Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, November 5, 2012

Wabunge: Tunasubiri..!

Wasema isipowasilishwa wataangalia hatua za kuchukua
Spika Anne Makinda
Wakati kukiwa na utata wa kutowasilishwa Bungeni ripoti ya Kamati ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, wabunge wamekuja juu na kueleza kuwa kama haitawasilishwa wataangalia hatua za kuchukua kwani kuifanya kuwa siri kutazua maswali mengi na kuwaathiri kwa wabunge waliotuhumiwa kwa rushwa.

Ripoti hiyo inasubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania ili kuweka mambo hadharani kuhusu wabunge wanaotuhumiwa kuhongwa na makampuni ya mafuta ili wakwamishe Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha wa 2012/13 na kuwajibishwa kwa viongozi wandamizi wa wizara hiyo.

Wanaodaiwa kutakiwa kuwajibishwa ni Waziri wa wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofaut jana, wabunge ambao walikuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika Anne Makinda, walisisitiza kuwa ripoti hiyo iwasilishwe na kujadiliwa Bungeni ili kumaliza ubishi na kama kuna watu wa kufa ijulikane kuliko kuendelea kuificha.

DAVID SILINDE

Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, alisema kuna umuhimu wa kuwasilishwa kwa ripoti hiyo Bungeni ili kila mtu ajue ukweli wa tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge waliotuhumiwa, lakini ikifanywa siri, kuna athari kubwa kwa Bunge na kwa jamii.

Alisema kama haitawasilishwa wananchi watahoji kwamba Wabunge wakituhumiwa kwa rushwa na kuundiwa kamati, ripoti haziwekwi wazi kwa jamii kama ilivyo kwa kamati nyingine zinazoundwa na serikali ambazo zimekuwa zikiwekwa wazi.

“Kwa kuwa mwenye mamlaka ya kuruhusu kuwasilishwa kwa ripoti hiyo ni Spika wa Bunge, kwa hiyo kama haitawasilishwa nadhani wabunge wataona hatua za kuchukua, lakini kwanza tutaendelea kumuomba Spika akubali iwasilishwe Bungeni kumaliza kiu ya Watanzania,” alisema Silinde.

YUSUFU NASSIR


Mbunge wa Korogwe Mjini (CCM),Yusufu Nassir, alisema Spika anatakiwa atumie busara zaidi kukubali ripoti hiyo kuwasilishwa Bungeni ili kuwatendea haki wabunge na watendaji wa serikali ambao walituhumiwa kupewa rushwa.

Nassir alisema hofu inayodaiwa kuwepo kuwa kama itawasilishwa pengine italeta athali kwa chama tawala na serikali haina msingi kwa sababu suala la uadilifu siyo la chama kwani kama mbunge alipokea rushwa ni utashi wake mwenyewe na siyo chama tawala.

“Sheikh akifumaniwa ni yeye, haina maana kuwa msikiti mzima unakuwa umefumaniwa, hizo ni hisia tu, jambo la msingi ni je, wewe ulihusika na kupokea rushwa?” alihoji na kuongeza:
 “Maana katika Wabunge waliotuhumiwa hawapo chama tawala pekee bali pia wapo wa vyama vya upinzani.”

CHARLES MWIJAGE

Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage, alisema Bunge linaongozwa na Spika wa Bunge ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuamua kama ripoti hiyo iwasilishwe au isiwasilishwe.

Alisema athari za kutokuwepo kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliyovunjwa kwa tuhuma za rushwa zimeanza kujitokeza ambazo ni pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta mara dufu na hivyo kuzua malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

“Watoe ripoti Bungeni wa kufa afe, lakini kama Spika ataamua isitolewe kwa sababu ana mamlaka hakuna wa kumuingilia, hatuwezi kufanya chochote hata kujinyonga hatuwezi,” alisema Mwijage ambaye aliongeza kuwa jimboni kwake mafuta yamefikia bei ya Sh. 4,000 kwa lita.

CATHERIN MAGIGE

Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Magige, alisema itakuwa vyema kama ripoti hiyo itawasilishwa kwani kuendelea kuifanya siri inawaweka njia panda Wabunge.

SELEMAN ZEDI

Mbunge wa Bukene (CCM) Seleman Zedi, alisema pamoja na kwamba katika ratiba ya vikao vya Bunge katika mkutano unaoendelea haionyesha kupangwa kuwasilishwa kwa ripoti hiyo,  bado wabunge wana matumaini kuwa itawasilishwa.

