Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, October 6, 2014

Uongozi wa gereza kuu la karanga mjini Moshi umetoa wito kwa wadau kuwatembelea maabusu na wafungwa

KILIMANJARO uongozi wa gereza kuu la Karanga mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, umetoa wito kwa wadau mbalimbali kujitolea misaada ya hali na mali  kwa ajili ya wafungwa na mahabusu, kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazosimamia jeshi la magereza nchini.

Wito huo umetolewa na mkuu wa gereza hilo kamishna msaidizi wa magereza (ACP), Hassan Mkwiche, alipozungumza na viongozi wa umoja wa wanawake wa CCM (UWT), wilaya ya Moshi mjini, waliofika kukabidhi misaada kwa ajili ya wafungwa na mahabusu gerezani hapo juzi.

Msaada huo ukijumuisha vyakula, sabuni, mafuta, nguo za wafungwa na watoto wa wafungwa na mahabusu, wenye thamani ya shilingi milioni moja, ulitolewa na UWT wilaya ya Moshi mjini, katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya UWT wilayani humo.

Kamishna Mkwiche alisema kuwa pamoja na kuwa suala la matunzo ya wafungwa na mahabusu linabaki kuwa jukumu la serikali, alishauri umuhimu wa raia kushirikiana na serikali katika kutoa misaada ya kiutu itakayowezesha walengwa hao kupata mahitaji muhimu na bora zaidi.

Aliwapongeza UWT wilaya ya Moshi kwa msaada wa hali na mali na kusema kuwa ni mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine kuweza kujitokeza kusaidia na kuongeza kuwa taasisi za dini nazo zimekuwa miongoni mwa taasisi  zinazojitokeza kusaidia kikamilifu wafungwa na mahabusu
gerezani hapo.

Awali akizungumza na wafungwa pamoja na mahabusu wanawake gerezani hapo, mwenyekiti wa UWT manispaa ya Moshi Lucresia Kundi, aliwataka kutokata tamaa kutokana na adhabu au makosa yanayowakabili, akisema bado wanao mchango mkubwa katika jamii.

Kundi alisema UWT manispaa ya Moshi, ilitambua  umuhimu wa kuwatembelea gerezani hapo, katika  maadhimisho hayo, ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuwafanya waliofungwa au mahabusu watambue jamii inawatambua na kuwathamini.

Katika kilele cha maadhimisho hayo ya wiki ya UWT, viongozi wa jumuiya hiyo, akiwemo katibu wake Shakila Singano, wajumbe wa kamati ya utekelezaji na baraza la UWT wilaya, waliongozana na mwenyekiti Kundi, kuwatembelea  wafungwa gerezani hapo.

Katika ziara hiyo, viongozi hao walipata fursa ya kuzungumza na wafungwa na mahabusu wanawake, ambao walionesha furaha kubwa ya kutembelewa na viongozi hao wa jumuiya ya CCM.

Kwa upande wao wafungwa na mahabusu wanawake, walitoa neno la shukrani kwa kunukuu maandiko ya biblia, hali ambayo iliwafanya viongozi wa UWT, kujikuta katika hali ya kutokwa na machozi.

No comments:

Post a Comment