Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, November 5, 2012

Wakimbizi wazidi kupungua nchini..!

Idadi ya wakimbizi nchini imeendelea kupungua baada ya serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kuwarudisha nchini kwao wakimbizi wa Kirundi 356 kutoka kambi ya Mtabila iliyopo mkoani Kigoma.

Hatua hiyo ni moja ya mikakati ya serikali na UNHCR ya kuhakikisha idadi ya wakimbizi 35,000 waliokuwa wamebaki katika kambi hiyo inamalizika na kambi hiyo kufungwa rasmi ifikapo Desemba, mwaka huu.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisi ya UNHCR nchini, ilieleza kuwa kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, Kanda ya Kaskazini Magharibi ya Tanzania, idadi ya wakimbzi imeendelea kupungua kutokana na mikakati iliyowekwa na serikali kwa kushirikiana na UNHCR huku makambi tisa yaliyokuwa katika mikoa ya Kigoma na Kagera yakiwa tayari yamefungwa.

Pia zaidi ya wakimbizi wa Kirundi 500,000 wameripotiwa kurudishwa nchini kwao katika kipindi cha takriban muongo mmoja uliopita kukamilisha operesheni ya kurudishwa kwa Warundi kufuatia kufungwa kwa kipengele cha kisheria cha wakimbizi hao hapa nchini.

Afisa Uhusiano Msaidizi Masuala ya Nje wa UNHCR nchini, Melanie Senelle, alisema mpango wa kuwarudisha wakimbizi hao unafanywa na shirika hilo kwa ushirikiano na serikali za Tanzania na Burundi, Kamati ya Kimataifa ya Uokozi, Shirika la Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Msalaba Mwekundu kutoka katika nchi hizo mbili.

Wakimbizi kutoka Burundi walianza kukimbilia nchini tangu miaka ya 1970 na kuendelea kuongezeka katika miaka ya 1990 kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa jumla ya wakimbizi 2,715 walioishi kwa muda mrefu wataendelea kuhifadhiwa nchini baada ya kuridhika na tathmini ya usaili kutoka kwa mwanchi mmoja mmoja kuhusu mahitaji ya ulinzi kwa idadi hiyo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment