MLIMA mrefu kuliko
yote na wenye heshima kubwa dunia nzima na mlima unaoipatia serikali ya
Tanzania mapato makubwa sana kutokana
na watu wa ndani na nje ya Tanzania kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika,
mlima Kilimanjaro una urefu wa mita 5,895 (futi 19,340). Mlima Kilimanjaro wenye vilele
vitatu Kibo, Mawenzi na Shira. Mlima Kilimanjaro
umepoteza takribani asilimia 80 ya theruji yake kuanzia mwaka 1912 kutokana na
mabadiliko ya tabia nchi.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni Dodoma, na Naibu Waziri nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Mazingira), Ummy Mwalimu alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ole, Rajabu
Mbarouk Mohamed (CUF).
Mbunge huyo alitaka kujua kuwa tathmini inaonyesha ni kiasi gani cha theruji kilichopungua kutokana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi. Aidha katika swali la nyongeza Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, (CHADEMA), amesema wazee ambao wamepanda miti miaka 20 iliyopita wanakatazwa kukata miti yao kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Akijibu maswali
hayo kwa pamoja, Mwalimu amesema kulingana na jopo la wanasayansi wa mabadiliko
ya tabia nchi, Mlima wa Kilimanjaro umepoteza takribani asilimia 80 ya theruji
yake kuanzia mwaka 1912 kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema Serikali na Jumuiya za kimataifa zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali
katika kukabiliana na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni
pamoja na kusaini/kuridhia mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi wa mwaka 1992.
Ameongeza kuwa
Serikali ilisaini na kuridhia Itifaki ya Kyoto chini ya mkataba huo, kuandaa
sera, sheria na mikakati mbalimbali. Kwa upande wa wazee kunyimwa kukata miti yao, amesema ni kweli kuna changamoto
hiyo katika maeneo mbalimbali na kuwataka kufuata utaratibu ili kupata kibali
cha kukata miti.
No comments:
Post a Comment