Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, January 23, 2015

Uchumi Bank yafanikiwa kukopesha zaidi ya bilioni 12 kwa wateja wake

KILIMANJARO katika harakati za kuwakomboa wananchi kutoka katika lindi la umaskini, na hatimaye kuinua uchumi wao, benki ya Uchumi imetoa mikopo ya zaidi ya Shilingi Billioni 12 kwa wateja wake kwa kipindi cha miaka sita.

Mikopo hiyo iliyotolewa ilielekezwa katika sekta ya kilimo, ujenzi wa nyumba bora za kisasa, biashara, ujasiriamali na ada kwa wanafunzi wa shule za sekondari na wale walioko vyuoni.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Bw. Wilson Ndesanjo wakati akitoa salamu za benki hiyo, kwenye ibada yao ya shukrani ya kumshukuru Mungu kwa kuifanikisha benki huyo kwa kuweza kupiga hatua mbalimbali za kimaendeleo,ibada iliyofanyika katika Usharika wa Moshi Mjini Dayosisi ya Kaskazini.

Bw. Ndesanjo alisema benki hiyo imekuwa ikirudisha fadhila kwa wateja wake, kwa kutoa mikopo iliyoelekezwa katika sekta mbalimbali, pamoja na kutoa gawio kwa wale wote walionunua hisa katika benki hiyo.

Alisema benki hiyo inayomilikiwa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini imekuwa ikiwanufaisha wateja wake walioko katika mkoa wa Kilimanjaro na mikoa mbalimbali hapa nchini,kwa kuwapatia mikopo ambayo imewawezesha kupiga hatua mbalimbali za kimaendeleo.

‘Benki yetu ya Uchumi ilianzishwa kwa lengo la kutoa huduma bora za kibenki kwa watu wote pasipo kubagua rangi, udini na ukabilia, na kwa kulitimiza hilo kwa sasa benki imeunganishwa kwenye mtandao wa Umoja Switch, ambapo wateja wetu wote wanapata huduma za benki popote waliopo’alisema Ndesanjo

Alisema pamoja na kutoa huduma hizo kwa wananchi, pia benki imekuwa ikiinufaisha serikali kwa kulipa kodi stahiki kwa maendeleo ya Taifa, hivyo kutoa wito kwa wananchi wote kutumia huduma za benki hiyo ili waweze kunufaika zaidi na hatimaye waweze kukuza uchumi wao.

Bw. Ndesanjo alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mungu kwa jinsi ambavyo taasisi hiyo imekuwa ni taasisi ya kwanza ya kanisa kuweza kuongozewa ibada tangu Askofu Dkt Fredrick O. Shoo asimikwe kuwa Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Januari 11 mwaka huu, na kuwaomba watu wote wakiongozwa na viongozi wa dini kuendelea kuiombea benki hiyo ili iendelee kutoa huduma nzuri kwa wateja wao.

Katika ibada hiyo ya Shukrani, uongozi na wafanyakazi wa benki hiyo walitoa zaidi ya kompyuta yenye thamani ya shilingi milioni moja kwa usharika wa Moshi Mjini, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango mkubwa wa usharika huo wa kununua hisa kwa nyingi zaidi katika benki hiyo.

Akizungumza katika ibada hiyo Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo alisema Mungu na Kanisa limewekeza vitu vingi katika benki hiyo, hivyo kuwataka watenda kazi wote ndani ya benki hiyo kutenda kwa uaminifu wajibu wao ili benki iweze kukua zaidi.

Sambamba na hilo aliwataka watu kuacha desturi ya kuhifadhi fedha nyumbani ambako hakuna usalama, na kuwasihi kuwekeza katika benki hiyo ili waweze kupata faida na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.

Akishukuru kwa zawadi iliyotolewa na benki hiyo, Askofu Dkt. Shoo alisema mpaka sasa Usharika wa Moshi Mjini umeweza kununua hisa za zaidi ya shilingi milioni 50 katika benki hiyo, na kuahidi kuendelea kuwekeza zaidi katika benki hiyo.

Ibada hiyo hiyo ya shukrani iliyoongozwa na mchungaji kiongozi wa Usharika huo Leonce Shirima, ilihudhuria na Msaidizi wa Askofu wa dayosisi hiyo Mchungaji Elingaya Saria, Meneja wa kwanza wa benki hiyo Bw. Fuhanael Kihundrwa, Mwenyekiti wa kwanza wa bodi ya benki Dkt. Sadikiel Kimaro, watumishi toka ofisi kuu ya dayosisi wakiongozwa na katibu Mkuu Bw. Julius Mosi, meneja mkuu wa benki Bi. Anjela Moshi, mameneja, wakurugenzi na watumishi wa benki hiyo.

No comments:

Post a Comment