Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, January 30, 2013

LULU AREJEA URAIANI HUKU AKIBUBUJIKWA NA MACHOZI...!


HATIMAYE msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia amerejea uraiani jana baada ya kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Lulu anakabiliwa na shtaka la kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu. Aliachiwa kwa dhamana jana saa 9:56 alasiri, baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa ametimiza masharti. Hadi anaachiwa kwa dhamana jana saa 9:55 alasiri, msanii huyo alikuwa ameshakaa mahabusu kwa miezi tisa, tangu alipokamatwa kwa tuhuma hizo, Aprili 7, 2012.

Aliachiwa baada ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Francis Kabwe kukagua na kuridhishwa na nyaraka muhimu zilizohitajika kama sehemu ya masharti ya dhamana na kutoa amri kwa msanii huyo kuachiwa huru kwa dhamana.

Dhamana hiyo ilitolewa juzi lakini msanii huyo hakuweza kutoka gerezani kutokana na Msajili wa Mahakama aliyepaswa kuthibitisha vielelezo vya dhamana hiyo kutokuwepo mahakamani.

Akizungumza huku akitokwa machozi muda mfupi baada ya kuachiwa, Lulu alimshukuru Mungu, mawakili wake na watu wote waliokuwa wakimwombea katika mapito yake hayo.

“Nawashukuru watu wote. Watu waendelee kuniombea, hii ni dhamana tu lakini kesi bado ni safari ndefu. Nawashukuru watu wote waliokuwa pamoja nami, namshukuru Mungu kwani yeye ndiye kila kitu,” alisema Lulu.

Mmoja wa mawakili wake, Peter Kibatala aliishukuru Mahakama kwa ushirikiano katika kufanikisha dhamana hiyo... “Sisi mawakili pamoja na Lulu mwenyewe tunaishukuru sana Mahakama kwa kufanikisha haki hii ya msingi. Msajili ametusubiri hadi sasa na hatimaye mchakato huu umetimia.”


Hali ilivyokuwa mahakamani

Lulu aliwasili mahakamani hapo saa 7:58 mchana akiwa kwenye gari la Jeshi la Magereza aina ya Landrover chini ya ulinzi.

Alipofikishwa, alipelekwa katika mahabusu na baada ya takriban saa moja, aliingizwa katika Ofisi ya Naibu Msajili, Kabwe huku akiambatana na wakili wake, Wakili wa Serikali, Joseph Maugo, wadhamini wake wawili na askari Magereza.

Kabwe alipitia masharti yote ya dhamana ikiwamo wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh20 milioni kila mmoja. Bondi hiyo iliwekwa na Florian James Mutafungwa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Dk Verusi Mboneko Kataruga wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Saa 9:26 alasiri alitoka katika ofisi hiyo na kurudishwa mahabusu ya mahakama hiyo kwa ajili ya kukamilisha taratibu nyingine za kimahakama na za Jeshi la Magereza na baadaye aliingizwa masjala ya makosa ya jinai kwa ajili ya kusaini hati ya dhamana.


Baada ya hapo, alitoka nje ya masjala hiyo na kutoa shukrani kwa waandishi wa habari, ndugu na jamaa waliojitokeza mahakamani kisha kuondoka mahakamani hapo kwa gari aina ya Toyota Landcruiser.

Lulu anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, Aprili 7, 2012, nyumbani kwake (Kanumba), Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.Picha zaidi angalia hapa chiniDr. Cheni ( Big Brother wa LULU) amekuwa mstari wa mbele toka mwanzo hadi leoHapa LULU akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuwa huru, Dr Cheni na mama LULU walikuwa karibu naeOMG..... Familia ni kitu kingine , Mama na LULU akikumbatiana na Mwanawe huku wakilia kwa furahaWakili wake akiongea na wanahabariLULU aliondoka na gari hii kuelekea nyumbani

Habari na James Magai na Vicky Kimaro Chanzo - Mwananchi
Picha - kishymba blog

No comments:

Post a Comment