UAMUZI wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kukataa kuwasilisha ushahidi wa mauji ya mlipuko wa bomu uliotokea
jijini Arusha, umeliweka njia panda Jeshi la Polisi na hivyo kushindwa
kuchukua hatua.
Licha ya jeshi hilo kumhoji Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na
kumtaka awasilishe ushahidi huo, kiongozi huyo amekataa agizo hilo
akisema kuwa wamekubaliana kuutoa ushahidi huo kwa tume huru ya majaji
endapo Rais Jakaya Kikwete ataiunda kama walivyomuomba.
Chanzo chetu ndani ya jeshi hilo, kimedokeza kuwa msimamo huo wa CHADEMA
umeliweka njia panda na hivyo kushindwa kuchukua hatua za kuwabaini
watuhumiwa wa tukio hilo na kuwafungulia mashtaka kutokana na
mkanganyiko wa taarifa zinazotolewa.
Jeshi hilo linadaiwa kuwa awali lilitaka kujiegemeza kwenye kauli za
kisiasa za baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali
ili kuonyesha kuwa CHADEMA ilisababisha mlipuko huo yenyewe kwa ajili ya
kuwahadaa wafuasi na kujitafutia umaarufu.
Hata hivyo, mbinu hiyo ya kutaka kuwasakama baadhi ya viongozi na
wafuasi wa CHADEMA inadaiwa kufifishwa na tamko la Mbowe pamoja na
mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwamba chama kina ushahidi
unaoonyesha kuwa tukio hilo lilifanywa na polisi.
“Hapa kuna mkanganyiko hasa baada ya Mbowe kudai wanao ushahidi wa video
ya tukio hilo. Wakubwa wetu wamegawanyika na kujikuta wakitoa kauli za
kukinzana maana wanahofia wakiwafungulia kesi watu wengine mashtaka
halafu CHADEMA ikaonyesha ushahidi tofauti itakuwa ni aibu,” kilisema
chanzo chetu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, jeshi hilo mkoani Arusha lilikuwa
limewakamata watu wawili raia wa kigeni likiwatuhumu kuhusika na mlipuko
huo lakini baada ya Mbowe kugoma kupeleka ushahidi huo, watuhumiwa hao
hawakuweza kufunguliwa mashtaka.
Pia katika hali ya kushangaza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo,
alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa makachero wa Taasisi ya
Uchunguzi ya Marekani (FBI) wamefika mkoani Arusha kuchunguza jambo
hilo.
Hata hivyo taarifa kutoka ubalozi wa Marekani zilikana FBI kuingia
nchini kuchunguza jambo hilo hivyo kusababisha mkanganyiko wa tukio hilo
lililovuta hisia kubwa ndani na nje ya nchi.
CHADEMA mara kwa mara imekuwa ikilituhumu jeshi la polisi na makada wa
CCM kuendesha harakati za kukidhoofisha kwa kutumia matukio mbalimbali
yanayofanywa na chama hicho cha upinzani.
Mmoja wa viongozi wa CHADEMA ameliambia Tanzania Daima, kuwa polisi
walikuwa wamepanga kuwatumia FBI kuuhabarisha umma kuwa CHADEMA
ilihusika na ulipuaji huo bomu lakini kutokana na mazingira yaliyopo
wameshindwa kutekeleza uovu huo.
“Unajua hila za polisi na CCM kila siku zinabadilika lakini kwa bahati
mbaya hawajui kuwa wananchi wanajua kinachofanyika, kuna askari
hawaridhiki na uovu unaofanywa na wenzao,” alisema kiongozi huyo.
Tanzania Daima, iliwasiliana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Robert Manumba, kuhusu sakata hilo ambapo alikataa kulizungumzia akidai
msemaji wa jeshi hilo Advera Senso anayo majibu.
Hata hivyo Senso hakuwa tayari kulizungumzia akisema kuwa alikuwa eneo
baya na akitoka eneo hilo angelijulisha gazeti hili lakini mpaka
tunakwenda mitamboni hakutimiza ahadi hiyo.
Mlipuko huo ambao ulisababisha vifo vya watu wanne na wengine zaidi ya
60 kujeruhiwa, ulitokea Juni 15 mwaka huu wakati wa kuhitimisha kampeni
za uchaguzi mdogo wa madiwani jijini humo, zikiwa zimepita dakika chache
baada ya Mbowe kumaliza kuhutubia na kutelemka katika jukwaa
lililokokuwa limeelekezwa bomu hilo.
Siku moja baada ya tukio hilo, serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ilitoa
taarifa tata bungeni ikionyesha kulikingia kifua jeshi la polisi na
kuwatwisha lawama viongozi wa CHADEMA.
Lukuvi alisema kuwa mkutano wa CHADEMA ulikuwa na ulinzi wa polisi wenye
magari mawili waliosimama upande wa kaskazini ya uwanja na mrushaji wa
mlipuko huo akiwa upande wa mashariki ya uwanja huo na kurusha kuelekea
magharibi.
“Jaribio la askari kutaka kumfuata aliyerusha mlipuko huo zilizuiliwa na
makundi ya wananchi ambao walianza kuwashambulia askari kwa mawe na
kuwazomea na hivyo polisi kulazimika kuanza kujiokoa badala ya kumsaka
mhalifu huyo.
“Hivi karibuni zimekuwepo jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya
siasa, makundi ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki ya raia
dhidi ya vijana wetu wa polisi, kuwafanya raia wawachukie, wasiwaamini,
wasiwape ushirikiano na kuifanya nchi isitawalike,” alisema Lukuvi.
Aliliongeza kuwa kufanikiwa kutoroka kwa mhalifu wa tukio hilo ni
matokeo ya uchochezi unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wanasiasa
dhidi ya serikali na polisi na hivyo kuwafanya wananchi wajenge chuki
dhidi ya polisi.
Siku chache baadaye viongozi wa CCM pamoja na baadhi ya mawaziri kana
kwamba wanafahamu mlipuaji wa bomu hilo, waliitwisha lawama CHADEMA
wakidai ilihusika na tukio hilo ingawa hadi leo hakuna aliyehojiwa na
polisi kati yao kuthibitisha tuhuma hizo badala yake Mbowe pekee ndiye
anaandamwa awapelekee ushahidi.
Makada hao ni Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba, na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, ambao walidai kuwa CHADEMA ndiyo imekuwa
ikihusika na vurugu zote zinazohusisha mauaji nchini.
Kauli za viongozi hao zilitplewa baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu
(NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye,
kudai kuwa wanao ushahidi wa kutosha kuwa CHADEMA iliandaa na kuratibu
shambulio hilo.
“Ni lazima tuwaze na kuvuka mipaka, kuna mambo ambayo yanawezekana
kabisa yakawa yamejificha pale. Watu wanaangalia, wanaojitoa ufahamu
wanafikiria CCM inaweza kushiriki.
“Mimi niwaambie CCM hata bila kushiriki ni moja kwa moja inawekwa kwenye
lawama jambo kama hilo likitokea. Ila CCM haina ushiriki katika jambo
kama hili kwa sababu ndio watu wake kupitia serikali yake wanatakiwa
kuwahakikishia usalama,” alisema.
Mwigulu ambaye pia ni mbunge wa Iramba Magharibi aliongeza kuwa hata
video ya mauji ya Arusha iliyowekwa kwenye mtando wa You tube inaonesha
wazi kuwa yalipangwa.
“Yule aliyekuwa anachukua video eti hakushtushwa kabisa na lile bomu,
aliendelea kufuatilia kama vile ni mkanda wa harusi. Iliwahi kutokea
wapi mchukua video kwenye mkutano wa hadhara kitu ambacho hakikupangwa
kimelipuka, kinaua watu, yeye anendelea kama anachukua send off?”
alihoji.
Ghasia naye alidai kuwa CHADEMA wamechochea vurugu Mtwara, Mwanza,
Mbeya, Morogoro na sasa Arusha ili maeneo hayo yasipate maendeleo.
Kutokana na mlipuko huo, CHADEMA ilitangaza kuanza mpango wa kutoa
mafunzo kwa vijana wake kwa ajili ya kulinda mikutano na viongozi wake
lakini CCM, polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa,
walikionya chama hicho wakidai kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria za
nchi, Katiba na sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.
Hata hivyo hoja zao zilipingwa vikali na baadhi ya wadau wa siasa na
wananchi wakihoji walikuwa wapi kwa kutoionya CCM ambayo ina kikundi cha
vijana cha Green Guard ambacho kinapewa mafunzo ya kijeshi na matumizi
ya silaha za moto.
Julai 17 mwaka huu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini,
alimwandikia Mbowe barua na kumwamuru awasilishe ushahidi wa video
aliyodai kuwa nayo ikiwaonesha baadhi yao walivyoshiriki kwenye tukio la
mlipuko wa bomu Arusha kabla ya Julai 23 mchana saa nane.
Katika hatua ya kuchanganyana, jeshi hilo Juni 20 mwaka huu, kupitia kwa
Mkuu wa Mafunzo na Operesheni, Paul Chagonja, aliwaeleza wanahabari
kuwa Mbowe anapaswa kuwa mkweli na kuacha kuuchezea umma kwa
alichowaeleza polisi ni tofauti kwani hana ushahidi huo.
Lakini katika hatua ya kushangaza Chagonja huyo huyo ndiye amemwamuru
Mbowe kupeleka tena ushahidi huo polisi akitamba kuwa baada ya kukaidi
kufanya hivyo, polisi inao makachero wake wanaojua jinsi gani ya
kuendelea na kazi hiyo.
Pamoja na polisi kudai Mbowe hana ushahidi, Julai 10 mwaka huu usiku wa
manane askari kadhaa wakiwa na silaha walifika nyumbani kwake wamkisaka
bila mafanikio wakitaka awapatie video hiyo.
Hata hivyo, kesho yake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius
Wambura, alidai hana taarifa za askari wake kufika nyumbani kwa Mbowe.
Muda aliopewa Mbowe umemalizika bila kuwasilisha ushahidi huo, akidai
kuwa hawezi kwenda kinyume na msimamo wa chama kwani jeshi hilo ni
watuhumiwa kwenye tukio hilo la Arusha.
Juzi jeshi hilo lilimtaka Mbowe kuwasilisha msimamo huo wa utetezi wake
kwa maandishi leo ambapo kiongozi huyo wa upinzani alisema mwanasheria
wa chama hicho ataandaa maelezo hayo.
Chanzo - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment