Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama
kawaida na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimedhibiti hali ya
ulinzi na imeimarishwa katika maeneo yote ya Zanzibar.
Taarifa
ya Serikali iliyotolewa leo usiku na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed ( pichani) amesema Zanzibar bado
ni shwari na inaendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu.
Akizungumzia
tukio la vurugu zilizofanywa na wananchi wachache, Waziri Mohamed Aboud
alisema vikundi vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh
Farid Hadi walifanya vurugu hizo katika mitaa ya Darajani, Michenzani,
Muembeladu,Magomeni,Amani wakidai Sheikh wao haonekani na kudhani
amekamatwa na vyombo vya Dolan a kuwekwa ndani.
Waziri
Mohamed Aboud alisema Serikali imewasiliana na vyombo vya Dola ikiwemo
Polisi,Jeshi la wananchi wa Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa, Vikosi
vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,KMKM,JKU,Chuo cha Mafunzo,Zimamoto na
Valantia ambapo vyombo vyote hivyo vimeeleza kutoelewa chochote kuhusu
Sheikh Farid.
Waziri
huyo alisema kwamba Jeshi la Polisi limepokea taarifa ya kutoonekana
kwa Sheikh Farid ambapo kwa sasa Jeshi hilo linaendelea kumtafuta na
kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo ili kupata ukweli wake na kuchukua
hatua zinazofaa.
Alisema
kwamba wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wake, wananchi
wameombwa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa vituo vya Polisi au
kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na Mikoa katika maeneo yao.
Waziri
Mohamed Aboud amesema Serikali inawasihi wwananchi waache kujiingiza
katika vitendo vya fujo na vurugu kwani kutenda hivyo ni kosa kwa mujibu
wa sheria na Serikali haitovumilia vitendo hivyo.
Katika
tukio la leo mchana, vijana hao wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh
Farid Hadi walifanya vitendo vya vurugu ikiwemo kuchoma moto Maskazini
za CCM,kuvunja maduka,kupora mali za watu na kuharibu miundombinu ya
barabara na kusababisha hasara kubwa.
No comments:
Post a Comment