Na Martin Malera
SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi Makao Makuu na Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam kutoa kauli tata kuhusu uchunguzi wa tukio la kutekwa,
kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka,
mtuhumiwa pekee katika kesi hiyo hadi sasa, raia wa Kenya, Joshua
Mulundi, ameibuka na kutoa kauli na siri nzito ya tukio hilo.
Mtuhumiwa huyo ambaye yuko mahabusu, ameliambia gazeti hili kuwa anataka
upelelezi wa kesi yake ukamilike haraka ili atendewe haki, lakini kubwa
kuliko yote ameitaka serikali imlete Dk. Ulimboka mahakamani ili aweze
kumtambua.
Akizungumza kwa kificho kwa njia ya simu kutoka ndani ya Gereza la Keko
alikohifadhiwa, raia huyo wa Kenya alisema ameamua kutoa kauli hiyo
baada ya kusoma taarifa ya gazeti hili juzi ilikionesha polisi
wakirushiana mpira na kutoa kauli zinazopingana kuhusu tukio la Dk.
Ulimboka.
Alisema hadi sasa haoni maendeleo ya kesi hiyo kwani kila ikifika
mahakamani, upande wa mashitaka hutoa hoja ya kutaka iahirishwe kwa
madai kuwa upelelezi haujakamilika.
“Kila ninapoenda mahakamani naiomba mahakama imlete Dk. Ulimboka
anitambue, nahoji kwanini upelelezi haujakamilika. Kwa bahati mbaya sana
siku hizi kesi hii inapokuja mahakamani, hata vyombo vya habari
havijulishwi. Nashukuru Mungu nimepata namba zenu za simu kutoka kwenye
gazeti lenu ili nitoe ya moyoni...
“Naomba Dk. Ulimboka aletwe mahakamani ili anitambue, kama atasema mimi ndiye niliyemteka na kumtesa, basi kesi iendelee na sheria ichukue mkondo wake, kama atasema sikuhusika, basi kesi iishe maana sioni sababu ya mimi kuteseka hapa gerezani kwa kusubiri upelelezi ambao haujulikani utaisha mwaka gani,” alisema Mulundi.
Kwa mujibu wa mtuhumiwa huyo, amepata kutoa malalamiko kwa Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,
Angela Kairuki na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), akiiomba serikali
imlete mbele yake, Dk. Ulimboka ili amtambue na kuhakikisha upelelezi wa
kesi hiyo unafikia tamati.
Mbali ya maombi hayo, mtuhumiwa huyo wa kesi inayovuta hisia za wengi
ndani na nje ya nchi, pia alisema aliwaomba viongozi hao wamsaidie
kupata dhamana kwani kesi inayomkabili inaruhusu dhamana na hana wakili
wa kumtetea.
“Dk. Nchimbi alipokuja hapa gerezani nilimwambia, lakini aliniangalia tu
bila kujibu kitu. Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Kairuki
nimemwambia, DPP nimemwandikia barua na hata Balozi wa Kenya nchini
Tanzania nimemwandikia, hajanijibu wala hakuna msaada ninaopata. Naomba
serikali, jamii inisaidie kesi hii imalizeke haraka,” alisema mtuhumiwa
huyo.
Hata hivyo mtuhumiwa huyo alitoa siri nzito ya kile alichokieleza kuwa,
ukweli kuhusu Dk. Ulimboka, jinsi alivyokamatwa, kuhojiwa na kufikishwa
mahakamani katika mazingira aliyodai tatanishi, ambayo gazeti hili kwa
sasa haliwezi kuripoti kwani kufanya hivyo ni kuingilia mwenendo wa kesi
iliyopo mahakamani.
Wakati Dk. Ulimboka alitekwa Juni 26 mwaka jana na watu wasiojulikana,
mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 3 na kufikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kitusu, Dar es Salaam Julai 13.
Dk. Ulimboka ambaye alikuwa kinara wa mgomo wa madaktari uliotikisa
nchini katika nyakati tofauti mwaka jana, alitekwa, kuteswa, kupigwa
hadi kung’olewa meno na kucha na kisha kutupwa katika msitu wa
Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Baada ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, alitangaza kuunda tume ya wataalam kutoka ndani ya jeshi
hilo, iliyoongozwa na ACP Ahmed Msangi.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Dk. Ulimboka mwenyewe kuwataja baadhi ya
watu aliodai kuwa ndio walihusika kumteka na kumtesa, lakini hadi sasa
Mulundi, ndiye mtuhumiwa pekee aliyekamatwa.
Hata hivyo, tume hiyo haijawahi kutoa ripoti yake kama Kova alivyoahidi
pamoja na kwamba hata majeruhi mwenyewe, Dk. Ulimboka hajawahi kuhojiwa,
huku vigogo wa jeshi hilo wakitupiana mpira kuhusiana na sakata hilo.
Katika hatua ya kushangaza, juzi jeshi hilo kupitia kwa msemaji wake,
Advera Senso, limekanusha kuwepo kwa tume hiyo likisema kuwa
walioteuliwa ni polisi ambao watafanya kazi za kiuchunguzi kwa taratibu
za polisi.
Kauli ya Senso ilipingana na ile ya Kova, ambaye juzi alikiri kuwepo kwa
tume hiyo, lakini akasema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa vile
taarifa zake alishazipeleka kwa wakubwa wake makao makuu baada ya
kukamilisha wajibu wake.
“Hili suala lipo mahakamani kwanza, na kuhusu kuhojiwa au kutokuhojiwa
kwa Dk. Ulimboka hilo lipo kwa mkubwa wangu, sasa unataka mimi niseme
kama amehojiwa au la wakati sijui kinachoendelea huko?” alisema Kova.
Lakini Senso alisema kuwa, hakukuwepo na tume hiyo na kwamba
walioteuliwa ni polisi ambao walifanya kazi za kiuchunguzi kwa taratibu
za jeshi hilo.
Alisema Jeshi la Polisi lisingeweza kuunda tume katika suala la Dk.
Ulimboka kwa kuwa kilichotokea ni uhalifu kama mwingine na
litashughulikiwa kwa mujibu wa jeshi hilo.
“Kwanza hilo ni suala la mwaka jana na sisi ripoti za mwaka huo
tumeshafunga, labda nianze kufuatilia sasa hivi kujua limefikia wapi,”
alisema Senso.
Wakati vigogo hao wakisigana katika kulifafanua sakata hilo, Dk.
Ulimboka mara kadhaa amekuwa akieleza kuwa yupo tayari kutoa maelezo
yake kama kutakuwa na tume huru ambayo si hiyo iliyoundwa na polisi.
Katika tamko lake mwishoni mwa mwaka jana lililosomwa kwa niaba yake na
wakili wa kujitegemea, Nanyoro Kicheere, akimwakilisha mwanasheria wake,
Dk. Ulimboka alisema wapo watu ambao hawatapenda kusikia siri
iliyojificha katika tukio zima la kutekwa kwake na kwamba hana jinsi
zaidi ya kueleza ukweli.
Alisema kuwa tukio la kutekwa kwake, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa,
kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno, na
hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande, lilitokea wakati akiwa
kikao na ofisa aliyetambulishwa kwake ni ofisa wa Ikulu, Ramadhani Abeid
Ighondu.
Chanzo: Tanzania Daima
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment