Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, October 4, 2012

BODI YA TANESCO YAKALIA KUTI KAVU

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi William Mhando

Takribani miezi miwili na ushei tangu Bodi ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuwasimamisha kazi viongozi wakuu wa shirika hilo akiwamo Mkurugenzi Mkuu, William Mhando na wenzake watatu kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka, wizara mama ya shirika hilo, imetangaza kuwa itaivunja bodi hiyo ili kuisuka upya kwa kuingiza watu wenye upeo na uzalendo.

Tamko kwamba bodi hiyo sasa imekalia kuti kavu lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, alipokuwa akizindua kitabu chenye taarifa kuhusu Haki za Binadamu na Biashara/Uwekezaji nchini kilichoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Julai 14, mwaka huu bodi ya Tanesco chini ya Mwenyekiti wake, Janerali Mstaafu, Robert Mboma, iliwasimamisha kazi Mhando; Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Manunuzi Harun Mattambo.

Vigogo hao walisimamishwa ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili.
Masele alisema wizara iko mbioni kuzivunja na kuziunda upya bodi za Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na ya Tanesco ili ziwe na watu wenye sifa na uzalendo wa kusimamia maslahi ya nchi kama ilivyofanyika kwenye Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Masele ambaye anashughulikia Madini, alisema kwamba wizara yake inakusudia kuchukua hatua hiyo kama mojawapo ya mapinduzi makubwa iliyodhamiria kuyafanya kutokana na mchango mkubwa inayoweza kuutoa katika uchumi wa nchi kutokana na kusimamia sekta muhimu kwa maendeleo ya nchi za madini, nishati na kwa hivi sasa gesi na mafuta.

“Stamico kwa sasa inatakiwa ibebe uchumi wa nchi, kwa kusimamia hisa za serikali kwenye uwekezaji wa madini, na kwa hali hiyo tunahitaji kupata watu walio na sifa stahiki na waliopatikana bila ya upendeleo na kujuana, bali kutoka kwenye ushindani wa wazi,” alisema.

Alisema shirika hilo pamoja na mengineyo, lina kazi za kusimamia asilimia 50 ya hisa toka kwenye kampuni ya Tanzanite One na asilimia 15, 20 hadi 30 ya hisa za serikali zinazotarajiwa kwenye makampuni mengine na kwa hali hiyo inabidi liwe na watu wenye uwezo na wanaoongozwa na uzalendo.

Masele alisema kuwa wizara yake imedhamiria kwa dhati kulinda maslahi ya Watanzania ili itoe mchango utakaowezesha kujenga ustawi wa wananchi na kutokana na hali hiyo, alisema kwamba wako tayari ‘kuchinja’ watu wachache watakaojaribu kuwazuia kulifikia lengo hilo kwa maslahi ya wengi na kwamba wamegundua kuwa ‘wanaoiua’ nchi ni Watanzania wenyewe.

“Wakati wanaandikisha maelezo yao wale wawekezaji tuliowakamata hivi karibuni kwa kosa la kutolipa kodi inayotakiwa, walieleza kuwa mara nyingi maofisa wa Kitanzania waliowekwa kwa ajili ya kuona na kuchukua takwimu za madini yanayofungwa kwa ajili ya kusafirishwa nje waliwaruhusu wawekezaji hao kufunga madini bila ya wao kuwapo kwa maelezo kuwa watazisaini nyaraka za mizigo hiyo kesho yake,” alisema.

Akiizungumzia Tanesco, Masele alisema kwamba wanakusudia kuivunja bodi ya shirika hilo kutokana na dhamira yao ya kuhakikisha kwamba mgawo wa umeme hautokei tena na kwamba kukamilika kwa bomba la gesi hapo Machi mwakani na kuanza kutumika kwa gesi hiyo viwandani na majumbani kunahitaji bodi imara, yenye weledi na uzalendo kwa nchi.

Alisema wizara yake imeunda kikosi kazi kinachoundwa na wastaafu wa shirika hilo wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Tanesco, Baruany Luhanga, kwa lengo la kuupitia muundo wa shirika hilo na kupendekeza muundo stahiki unaofaa kufuatwa na shirika na kwamba kikosi kazi hicho kimewezeshwa kwenda nje ya nchi kwa lengo la kujifunza mfumo unaofaa.

“Kuna maelezo yanayotolewa kwamba shirika limewekeza rasilimali na utaalamu zaidi kwenye uzalishaji wa umeme, badala ya usafirishaji na usambazaji, hali inayoweza ikasababisha umeme mwingi ukazalishwa zaidi ya uwezo wa kuusafirisha au zaidi ya uwezo wa kuusambaza na mapendekezo yanatolewa kwamba pengine ni vizuri kila eneo likajitegemea,” alisema Naibu Waziri huyo.

Alisema wizara inakusudia kuwa na bodi itakayolenga kuhakikisha kwamba bei ya nishati hiyo inashuka na hivyo kushusha gharama za uzalishaji viwandani na hatimaye kupunguza makali ya maisha kwa wananchi.

Aidha, mbali na kuvunja bodi hizo, Masele alisema kwamba wanakusudia kuziongezea nguvu za wataalamu na rasilimali menejimenti za mashirika hayo ili ziende na kasi wanayoihitaji ya kulinda rasilimali za nchi kwa faida ya Watanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Helen Kijo- Bisimba, aliipongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na wizara hiyo chini ya Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo, baada ya kuteuliwa kuiongoza.

“Tunaipongeza wizara kwa kukataa nchi yetu kuendelea kuwa shamba la bibi, kwamba kila mtu anakuja kuchuma na kuondoka zake,” alisema Dk. Bisimba na kuongeza:

“Tunawaunga mkono katika dhamira yenu ya kuwatupa nje wale wachache wasiolinda maslahi yetu na sisi tutaungana na nyie kuwacheka na kuwang’ong’a mtakapowatupa kupitia madirishani.”

Taarifa iliyozinduliwa jana ni ya kwanza kutolewa na LHRC katika historia ya utetezi wa haki za binadamu nchini na imetazama sheria na sera mbalimbali katika biashara/uwekezaji, mkazo ukiwa kwenye maeneo matano.

Maeneo hayo ni haki za ajira na kazi, haki ya kumiliki ardhi, haki ya kuishi katika mazingira safi na salama, haki za walaji na bidhaa zinazozalishwa viwandani pamoja na uwajibikaji wa kampuni kwa jamii.

No comments:

Post a Comment