Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, November 9, 2012

Rais Kikwete azindua mradi wa gesi Dar..!



Rais Jakaya Kikwete (wa Pili kushoto)Makamu wa Rais,Dkt.Mohamed Gharib Bilal,(watatu kushoto) na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadick, (Kulia)

Pamoja na mvua kubwa kuendelea kunyesha, maelfu ya wananchi jijini Dar es Salaam, walifurika kushuhudia uzinduzi wa mradi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya kusafisha na kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam, uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete.
Mradi huo unaogharimu kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 sawa na fedha za Kitanzania Sh. trilioni 1.6 ulizinduliwa na Rais Kikwete katika eneo la Kinyerezi Manispaa ya Kinondoni, mahali ambapo mitambo ya gesi hiyo itakapojengwa.
Rais Kikwete katika hotuba yake kabla ya kuweka jiwe la msingi, alieleza historia ya mradi huo na jinsi alivyopingwa na baadhi ya watu aliowaita yeye mwenyewe kwa majina ya ‘wazito’ au ‘vigogo’ waliowahi kumshauri na kumwandikia barua za kumuomba aachane na mradi huo kwa kuwa ungeigharimu serikali na nchi kwa ujumla.
“Wazo la kuanzisha mradi wa umeme unaozalishwa kwa nguvu za gesi nilianza nalo wakati ule nikiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini mwaka 1988 hadi 1992, lakini baadhi ya viongozi wazito kweli, vigogo waliupinga mradi. Wengine wameandika na barua zao zipo pale ofisini wakitoa maoni ya kupinga mradi huu, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu, nikawaambia wazee nashukuru lakini mimi naendelea,” alisema.
Miundombinu ya mradi huo inahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Mtwara na Lindi na pia ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha gesi asilia la inchi 36 kutoka Mkoa wa Mtwara kupitia mikoa ya Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam katika umbali wa kilometa 532.
Rais Kikwete aliitaja miradi mingine ambayo serikali inayo katika kukabiliana na matatizo ya umeme, kuwa ni pamoja na ule wa kuzalisha umeme kwa njia ya nguvu za upepo mkoani Singida, umeme kutokana na nguvu ya jua ambao kwa sasa upo katika hatua ya kumtafuta mwekezaji atakayejenga mitambo kuanza kuzalisha kiasi megawati 500 za umeme.
Miradi mingine ni pamoja na ile ya makaa ya mawe ya Kiwira, Mchuchuma, Ngaka pamoaj na madini ya Urani mkoani Ruvuma, akieleza kuwa Tanzania ni nchi ya saba duniani kwa kuwa na wingi wa madini hayo.
Alisema serikali haina nia ya kutumia madini hayo kutengenezea mabomu bali kuzalisha umeme na pia kuendeleza ile ya kutumia mbolea ya Kilwa Ammonia na Minjingu.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilali, mawaziri, mabalozi, wakuu wa mikoa, wabunge, wakurugenzi na wananchi kutoka vitongoji mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Rais Kikwete alimtaka mkandarasi kumaliza mapema mradi huo na katika viwango vilivyokubaliwa kati yao na Serikali ya Tanzania.
Naye Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, alisema rasilimali ya gesi iliyopo nchini ni takribani futi za ujazo trilioni 33 sawa na mapipa ya mafuta bilioni sita akiongeza kuwa gesi nyingi ipo baharini kwenye maji ya kina kirefu ambayo inakadiriwa kuwa na futi za ujazo trilioni 25.
Aliongeza kuwa iwapo kasi ya utafutaji na uchimbaji ikisimamiwa kwa uhakika, kwa upande wa Songosongo (Lindi) Mnazi Bay (Mtwara) na Ntorya (Ruvuma), kiasi cha gesi asilia kitakachozalishwa kina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya umeme nchini wa megawati 2,780 kwa miaka 35 hadi 89 iwapo utatumiwa wa futi za ujazo miliomi 400 kwa siku.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuleta maendeleo makubwa ya kiuchumi hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuinua hali ya maisha ya Watanzania, kukuza sekta ya viwanda, kuokoa kiasi cha fedha nyingi zilizokuwa zinapotea kutokana na kununua nishati ya mafuta kutoka nje na kuongeza pato la taifa kwa kuiuza gesi hiyo kwa nchi jirani na kulinda misitu iliyokuwa inapotea kwa kukatwa kwa matumizi ya kuni na mkaa ambapo kwa mwaka taktibani hekta laki nne ya misitu huteketea.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment