Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Saturday, July 14, 2012

Dk SLAA ATINGA KORTINI MWENYEWE...!


Katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema)Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa zamani wa Arusha, Godbless Lema wakizungumza na Maofisa wa Polisi baada ya kuwasili kwenye ofisi za Makao makuu ya Jeshi hilo kwa mahojiano dhidi ya tuhuma za kutaka kudhuriliwa kwa viongozi hao jijini Dar es Salaam jana.Picha na Fidelis Felix
 Nora Damian na Ibrahim Yamola
 HATIMAYE Katibu Chadema, Dk Willibrod Slaa     amesalimu amri kwa Jeshi la Polisi baada ya kukubali wito wa kuhojiwa na jeshi hilo lenye dhamana ya usalama wa raia.Hata hivyo, baada ya kuripoti Dk Slaa aligoma kuandikisha maelezo ya tuhuma alizotoa hivi karibuni kwamba kuna njama zimepangwa kuwaua viongozi waandamizi wa Chadema akiwamo yeye mwenyewe.
Hatua aliyochukua jana Dk Slaa ni tofauti na aliyotoa siku chache zilizopita baada ya kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi kuagiza kwamba lazima viongozi hao wa Chadema wahojiwe na  polisi kutokana na madai yao kuwa wanataka kuuawa na mmoja wa kigogo wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Baada ya agizo hilo la Waziri Nchimbi, Dk Slaa alisema hatakwenda polisi, wakitaka polisi wakamkamate.
Alilitaka jeshi hilo litumie taarifa zake za kiintelejensia kubaini watuhumiwa waliowataja katika mkutano wa waandishi wa habari hivi karibuni.
Dk Slaa; "Kwani wao wanapozuia mikutano yetu kwa madai kwamba taarifa zao za kiintelejensia zinaonyesha kutakuwa na vurugu huwa tunauliza wamezitoa wapi?"
Jana, mtendaji huyo wa Chadema aliwasili Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam saa 4.30 asubuhi wakiwa katika gari la Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema na aliposhuka alisema ameamua kuitikia wito wa jeshi hilo.
“Siku zote wito lazima uitikiwe lakini, pia mtambue kuwa mjumbe huwa hauwawi,” alisema Dk Slaa huku akielekea ndani.
Dk Slaa na Lema waliitwa Makao Makuu ya Polisi kwa ajili ya kuandika maelezo kuhusu tuhuma walizozitoa hivi karibuni za kutaka kuuawa.
Pamoja na kuripoti polisi, Dk Slaa alikataa kuandika maelezo ya tuhuma alizotoa hivi karibuni kwamba kuna njama zimepangwa kuwaua viongozi waandamizi wa Chadema, akiwamo yeye mwenyewe.
Badala yake, amelitaka jeshi hilo kufanya kwanza uchunguzi wa malalamiko kadhaa ambayo amekuwa akiyatoa mara kwa mara kwa kuwa tayari ushahidi upo na umekamilika.
Akizungumza baada ya kutoka kuhojiwa, Dk Slaa alisema aliamua kwenda baada ya wito wa polisi na kwamba kuitikia wito ni jambo la kawaida.
“Tulichokataa ni kutoa statement (kuandika maelezo) wafanye upelelezi ni wajibu wao…, tunawalipa kwa kazi hiyo,” alisema Dk Slaa na kuongeza;
“Wana document (nyaraka) nyingi ndani ya ofisi zao hivyo warudi kwenye document zao.” alisisitiza.
Alisema alishatoa malalamiko mengi kama vile kukutwa na kinasa sauti ndani ya chumba chake na kwamba jina lake pia lilikuwapo kwenye orodha ya Mwakyembe (Dk Harrison).
“Tuna taarifa nyingi za polisi hivyo zifanyiwe kazi na sisi tutatoa ushirikiano,” alisisitiza.
