Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, November 9, 2012

Moto wateketeza watoto watatu..!


Watoto watatu wa familia moja wamekufa kwa mkupuo baada ya nyumba walimokuwa wamelala kuteketea kwa moto katika kijiji cha Ilundo wilayani Rungwe.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa juzi usiku baada ya watoto hao kufungiwa ndani ya nyumba na mama yao mzazi, Sifa Asangwile (27) aliyewaacha na kwenda nyumbani kwao kumfuata mtoto mwingine aliyekuwa akishi na bibi yake.
Watu walioshuhudia tukio hilo walisema mama mzazi wa watoto hao alipomaliza kuandaa chakula cha usiku aliwafungia watoto hao na kuondoka kwenda nyumbani kwao ambapo ni jirani na nyumbani kwake kwa lengo la kumchukua mwanawe mwingine ili aje wale chakula pamoja.
Balozi wa eneo hilo, Andimile Gwabola alisema wakati mama huyo akirejea nyumbani aliiona nyumba yake ikiwaka moto na ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada.
Alisema majirani walijitokeza kwa wingi kutoa msaada na iliwabidi kuvunja ukuta wa upande mmoja wa nyumba hiyo ili kuokoa miili ya watoto hao.
“Tulipofika hapa tulikuta moto ukiwaka lakini tukashirikiana na vijana kumwagia maji upande huu (anauonyesha) na kisha kuvunja ukuta, ambapo tulifanikiwa kuitoa miili ya watoto wote watatu ikiwa imeungua vibaya,” alisema Gwabola.
Aliwataja watoto waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni George Nuru (9), Nevis Nuru (4) na Winfrida Nuru (2) wote wakiwa ni wakazi wa kitongoji cha Busweme kijiji cha Ilundo.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Crispin Meela ambaye alitembelea eneo la tukio kwa lengo la kuwafariji wafiwa, aliwataka wananchi wa eneo hilo kutohusisha suala hilo na jambo lolote na badala yake waviache vyombo vya dola vifanye uchunguzi wake.
“Tusije tukatufuta chanzo cha tukio hili wenyewe wala tusiongeze chumvi kwani kuna vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi na tutapewa taarifa punde uchunguzi huo utakapokamilika,” alisema Meela.
Meela aliwataka wananchi hao kuwa watulivu na kushirikiana katika kuisaidia familia ya wafiwa ili waweze kupata mahali pa kuishi kwa kuwa nyumba yao imeteketea kabisa kwa moto.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye kwa niaba ya Serikali alitoa Sh. 500,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba ya familia hiyo, pia aliongoza harambee ya kusaidia ujenzi huo, ambapo fedha taslimu na vifaa vya ujenzi vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. milioni 1.3 zilipatikana.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kiwira, Laurent Mwakalebule aliwataka wananchi wa eneo hilo kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu na kwamba atashirikiana nao kuhakikisha kuwa wafiwa wanajengewa nyumba mpya na kupata makazi salama ya kuishi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment