Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, October 5, 2012

MNYIKA AMVAA WAZIRI MUHONGA

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amemtaka Waziri wa wizara hiyo Prof. Sospeter Muhongo, kufutia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wake, Eliakim maswi, kuwa lengo la agizo la kupitiwa kwa mikataba 26 ya utafutaji mafuta na gesi asili, ni kuhakikisha kwamba endapo kuna mapungufu katika mikataba hiyo, mapungufu hayo yasijirudie tena katika mikataba mipya ya baadaye kwa kuwa ikiachwa ilivyo italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa rasilimali za taifa.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), alieleza kuwa ufafanuzi uliotolewa na Maswi unatoa mwanya kwa mikataba mibovu kulindwa wakati ambapo kuna madai aliyotoa  toka mwaka 2011 kwamba baadhi ya mikataba hiyo imeingiwa kifisadi.

“Tafsiri ya ufafanuzi huo uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ni kwamba hata kama mikataba iliyopo ina mapungufu yasiyozingatia maslahi ya taifa, matokeo ya mapitio hayo hayatarekebisha mikataba iliyopo bali mikataba ya baadaye,” alisema.

Aidha, alisema taarifa ya Katibu Mkuu  huyo ni ya kurudi nyuma tofauti na kauli za awali za Waziri Muhongo zilizokubaliana na madai yake ya mwaka 2011 ndani na nje ya Bunge, ya kutaka mikataba yote ipitiwe upya, isiyozingatia maslahi ya taifa ivunjwe au ifanyiwe marekebisho makubwa na mikataba mipya isiingiwe mpaka kwanza kuwepo sera na sheria bora zenye kulinda uchumi na usalama wa nchi.

Septemba 15, mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC), Waziri Muhongo aliagiza bodi hiyo kuipitia mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na gesi asili ili kujiridhisha endapo maslahi ya taifa yalizingatiwa.

Mnyika alisema kuwa Waziri Muhongo na Katibu Mkuu wake wanapaswa kuendelea kuonyesha kwa maneno na matendo tofauti yao na viongozi waliowatangulia katika Wizara hiyo, kwa kutoa ufafanuzi wa ziada na kuchukua hatua zaidi vinginevyo taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa  Septemba 21, mwaka huu   itakuwa ni mwendelezo wa kulinda udhaifu wa kimfumo uliojikita katika Wizara hiyo na serikali kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment