NI
wazi sasa, inaonekana ulimi umemponza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, baada
ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kuendesha kazi ya
kukusanya saini za watu mbalimbali ili kumwajibisha. Kituo hicho
kimesema hadi jana, kilikuwa kimekusanya saini 1,000 za watu mbalimbali
ambazo zinamtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kufuta kauli yake aliyoitoa
bungeni wiki iliyopita.
Wiki
iliyopita, Pinda alitoa baraka zote kwa Jeshi la Polisi nchini kutumia
nguvu dhidi ya watu wote wanaovunja amani na utulivu, wakati akijibu
maswali ya papo kwa papo mjini Dodoma.
Katika kauli yake, alivitaka vyombo vya ulinzi, hasa Jeshi la Polisi
kuwapiga watu watakaokaidi au kupinga amri halali zinazotolewa na vyombo
hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi
wa LHRC, Dk. Helen Kijo Bisimba, alisema kamwe hawakubaliani na kauli ya
Pinda, kwa sababu haifuati haki za binadamu.
Alisema ni aibu kauli hiyo kutolewa na kiongozi wa juu serikalini, kwani
inaonyesha wazi imevunja Katiba, sheria na misingi ya haki za binadamu.
Alisema Pinda, hatafuta kauli yake au kuomba radhi Watanzania, wao kama
kituo watajua njia gani ya kufanya ili kulinda maisha ya Watanzania.
Alisema katika saini hizo, kituo chake kimezipokea kutoka maeneo
mbalimbali, yakiwamo ya Kinondoni (Dar es Salaam), Chato, Biharamulo
(Kagera), Temeke (Dar es Salaam).
Alisema mpaka jana, wananchi wengi wanaendelea kutuma saini zao kwa njia ya mtandao.
“Tunamtaka Waziri Mkuu Pinda, afute kauli yake aliyoitoa bungeni
kubariki polisi kupiga raia katika mkutano huu wa Bunge la Bajeti au
aombe radhi kwa Watanzania kwa kile alichokisema bungeni.
“Tunapenda kumkumbusha, utawala wa sheria unajumuisha serikali, vyombo
vya utekelezaji na ulinzi pamoja na wananchi kuheshimu sheria na si
kuvunja sheria…tamko hili limetoa mwanya mkubwa wa nguvu kwa vyombo vya
usimamizi wa sheria kuvunja haki za raia.
“Hali hii ni ya kushtusha kwenye nchi yenye utulivu na amani na kama
tunavyopenda kusema kisiwa cha amani, kiongozi huyu wa ngazi za juu
anatoa tamko linaloashiria kutoa ruksa kwa Jeshi la Polisi kuvunja tena
sheria, tunasema hatukubaliani nalo kamwe,” alisema Dk Bisimba.
Alisema katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matukio mengi ya
ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa yale yanayotokana na vyombo vya dola
na Jeshi la Polisi, kwa kupiga na kuua watu kwa risasi za moto.
Waziri Pinda alitoa kauli hiyo bungeni, alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), aliyetaka kujua hatua
zinazochukuliwa na serikali kutokana na matukio ya vurugu mara kwa mara
nchini, hususani katika mikoa ya Mtwara na Arusha.
Katika swali hilo, Pinda alijibu: “Na mimi nasema wanaokaidi amri halali
ya Jeshi la Polisi muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine ya
kupambana na wakaidi zaidi ya kuwapiga”.
Kauli hiyo, pia ilipingwa vikali na Jaji mstaafu, Mark Bomani, ambaye
alisema kutumia vyombo vya dola kudhibiti au kupiga watu kama
ilivyoamuliwa na Pinda, haikubaliki.
habari NA ADELINA RUTALE, DAR ES SALAAM
chanzo - mtanzania
No comments:
Post a Comment