini ya Mapitio ya Tano, chini ya Mpango wa Ushauri wa Sera za Uchumi na Tathmini ya Kwanza ya chini ya Mpango wa Msaada wa Dharura.

Maura alisema kuwa kugundulika kwa gesi nchini ni neema kwa uchumi wa nchi endapo rasilimali hiyo itaandaliwa tararibu madhubuti, zitakazolenga kunufaisha ustawi wa wananchi.

“Kwa hiyo nashauri ziandaliwe sera, sheria na kanuni ambazo zitasimamia mapato yanayotokana na rasilimali hiyo ili shughuli za uchumi na ukuaji wa pato la Taifa uongezeke toka kiwango cha sasa cha asilimia 6.5 na asilimia 7, hali itakayoleta manufaa kwa wananchi,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa alisema Serikali imedhamiria kupunguza mfumuko wa bei kutoka kiwango cha sasa cha  asilimia 14.9 hadi kufikia tarakimu moja kwa lengo la kuwapunguzia wananchi makali ya maisha.

“Ukilinganisha hali ya mfumuko wa bei tuliyokuwa nayo mwaka jana na wakati huu, utaona kwamba tunafanya vizuri.
Hata hivyo, Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu (BoT) tutaendelea kudhibiti matumizi ya fedha na kuboresha uzalishaji kwa lengo lile lile la kupunguza mfumuko wa bei na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema.

Ujumbe wa IMF ulikuwa nchini kuanzia Septemba 19, mwaka huu na ulikutana na Waziri wa Fedha, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, pamoja na maafisa waandamizi wa Serikali.

Vilevile, ujumbe huo kukutana na wawakilishi wa Sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

No comments:

Post a Comment