Zedi alisema Wabunge na Watanzania kwa ujumla wana kiu kubwa kutaka kujua ukweli wa yaliyoelezwa katika ripoti hiyo, hivyo hata kama haitawasilishwa katika mkutano wa sasa, watasubiri ujao.

OLE SENDEKA

Naye Mbunge wa Simanjiro (CCM) Christopher Ole Sendeka, alisema viongozi wakuu wa serikali wameonyesha nia ya kutaka ripoti hiyo iwasilishwe Bungeni, hivyo Wabunge wana matumaini itawasilishwa.

Oktoba 24 mwaka huu gazeti hili lilipowasiliana na Katibu wa Bunge, Dk.Thomas Kashililah, ambaye alisema Kamati  ya Uongozi ya Bunge ingekutana kujadili kama suala la kuwasilishwa ripoti ya kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali Mstaafu, Hassan Ngwilizi, liingizwe kwenye ratiba ya vikao vya Bunge kwa ajili ya kuwasilishwa na kujadiliwa.

Hata hivyo, ratiba ya mkutano unaoendelea haionyeshi kama ripoti hiyo itawasilishwa na kujadiliwa.

Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa ambazo zinaeleza kuwa huenda ripoti hiyo isiwasilishwe kabisa kujadiliwa Bungeni kutokana na baadhi ya mambo kutokuwa sawa baada ya kamati ya Ngwilizi kukamilisha uchunguzi wake.

Habari zinasema kuwa baada ya kukamilika kwa ripoti hiyo na kukabidhiwa kwa Spika Makinda Septemba 27, mwaka huu, yameibuka makundi mamwili yanayovutaka. Moja linaitetea serikali ili ripoti hiyo iisafishe na lingine linataka haki itendeke kwa ukweli kuwekwa wazi na kujulikana.

Kundi linalotaka haki itendeke linaamini kama kuna waliohongwa wajulikane na kama siyo kweli ukweli ujulikane kwa kuwa baadhi ya wabunge walilalamika na kutaka ripoti hiyo itolewe mapema kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano wa Nane wakisema kuwa bila hivyo watakutana na hali ngumu katika majimbo yao kwa kuwa wamevunjiwa haki zao.

Julai 28 mwaka huu wakati wa Bunge la Bajeti, Spika Makinda alivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kutokana na baadhi ya wajumbe wake kutuhumiwa kuhongwa na kampuni za mafuta nchini.

Kamati hiyo iliyovunjwa ilikuwa ikiundwa na wajumbe zaidi ya 20 ambao ni pamoja na Mwenyekiti wake, Selemani Zedi na Makamu mwenyekiti, Diana Chilolo, Profesa Kulikoyela Kahigi, Yusufu Haji Khamisi, Mariam Kisangi, Catherine Magige, Dk. Anthony Mbassa, Abia Nyabakari, Charles Mwijage, Yusufu Nassir, Christopher Ole Sendeka na Dk. Festus Limbu.

Wajumbe wengine waliokuwamo katika kamati hiyo iliyovunjwa kwa tuhuma za rushwa ni Shafin Sumar, Lucy Mayenga, Josephine Chagulla, Mwanamrisho Abama, David Silinde, Suleiman Masoud, Kisyeri Werema Chambiri, Munde Abdallah, Sara Msafiri, Vicky Kamata na Ali Mbaruk Salim.

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliwataja kwa majina wabunge wenzake kwamba wamehusika katika kupokea rushwa.

Kuvunjwa kwa Kamati ya Nishati na Madini kulifuatia baada ya  Mbunge  wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa, kuomba Mwongozo wa Spika, akitaka jambo hilo lijadiliwe na Bunge na kupendekeza kuwa Kamati za Bunge zinazotuhumiwa kwa rushwa zivunjwe.

Bunge lilikubali kuivunja na kuiunda upya Kamati ya Nishati na Madini na kamati na baada ya hoja hiyo kuungwa mkono, Spika Makinda aliikubali  hoja hiyo na kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na Madini.

Baadaye Spika Makinda aliunda kamati ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ambayo Mwenyekiti wake ni Ngwilizi. Wajumbe wengine ni John Chiligati (Manyoni-CCM); Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Riziki Omary (Viti Maalum-CUF) na Said Arfi (Mpanda Mjini-Chadema).

Wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, baadhi ya wabunge walidai kuwa kuna wenzao wamehongwa na kampuni za mafuta ili kushinikiza Waziri Muhongo na Maswi, wang’olewe katika nafasi zao kwa kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment