Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Saturday, October 6, 2012

MKAPA ASEMA "KOPENI NA KUREJESHA KWA WAKATI"

Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa

Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, amewataka watu na vikundi vinavyokopa pesa benki, kuhakikisha wanarejesha mapema mikopo hiyo sambamba na riba ili iweze kuwasaidia wengine kufanya hivyo.

Mkapa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua Benki ya Biashara ya DCB ambayo awali ilijulikana kama Benki ya Wananchi wa Dar es Salaam.

“Hakuna mkopo ambao ni bure…hakikisheni mnakopa na kurejesha kwa wakati muafaka ili pesa hizo ziweze kufanya kazi kwa watu wengine wanaohitaji mikopo,” alisema Mkapa.

Alisema, changamoto kwa uongozi wa benki ni kuhakikisha wanachukua hatua madhubuti kwa wateja wao ambao watajaribu kukwamisha malengo ya benki ya kueneza huduma kwa wateja wengi zaidi.

Rais mstaafu Mkapa licha ya kuzindua benki hiyo, ambayo pia ilikuwa ikiadhimisha miaka 10 tangu ianze kutoa huduma zake jijini Dar es Salaam  huku ikiwa na matawi matano katika wilaya zote tatu za Kinondoni, Ilala na Temeke.

Mkapa alialikwa kuizindua benki hiyo kutokana na kuwa muasisi aliyetoa wazo la kuanzishwa kwake kutokana na kilio cha wafanyabiashara waliolalamikia ukosefu wa mitaji ya kuendeleza biashara.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo, Balozi Paul Rupia, alisema tangu kuanzishwa kwa benki hiyo, wateja wengi wamefanikiwa kukopeshwa na kurejesha mikopo yao bila usumbufu na hivyo kufanikiwa kuongeza tawi la sita huko Chanika wilayani Ilala ambalo litafunguliwa hivi karibuni.

Alisema dhana ya kuongeza wateja zaidi bado ipo pale pale kutokana na kuingia kibiashara zaidi, na benki hiyo imefanikiwa kushika nafasi ya tano kati makampuni 10 ya kibenki katika soko la mitaji Afrika na ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki.

“Kwa sasa benki ina wateja zaidi ya laki mbili hadi Juni 30 mwaka huu ukilinganisha na wateja 12, 141 walioanza na benki 2002…na amana imeongezeka kutoka Sh.bilioni 1.8 hadi kufikia Sh.bilioni 77.9,” alisema.

Naye mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Edmund Mkwawa aliwashukuru wateja waliojiunga na benki hiyo kwa kuipa sapoti hadi kufikia hatua ya kufahamika zaidi.

No comments:

Post a Comment