Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, October 23, 2012

Shahidi adai alikuwa akimpa mshitakiwa fedha za kodi.

Mfanyabiashara, Onesmo Massawe (26), ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kwamba, mshtakiwa anayedaiwa kumwibia mwenye nyumba wake zaidi ya Sh. milioni 37 ndiye aliyekuwa akimpa fedha za kodi.

Massawe alitoa madai hayo jana wakati akitoa ushahidi wa Jamhuri akiongozwa na Charles Anindo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Genivitus Dudu.

Alidai kuwa alipanga chumba cha duka katika nyumba ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, iliyopo Mikocheni ‘B’ na alilipa pango la mwaka kwa mkataba wa kwanza 2011-2012.

Alidai alimpa mshitakiwa, Abdallah Mzombe, kodi za dukani, lakini alikuwa ana mkataba kwa sababu alikuwa anachukua vitu mbalimbali dukani, kama vile mafuta ya kupikia, lakini ikifikia wakati wa kulipa kodi anamkata kinachobaki anampa.

“Mkataba wa pili mwaka 2012-2013 kodi iliongezeka na kufikia Sh. 60,000. Nilikarabati chumba cha duka kwa kuweka vigae. Ikagharimu Sh, 570,000. Iliyobaki Sh. 150,000 nilimpa mshitakiwa na hakuonekana tena kuniletea mkataba, ndio namkuta mahakamani,” alidai shahidi huyo wa tano wa upande wa mashitaka.

Shahidi alidai katika nyumba ya Mwinyi kuna wapangaji wanne katika fremu za duka, lakini hajui wapangaji wengine walikuwa wanalipaje kodi zao.

Anindo aliomba kuahirisha kesi hadi tarehe nyingine kwani shahidi wake mmoja wa mwisho amekwenda Hijja.

Hakimu Dudu alikubali kuahirisha kesi hadi Novemba 7, mwaka huu, na kuamuru siku hiyo wamalize kutoa ushahidi wa upande wa mashitaka.

Mzombe alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 21, mwaka huu, akidaiwa kwamba, kati ya Januari 2011 na Julai 2012, maeneo ya Mikocheni, Dar es Salaam, akiwa mfanyakazi wa Ali Hassan Mwinyi aliiba Sh. 17,640,000 alizokusanya kodi katika nyumba namba 481 plot ‘A’ eneo la Mikocheni kwa ajili ya kodi mwaka 2011/2012 na 2012/2013 alizotakiwa kuzikifikisha kwa Mwinyi, lakini hakufanya hivyo.

Mshtakiwa pia anadaiwa katika kipindi hicho maeneo ya Msasani Village, aliiba Sh. 19,800,000 alizokusanya kodi katika nyumba namba 55 block C Msasani Village. Alikana mashitaka na amerudishwa rumande kwa kukosa dhamana.


No comments:

Post a Comment