Akifafanua juu ya wito huo, Wakili wa Dk Slaa, Dk Rugemeleza Nshalla alisema kuwa, mteja wake alikwenda Makao Makuu ya Polisi kutokana na taarifa walizokuwa wamezitoa kwenye vyombo vya habari hivi karibuni.
Akizungumzia kuhusu mteja wake kukataa kutoa maelezo, wakili huyo alisema badala yake wamekubaliana na jeshi hilo kwamba, wiki ijayo watapeleka maelezo waliyoyatoa wakati wa mkutano na waandishi wa habari ili yaweze kufanyiwa kazi.
Alivyoingia polisi
Wakiongozwa na askari wa Jeshi la Polisi ambaye hakuweza kufahamika jina lake, waliingia chumba namba 703 na ilipofika saa 4.38 asubuhi, walihamishiwa chumba namba 808 yalipofanyika mahojiano hayo.
Kadiri muda ulipokuwa ukiendelea, umati wa watu ukiongozwa na viongozi na wanachama wa chama hicho uliendelea kuongezeka katika ofisi hizo za polisi.
Ilipofika saa 6:28 mchana viongozi hao wa Chadema walitoka nje kuashiria kuwa zoezi hilo lilikuwa limekamilika.
Dk Slaa alisema; "Tumefika hapa na tumekataa kutoa maelezo kwani tuhuma walizonazo ni nyingi na hawajazifanyia kazi."
Aliongeza, “Tumewaambia watumie mkanda au maelezo ambayo tuliyatoa kwa waandishi wa habari wiki hii ili kufanyia uchunguzi.”
Dk Slaa alidai kuwa miaka minne imepita tangu Jeshi la Polisi lilipochukua vinasa sauti walivyovikuta katika chumba alichokuwa analala mjini Dodoma wakati wa Bunge, lakini hakuna kinachoendelea.
“Hawa ambao leo (jana) wanataka kuchukua maelezo yangu, miaka minne imepita hawataki kutoa taarifa juu ya vinasa sauti nilivyowakabidhi. Kuna haja ya kutoa maelezo tena,” alisema Dk Slaa.
Kauli ya Jeshi la Polisi
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, Dk Slaa na Lema walipelekewa hati ya wito wa kwenda polisi kuandika maelezo.
“Tumewaita kwa hati maalumu  waje watupe maelezo yatakayotusaidia kuendelea na uchunguzi, siku za nyuma viongozi hawa walitoa malalamiko kwamba wanataka kuuawa, hivyo Jeshi la Polisi tumepokea malalamiko na kuanza kuyafuatilia,” alisema.
Alisema jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi kufuatilia tuhuma hizo na kwamba watakapokamilisha uchunguzi, watapeleka jalada kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Madai ya Chadema
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika mapema wiki hii jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman  Mbowe alitaja majina ya baadhi ya maofisa idara hiyo  (majina tunayo), akidai mmoja kati yao anaratibu shughuli hiyo na tayari yupo mjini Dodoma kwa ajili ya kuongozi kundi linalotaka kumdhuru Mbunge wa Ubungo John Mnyika.
Akiendelea kutoa tuhuma hizo, Mbowe alidai kwamba idara hiyo ambayo haifanyi shughuli za siasa, inatumia ofisi vibaya kwa kufuatilia viongozi hao wakidhani chama hicho kina mambo ya siri  kinayotaka kuyafanya katika nchi hii
"Sisi Chadema hatuna mambo ya siri tunayotaka kufanya katika nchi hii. Matatizo ya Watanzania yapo wazi na yanajulikana na kila mmoja na kinachotakiwa ni Serikali ya CCM kutekeleza sera na ahadi walizotoa kwa wananchi na si vitisho, "alisema Mbowe.
Dk Slaa alisema ofisi yake imepokea madai mengi kutoka kwa viongozi na wananchama ya kutendewa visivyo haki na kuwasilisha taarifa katika jeshi hilo, lakini hakuna dai hata moja lililofanyiwa kazi.

No comments:

Post a Comment