Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba |
Jukwaa la Katiba Tanzania limesema kupatikana kwa katiba mpya ifikapo Aprili, 2014 ni ndoto kutokana na kusuasua kwa zoezi la ukusanyaji wa maoni linalofanywa na Tume ya Katiba kushindwa kufika maeneo mengi.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya ufuatiliaji wa mchakato wa ukusanyaji wa maoni katika mikoa saba, ambayo ni Kigoma, Lindi, Mwanza, Morogoro, Mbeya, Katavi na Ruvuma.
“Mchakato wa katiba bado unasuasua sana. Hivyo, itachukua muda mrefu kumfikia kila Mtanzania ili kupata maoni ya kila mwananchi. Hivyo, ni wazi kuwa ni jambo lisilowezekana kukamilisha hatua zote za mchakato kupata katiba mpya ifikapo Aprili, 2014,” alisema Kibamba.
Alisema tume hiyo haikufika kata nyingi kwa ajili ya kukusanya maoni, huku akitolea mfano Mkoa wa Kigoma, Wilaya ya Kasulu yenye kata 25 na kusema zilizofikiwa ni nne tu; Kilosa yenye kata 35 zilizofikiwa ni nne pia.
Akizungumzia Mkoa wa Mwanza, wilaya ya Sengerema yenye kata 34, alisema tume hiyo ilitembelea kata tano, huku Nachingwea, mkoani Lindi yenye kata 32 akisema zilizofikiwa ni kata tano.
Alisema makundi yenye mahitaji maalum, hasa watu wenye ulemavu, yameshindwa kushiriki katika kutoa maoni kwa kukosa wakalimani wa lugha za alama.
Kibamba alisema upungufu mwingine walioubaini katika mchakato huo, ni uwapo wa wakuu wa wilaya katika mikutano.
Alisema jambo hilo limekuwa ni tishio kwa baadhi ya wananchi, ambao hushindwa kutoa maoni yao kwa kwa kuwa kuna baadhi ya wananchi wamependekeza nafasi hizo zifutwe.
Akizungumzia muda wa mikutano, alishauri kuwe na mkutano mmoja wa jioni ili wananchi waweze kutoa maoni yao kwa kuwa mikutano ya asubuhi wengi wanakuwa katika shughuli za uzalishaji na hivyo, kushindwa kuhudhuria.
Alipendekeza mchakato wa utungaji katiba mpya uendelee kwa kasi ya kawaida kwa umakini mkubwa, huku ikipitia hatua zote za uandishi wa katiba ya kidemokrasia hata baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hata hivyo, pamoja na tume hiyo kupitia maeneo mbalimbali ya nchi kukusanya maoni, lakini pia iliweka utaratibu wa kupokea maoni ya wananchi kupitia barua kwa njia ya posta, barua pepe, simu na mitandao ya kijamii.
Tume hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, iliapishwa na Rais Jakaya Kikwete Aprili 13, mwaka huu.
Ilianza kazi yake Julai 2, mwaka huu, baada ya kujigawa katika makundi saba na ilipewa muda wa miezi 18 kufanya kazi hiyo hadi Aprili 26, 2014.
Jaji Warioba alikaririwa akisema tume hiyo itafanya kazi yake kwa awamu mbili tofauti; awamu ya kwanza ikiwa ni kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi.
Alisema awamu ya pili itakuwa ni kuandaa taarifa, mapendekezo na rasimu ya Katiba Mpya na kwamba, baadaye tume itakutana na Mabaraza ya Katiba na mwishowe rasimu ya katiba itafikishwa kwenye Bunge Maalum litakalowakilishwa na makundi mbalimbali katika jamii.
Tume hiyo ina wajumbe 32 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wakiongozwa na Jaji Warioba (Mwenyekiti) na Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani (Makamu Mwenyekiti).
Wajumbe wake wanaotoka Tanzania Bara ni Profesa Mwesiga Baregu, Riziki Shahari Mngwali, Dk. Sengodo Mvungi, Richard Lyimo, John Nkolo, Alhaj Said El- Maamry, Jesca Mkuchu, Profesa Palamagamba Kabudi, Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Kashonda, Al-Shaymaa Kwegyir, Mwantumu Malale na Joseph Butiku.
Wanaotoka Zanzibar ni Dk. Salim Ahmed Salim, Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salma Maoulidi, Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohamed Said, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali na Ally Abdullah Ally Saleh.
No comments:
Post a Comment