Idadi ya watahiniwa waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana imeongezeka kwa kati ya asilimia 20 na 23 baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kufanya marekebisho alama za viwango vya ufaulu, Mwananchi limebaini.
Habari ambazo gazeti hili imezipata zinasema matokeo hayo ambayo yamewezesha kiwango cha ufaulu kupanda na kufikia asilimia kati ya 54 na 57, huenda yakatangazwa wiki hii pamoja na yale ya kidato cha sita ambayo pia yamechelewa kutangazwa.
Chanzo cha habari kutoka Necta kimesema matokeo hayo mapya yanaonyesha kuwa, ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi la nne umeongezeka kutoka asilimia 34.5 kwa matokeo yaliyotangazwa awali na huenda yakafikia asilimia 57. Hii inamaanisha kwamba watahiniwa wapatao 82,000 ambao awali walikuwa wamepata sifuri katika matokeo ya awali sasa wamepanda na kupata madaraja ya ufaulu katika matokeo mapya.
Kwa matokeo hayo, watahiniwa wa mwaka 2012 watakuwa wamefanya vizuri kuliko wa mwaka 2011, ambao watahiniwa 225,126 sawa na asilimia 53.37 ya 349,390 waliofanya mtihani huo walifaulu.
Msemaji wa Necta, John Nchimbi alisema upangaji wa matokeo hayo ulikuwa bado unaendelea. “Ninachojua kwa sasa ni kuwa mchakato unaendelea na matokeo yatatangazwa mapema tu ili watoto waweze kujiunga na shule mapema,” alisema Nchimbi.
Pia alisema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha sita umekamilika.
Matokeo ya awali
Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa yalionyesha kuwa kati ya watahiniwa 367,756 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, waliokuwa wamefaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa 126,847 sawa na asilimia 6.4. Waliopata daraja la nne walikuwa ni 103,327 sawa na asilimia 28.1.
No comments:
Post a Comment