Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, October 4, 2012

POLISI WAVAMIA NYUMBA YA KULALA WAGENI NA KUMUUA MCHIMBA MADINI...!

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Paulo Kasabago

Jeshi la Polisi limeendelea kuandamwa na matukio ya kuua raia baada ya askari wake wanne, akiwamo Mkuu wa Kituo (OCS) kukamatwa kwa tuhuma za kuvamia nyumba ya kulala wageni, kujeruhi, kupora mali na kumuua mchimbaji wa madini.

Tukio hilo limetokea katika Wilaya ya Chato, mkoani Geita baada ya askari hao kutuhumiwa kuwavamia wafanyabiashara wawili waliokuwa kwenye nyumba hiyo, kuwapora fedha, mawe yanayosadikiwa kuwa dhahabu na kuwajeruhi kwa vipigo ambavyo vilisababisha kifo cha mmoja wao.

Askari wanaotuhumiwa kuhusika katika tukio hilo ni wa kituo cha polisi cha Buziku wilayani Chato ambao waliwavamia David Gilles Vyamana na Gilbert Ntabonwa, wakazi wa kijiji cha Kakeneno wilayani humo na wazaliwa wa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Agosti 30, mwaka huu wakati watu hao wakiwa kwenye nyumba ya wageni ya Buziku Inn.

Watu hao wanaosadikiwa kuwa ni wachimbaji wadogo wa dhahabu, kabla ya kukumbwa na mkasa huo, walitokea kijijini kwao Kakeneno na kuelekea kijiji cha Buziku kwa ajili ya kuburudika na kwamba baada ya kupanga vyumba katika nyumba hiyo mmoja akiwa chumba namba mbili na mwingine namba tatu, walimuomba mhudumu kuendelea kuwahudumia vinywaji wakiwa vyumbani.

Habari zinasema kuwa saa 5:30 usiku, polisi walivamia eneo hilo na kuwaamuru wachimbaji hao kufungua milango ya vyumba vyao.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, baada ya watu hao kukataa kutii amri hiyo huku wakihoji uhalali wa kuwaamuru kufungua milango wakati wamelala, askari hao walitumia nguvu kubwa na kufanikiwa kuvunja milango kisha kuanza kuwaadhibu kwa vipigo vikali.

Habari zinadai kuwa katika chumba cha kwanza askari hao walichukua kiasi cha Sh. 500,000 na  mawe yanayosadikiwa kuwa ni dhahabu yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye mfuko mdogo katika chumba cha pili.

Baada ya kuwapa kichapo, waliwachukua na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi na kushikiliwa kwa muda na baadaye baada ya kubaini kuwa hali zao zinaendelea kuwa mbaya kutokana na majeraha, walilazimika kuwaondoa haraka na kuwapeleka kwenye Kituo cha Afya cha Bwanga kabla ya kuwahamishia  Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa  matibabu zaidi.

Shuhuda mwingine, alidai kuwa baada ya wachimbaji hao kukaidi kufungua milango licha ya mhudumu wa nyumba hiyo, Godesiliva Paulo, kuwataarifu kuwa wanaowahitaji ni askari polisi, polisi walilazimika kutumia nguvu kuingia ndani, lakini katika hali ya kushangaza wachimbaji hao walikutwa ndani ya chumba kimoja wakiendelea kunywa pombe na ghafla mmoja wao alimkwida koo PC Mwidin, hali iliyowalazimu kutumia nguvu kubwa kuwaondoa vyumbani vyao kwa lengo la kuwapeleka kituo cha polisi.

Aliongeza kuwa baada ya askari hao kufanikiwa kuwatoa ndani ya chumba wachimbaji hao walikaidi kwenda kituo cha polisi na kuanza kupiga yowe wakiomba msaada kwa wananchi na baada ya muda mfupi, watu wengi walikusanyika eneo hilo na kuanza kuwashambulia na kuwajeruhi.

Alisema kuwa baada ya kutambua hali zao siyo nzuri walilazimika kuwapeleka kupata matibabu, lakini wakati wakiendela kuhudumiwa, mmoja wao aliyefahamika kwa jina la Gilbert Ntabonwa (40) alifariki dunia akiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Chato.

KAULI YA KAIMU RPC

Akizungumza na NIPASHE, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Paulo Kasabago, mbali na kuthibitisha kuwapo kwa tukio hilo, alisema kuwa uchunguzi wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa askari wake walienda kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusiana na kuwepo kwa watu wanaohofiwa kuwa ni wahalifu kutokana na mazungumzo yao wakati wakinywa pombe kabla ya kuingia ndani ya vyumba vyao.

“Askari wetu walikwenda eneo hilo baada ya kupigiwa simu na raia mwema kuwa watu waliokuwa wakinywa pombe kwenye gesti hiyo siyo wema kutokana na mazungumzo mbalimbali waliyokuwa wakiyazungumza kabla ya kuhama nje na kuingia ndani ya vyumba vyao,” alisema Kasabago.

 Kufuatia hali hiyo jeshi hilo linawashikilia askari wake wanne akiwemo mkuu wa kituo hicho, Sajenti Raulens Bendera, kwa ajili ya uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo la mauaji na kwamba itakapothibitika kuhusika, hatua za kisheria zitashika mkondo wake.

 ASKARI WANAOSHIKILIWA

Kamanda Kasabago aliowataja wengine wanaoshikiliwa kuwa ni PC Mwidini, PC abdallah na PC Yusuph, wote wakiwa ni askari wa kituo kidogo cha Buziku wilayani Chato.

Kamanda Kasabago aliongeza kuwa baada ya upekuzi uliofanywa na askari hao, waliwakuta wachimbaji hao wakiwa na fedha taslimu Sh. 500,500, kiroba cha mfuko unaosadikiwa kuwa na mawe ya dhahabu na chupa moja ya bia.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, Dk. Pius Buchukundi, alithibitisha kupokea majeruhi wawili waliopelekwa hospitalini hapo kutoka Kituo cha Afya cha Bwanga na kwamba wakati wakiendelea kuwatibu, mmoja wao alifariki dunia na kwamba Vyamana anaendelea vizuri.

Dk. Buchukundi alisema kuwa uchunguzi wao ulibaini kuwa marehemu alijeruhiwa kutokana na kipigo kilichosababisha damu kuvujia ndani ya mwili.

Kwa mujibu wa Dk. Buchukundi, tayari ndugu na jamaa wa marehemu huyo wamefika na kuchukua mwili wake kwa ajili ya kuusafirisha kwenda nyumbani kwao Kibondo, mkoani Kigoma kwa ya maziko.

Septemba 2, mwaka huu, polisi walimuua aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi, Mkoa wa Iringa wakati viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakifungua tawi la chama chao.

Askari mmoja, Pacificus Cleophace Simon (23), alifikishwa mahakamni mjini Iringa akikabiliwa na kosa la kumua Mwangosi.

Jumapili iliyopita Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Septemba pamoja na mambo mengine aliwataka polisi kuacha kutumia nguvu kupita kiasi wanapokabilina na vikundi na raia.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment