Serikali
imetangaza nyongeza mpya ya mishahara ya kima cha chini kwa sekta
binafsi nchini, ambayo itaanza kutumika Julai mwaka huu. Vile
vile, serikali imetangaza kutengeneza ajira mpya 600, 000 kwa vijana
nchini kupitia programu ya ajira kwa vijana katika mwaka ujao wa fedha. Hayo
yalitangazwa bungeni jana mjini Dodoma na Waziri wa Kazi na Ajira,
Gaudence Kabaka, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya
wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014. Waziri
Kabaka alisema nyongeza hiyo mpya pia itakuwa katika sekta binafsi nne
mpya zilizoainishwa hivi karibuni ambazo ni Ujenzi, Shule Binafsi,
Nishati na Mawasiliano.
Alisema
wizara imekamilisha utafiti wa majadiliano ya kima cha chini cha
mshahara katika sekta binafsi 12 na kwamba katika sekta zote 12 kima cha
chini kimeongezeka.
Alitaja sekta hizo kuwa ni Ujenzi, Shule Binafsi, Nishati, Viwanda na Biashara, Hoteli na Huduma Majumbani.
Nyingine ni, Ulinzi Binafsi, Afya, Madini, Uvuvi na Huduma za Majini, Usafirishaji na Mawasiliano na Kilimo.
Waziri Kabaka alisema kima cha chini katika sekta zote 12 kimeongezeka
kwa kiwango tofauti tofauti, huku Viwanda na Biashara kikiongezeka kwa
asilimia 43.8, Hoteli na Huduma za Majumbani (asilimia 55.2), Ulinzi
Binafsi (asilimia 46.4), Madini (asilimia 25), Afya (asilimia 65), Uvuni
na Huduma za Majini (asilimia 21.2), Usafirishaji (asilimia 49) na
Kilimo (asilimia 42.9).
Kuhusu ajira 600, 000, Waziri huyo alisema utekelezaji wa programu hiyo
utafanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014-2015/16.
Aidha, alisema serikali katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 inatarajia
kuwezesha kupatikana kwa fursa za ajira zaidi ya 300,000 na kwamba ajira
hizo ni mbali ya ajira 61, 915 za watumishi wa umma watakao ajiriwa na
serikali.
Alisema serikali imewabaini waajiiri ambao hawalipi wafanyakazi wao
mishahara ya kima cha chini cha serikali, kutowapa mikataba ya kazi na
kuwafanyisha kazi kwa saa nyingi bila malipo ya ziada.
Alisema baadhi ya waajiri hawatoi likizo ya uzazi, lakini serikali
imeshawachukulia hatua za kisheria ikiwamo wizara kutoa amri elekezi kwa
waajiri 118 na kuwafikisha mahakamani waajiri 33.
Alisema wizara imehakiki mikataba ya ajira ipatayo 56,000, kati ya hiyo
mikataba 19,247 ni madereva wa malori yanayosafirisha bidhaa nje ya
nchi.
Waziri Kabaka alisema mpango huo utaanza kutekelezwa baada ya kukamilika
kwa taratibu na maandalizi ya utekelezaji wake kwa lengo la kuufanya
kuwa bora na endelevu.
Alisema wizara yake kwa kushirikiana na taasisi za hifadhi ya jamii
nchini zimefanya utafiti na tathmini ya tatizo la malipo ya fao la
kujitoa katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wafanyakazi watakaopoteza
ajira kabla ya umri wa kustaafu.
Alisema mapendekezo ya namna ya kushughulikia suala hilo yameandaliwa na
yatajadiliwa na wadau kabla ya kuwasilishwa bungeni katika mwaka ujao
wa fedha.
AJIRA MPYA ZA SERIKALI, SEKTA BINAFSI
Waziri Kabaka alisema katika mwaka 2012/13 jumla ya ajira 274,030
zilipatikana na kati ya hizo, ajira 56,746 zilitolewa na serikali, ajira
8,603 zilitangazwa na sekta binafsi kupitia vyombo vya habari na ajira
208,681 zilitokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
VIBALI VYA AJIRA KWA WAGENI.
Kabaka alisema katika kipindi hiki wizara ilipokea na kushughulikia
jumla ya maombi 6,424 ya vibali vya ajira za wageni vya daraja B na
imefanya ukaguzi katika kampuni 148 kwa lengo la kuhakiki vibali vya
ajira.
Alisema rasimu ya muswada wa vibali vya ajira kwa wageni utawasilishwa
bungeni katika mwaka ujao wa fedha na kwamba lengo lake ni kuwa na
sheria moja ya kusimamia masuala ya vibali vya ajira za wageni, hivyo
kuondoa utata na migogoro katika utaratibu unaotumika sasa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment