Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, October 25, 2012

MUFTI; WAISLAM MSIVUNJE SHERIA..!

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Bin Simba.

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Bin Simba, amewataka Waislamu kuheshimu na kutii sheria za nchi na kufuata miongozo ya kidini, ili kudumisha amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, kufuatia matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani yenye kuashiria mpasuko wa kidini yaliyotokea hivi karibuni.

Mufti Simba alisema Waislamu na Wakristo wamekuwa wakiishi kwa amani kwa muda mrefu, lakini matukio ya hivi karibuni yanaonyesha dalili za kuleta mpasuko.

Aliwaomba Waislamu kuwa watulivu na kujiepusha na matendo ya uvunjifu wa sheria, ili mamlaka za nchi zifanye kazi.

“Ninawaomba Waislamu wawe na utulivu, wajiepushe na matendo ya kuvunja sheria ili mamlaka za nchi hii ziweze kufanya kazi zao,” alisema.

Katika vurugu za hivi karibuni, makanisa kadhaa yalichomwa moto na watu wanaodaiwa kuwa Waislamu baada ya mtoto kukojolea Ku’ran katika eneo la Mbagala, jijini Dar es Salaam.

WAFUASI WA PONDA KUANDAMANA

Wakati Mufti Simba akitoa wito wa amani, Jumuiya na Taasisi za Kiislam zinatarajia kuandaa maandamano ya kuilaani serikali kwa kitendo cha kuwanyanyasa Waislamu na udhalilishwaji wa kitabu cha Ku’ran kufuatia kitendo cha mtoto mmoja kuikojolea.

Maandamano hayo yatafanyika Novemba 2, mwaka huu  kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam na ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa wale watakaokuwa mikoani.

Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, Kondo Bungo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

 Alisema walipokea kwa masikitiko makubwa  taarifa za kukojolewa tena kitabu cha Ku’ran na kijana  Daudi Kapaya (20) mkoani Dar es Salaam na wao  wanaliachia Jeshi la polisi kulishughulikia suala hilo.

Bungo alisema jumuiya hizo zimelazimika kutoa msimamo wao wa kuandaa maandamano ili serikali iweze kuchukua hatua stahiki na za haraka kutatua mambo yanayowadhalilisha waislamu hususani taasisi zao.

POLISI: WAFUATE TARATIBU

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kinyela, alisema ikiwa kuna kikundi au taasisi inayohitaji kuonana na Waziri Mkuu, wanapaswa kufuata taratibu na kanuni za kisheria zitakazoweza kuwasaidia kufanya mazungumzo.

Kenyela aliyasema hayo alipokuwa akizungunza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Alisema maandamano yasiyofuata sheria inatambulika ni maandamano haramu yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

WALIONDAMANA IJUMAA KORTINI

Watu saba wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwamo kufanya maandamano bila kibali.

Washtakiwa hao ni Abdallah Muhamed (17), mkazi wa Sinza; Ibrahimu Kimweli (19), Omari Haji (30), Hassan Hatibu (30), Khalfan Mangala (30), wakazi wa Michikichini; Jamal Amiri (30), mkazi wa Kurasini na Muhamed Mbarook (30), mkazi wa Keko.

Mwendesha Mashtaka, Denis Mujumba, alidai  kuwa, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 19, mwaka huu katika Msikiti wa Idrisa eneo la Kariakoo, Wilaya ya Ilala walifanya uhalifu kwa kufanya mkusanyiko ambao haukuruhusiwa.

Shtaka la pili, walidaiwa kuwa Oktoba 19, walikaidi amri waliyopewa na ofisa wa Polisi ya kuwataka wasitishe maandamano.

Katika shtaka la tatu, walidaiwa kuwa Oktoba 19, mwaka huu walifanya maandamano ambayo yalisababisha kuvunjika kwa amani eneo la Kariakoo.

Hata hivyo, Hakimu Mfawidhi Joyce Minde aliyekuwa anatakiwa kusikiliza shauri hilo, alikuwa na dharura hivyo Hakimu Janeth Kinyage aliyesikiliza shauri hilo alishindwa kutoa dhamana kwa kuwa halikupelekwa kwake.

Washtakiwa walirudishwa rumande hadi Novemba 7, mwaka huu.

Washtakiwa hao ni kati ya Waislamu waliokamatwa Ijumaa iliyopita wakifanya maandamano kushinikiza Jeshi la Polisi, limuachie huru kiongozi wao, Sheikh Ponda Issa Ponda aachiwe huru.

MBARONI KWA KUMSHAMBULIA SHEIKH


Jeshi  la Polisi Mkoani Ruvuma limewatia mbaroni watu sita  wanaodaiwa kumpiga na kumjeruhi vibaya Sheikh wa Wilaya ya  Tunduru, Waziri Ally (76), mkazi wa mtaa wa Mchangani Mjini.

Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Robart Mhunga, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 24, mwaka huu saa 2:30 usiku nyumbani kwa Sheikh Waziri Ally wakati akiwa amelala.

Alisema sababu za kumvania ni kuwa walichukizwa na kitendo cha Sheikh huyo kuhudhuria maadhimisho  ya Jubilei ya miaka  25 ya upadri wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi, Casto Msemwa hivi karibuni mjini Tunduru.

Sababu nyingine  ni kuwa  Sheikh Waziri Ally alihudhuria Jubilei ya kutimiza miaka 50 ya Kanisa la Bibila  lililopo Mjini Tunduru hatua iliyoliudhi kundi moja la vijana wa Kiislamu.

Waliokamatwa ni Shaibu Said (22), Rajabu Abdallah (17), Baraka Maloya, Rajabu Yassin Hasani (20), Ally Kapopo (25) na Selemani Likokoto (22) wote wakazi wa eneo la barabara ya kutoka Tunduru kwenda Masasi.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, amelitaka jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika katika tukio la kupigwa kwa Sheikh Waziri wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

VIPEPERUSHI ZANZIBAR

Watu wasiojulikana wamesambaza vipeperushi wakitaka kuiitishwe kura ya maoni ya kuvunja mfumo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoasisiwa Novemba 2010.

Vipeperushi hivyo vyenye kichwa cha habari ‘Tamko la watu wa Waunguja kwa Wawakilishi wote wa CCM kutoka majimbo yote ya Unguja’ vimekuwa vikisabazwa katika maeneo ya mikusanyiko na baadhi ya wananchi kupenyezewa katika milango yao.

“Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) imeshindwa kudumisha na kulinda amani na umoja wa kitafia wa wananchi wa Zanzibar,’ sehemu ya vipeperushi vimeleeza.

Vipeperushi hivyo vimetoa  mapendekezo matatu wakitaka serikali kuangalia upya mabadiliko ya 10 ambayo yanaruhusu kuudwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Wametaka viongozi dhamana waliopewa majukumu ya kusimamia sheria wafukuzwe  akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar kutokana na vurugu zinazofanywa na kikundi cha Uamsho kila mara Visiwani humo.

Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Leonce Zimbandu, Nuru Mfaume, Jacqueline Yeuda, Dar; Gideon  Mwakanosya, Songea na Mwinyi Sadallah, Zanzibar.

No comments:

Post a Comment