Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, October 16, 2012

UBAKAJI BADO NI TATIZO KUBWA KWA MKOA WA KILIMANJARO. ..!

MATUKIO ya ubakaji katika mkoa wa Kilimanjaro yameelezewa kuongezeka huku wahanga wakubwa wakiwa ni watoto jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa masiha yao.
 
Takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya makosa 46 ya ubakaji  yameripotiwa polisi katika kipindi cha Julai hadi septemba mwaka huu ambapo asilimia 90 kati yao ni watoto.
 
Hayo yamebainishwa na kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro Bw. Robert Boaz wakati akizungumza na mtandao huu ofisini kwake kuhusiana na matukio ya ubakaji katika mkoa huo, ambapo alisema matukio hayo  yamekuwa yakijirudia mara kwa mara.
 
Kamanda Boaz alisema matukio ya ubakaji yameanza kujitokeza kwa wingi katika mkoa wa Kilimanjaro hivyo kunahitajika ushirikiano wa hali ya juu kutoka katika jamii ili kuweza kuyadhibiti na kuyakomesha kabisa.
 
“Yapo makosa ambayo yameanza kujitokeza katika mkoa wetu,na makosa ya ubakaji ni makosa ambayo yamekuwa yakijirudiarudia,sasa jamii inapaswa kuchukua hatua za makusudi ili kulikemea hili kwani likiachwa liendelee ni hatari kubwa kwa jamii”alisema Kamanda Boaz.
 
Kufuatia hali hiyo Kamanda Boaz alizitaka taasisi za dini kutoa ushirikiano katika kudhibiti tatizo hilo ili kulikomesha ikiwa ni pamoja na kulikemea katika nyumba zao za ibada, kutokana na kwamba wanaofanya vitendo hivyo wapo pia katika nyumba za ibada.
 
“Tunawaomba watu wa dini watusaidie katika hili,walikemee kwenye nyumba zao za ibada lakini pia wanaharakati wa haki za watoto na wanawake nao watuunge mkono kwani tatizo hili limezidi kuwa kubwa na linawaharibu watoto”alisema.
 
Kamanda Boaz alisema katika kudhibiti tatizo hilo jeshi la polisi limeanzisha dawati ambalo limekuwa likishughulikia matatizo hayo ikiwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia ili kutoa uhuru kwa watu wa rika zote kufika na kujieleza.
 
Alisema madawati hayo yamekuwa yakifanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha haki za watoto zinafatwa ,ambapo pia hushughulikia masuala ya kijinsia na usuluhishi wa kifamilia.
 
Na Florah Temba, Moshi
Chanzo: www.kilimanjaro-yetu.blogspot.com

No comments:

Post a Comment