Na Makongoro Oging'
Mtoto Irene Adolf (12) (pichani), mkazi wa Chang’ombe Usalama, ambaye pia na mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi ya Ndarara wilayani Temeke jijini Dar, amefariki dunia baada ya kukosekana shilingi 350,000 za matibabu.
Kwa mjibu wa mama mzazi wa mtoto huyo, Blandina Benedicto (44), aliyezungumza na gazeti hili, Irene amefariki Jumanne wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokua amelazwa kutokana na figo zake kutofanya kazi.
Blandina alisema: “ ‘Kabla sijamfikisha hospitali yoyote marehemu alianza kuwa na tatizo la macho kuuma, nilimpeleka Hospitali ya Wilaya ya Temeke ambapo alipewa dawa ya matone hata hivyo haikusaidia, nikaenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Vipimo Muhimbili viligundua figo hazifanyi kazi hivyo zilihitajika kusafishwa na madaktari walisema kwamba mashine hiyo ya kusafisha figo haipo katika hospitali hiyo bali inapatikana katika hospitali binafsi na gharama yake nikaambiwa ni shilingi milioni moja.
“Nilikopa shilingi laki sita na nusu, nilipopeleka hospitali walikataa wakisisitiza kuwa lazima zifike shilingi milioni moja, nikiwa naendelea kutafuta lakini kabla sijafanikiwa mwanangu akafariki dunia akiwa ameshika Biblia, “ alisema mama huyo kwa huzuni.
No comments:
Post a Comment