Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, October 16, 2012

WASOMI WACHELEA USHIRIKISHWAJI HAFIFU WA RAIA KATIKA MTANGAMANO WA EAC...!

Wasomi kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania wameuelezea mtangamano wa miaka 10 wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwamba una sura ya ushirikiano baina ya serikali zaidi huku ukiwa umekosa ushiriki wa moja kwa moja wa raia ndani ya nchi tano wanachama wa jumuiya hiyo.

Wasomi hao walikuwa wanawasilisha kwenye mkutano matokeo ya utafiti waliofanya ndani ya nchi hizo juu ya ‘’ Ushiriki wa raia katika mchakato wa mtangamano wa Jumuia ya Afrika Mashariki’’ uliofanyika mjini Arusha.

Profesa Mwambutsya Ndembesa kutoka Uganda aliwakumbusha wajumbe wa mkutano huo kutoka nchi zote tano kwamba, hatua tatu kati ya nne za mtangamanano huo zinahusiana na masuala ya kiuchumi.

‘’Umoja wa Forodha unahusiana na masuala ya soko au feddha; Soko la Pamoja inatawaliwa na mambo ya uchumi;Umoja wa Sarafu unahusiana na ushikiano katika masuala ya fedha; hatua ya mwisho ni kufikia Shirikisho la Kisiasa. Hatuoni waziwazi katika mpango huo mzima jambo linalohusu ushirikiano wa raia au jamii,’’ Profesa Ndembesa alisema.

Alifafanua wazo kwamba suala la ushiriki wa raia limetajwa tu katika nyaraka mbalimbali zilizofufua upya jumuiya hiyo lakini halikupewa umuhimu unaostahili. ‘’Tunahitaji kuurekebisha na kuufanyia tathmini mkataba wa EAC ili ujumuishe mtangamano wa raia,’’ alisisitiza.

Dk. James Kasombo kutoka Kenya aliunga mkono mawazo ya msomi mwenzake kutoka Uganda juu ya mapungufu yaliyomo katika kushirikisha raia kwenye mchakato mzima wa mtangamano. ‘’Mtangamano umejikita zaidi kwenye serikali. Raia hawahusishwi moja kwa moja katika mchakato wa mtangamano.’’

Alisema vyama vya siasa havina budi sasa kuingiza masuala ya mtangamano katika ilani za vyama vyao ili kukuza ushiriki wa raia katika mchakato mzima ili kuongeza juhudi zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na vyama vya kiraia katika kukuza uelewa wa raia kuhusu masuala ya mtangamano.

Hata hivyo Profesa Bernadette Kilian wa Tanzania alisema matokeo ya utafiti huo haumaanishi kwamba mradi wa EAC umekufa. ‘’ Kuwepo au kutokuwepo kwa ushiriki wa raia katika mchakato, EAC itaendelea na shughuli zake. Hivi sasa wanalo jengo jipya la ofisi na wako tayari kuhamia humo wakati wowote,’’ alieleza.

Alifafanua kwamba mapungufu ya urasimu wa jumuiya na ushiriki wa watu katika mchakato wake, ni mambo ambayo yanaweza kushughulikiwa kadiri mchakato unavyozidi kusonga mbele, huku akipendekeza kwamba hatua itakayofuatia iwe ni ya kutathmini ukuaji wa EAC.

Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya taasisi ya Vision East Africa Forum Ltd (VEAF) na Shirika moja la Ujerumani FES , ofisi ya Tanzania.

NI/IM/NI

No comments:

Post a Comment