VURUGU
zilizofanyika hivi karibuni mkoani Mtwara zimechukua sura mpya, baada
ya mambo mazito yenye sura ya kinyama ndani yake kuibuliwa. Utafiti
uliofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s), umebaini watu
zaidi ya 12 wamepoteza maisha katika vurugu hizo tofauti na takwimu za
watu watatu wanaotajwa na Serikali. Taarifa
hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na Mtandao wa Haki za Binadamu Kusini
Mwa Afrika (SAHRINGON).
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
LHRC, Harold Sungusia alisema utafiti huo wa muda mfupi umebaini kasoro
katika takwimu za Serikali kuhusiana na vifo vya watu.
Sungusia alisema utafiti uliofanywa na shirika lake umebaini kuwapo kwa
vitendo vya ubakaji wa wanafunzi wa vyuo, huku wazee wa kimila wakidaiwa
kuchinja mbuzi za tambiko kupinga ujenzi wa bomba kwa ajili ya
kusafirisha gesi.
Vifo
Sungusia
alidai kuwa wamebaini vifo vilitokea katika vurugu hizo ni zaidi ya 12
na kwamba shirika lake linaendelea kuhakiki majina ya watu waliofariki
dunia na taarifa zao nyingine.
Sungusia alitoa shutuma nzito kwa askari polisi kwamba ndio waliohusika na ongezeko la vifo hivyo.
“Hivi vifo ni kutokana na askari polisi kuvamia nyumba za wananchi,
kuvamia maduka na kuingia ndani na kupiga mabomu ya machozi, huku
wakiiba mali za raia zikiwamo televisheni, redio na fedha,” alisema.
Alisema timu ya watafiti hao inaendelea kuzungumza na wazazi na familia
zilizopoteza ndugu zao ili kuwa na uhakika wa majina yao, umri na maeneo
walipozikwa.
Sungusia alisema katika hali isiyo ya kawaida, taasisi za Serikali
zikiwamo hospitali na polisi zimeshindwa kutoa ushirikiano wa karibu
pale walipotakiwa kutoa taarifa halisi kuhusu madhara ya vurugu hizo.
“Tumezungumza na baadhi ya wakazi wa Mtwara juu ya mambo mbalimbali
kuhusu gesi na athari zilizotokea katika vurugu za hivi karibuni.
“Walieleza ndugu zao waliokufa na baadhi tumepata majina yao, tutayaweka baada ya kukamilisha taarifa zote,” alisema.
Matambiko ya kimila
Alisema kuwa katika vurugu hizo zilizotokea, wamebaini kuwa tayari
baadhi ya wazee maarufu wa kimila wamekwishafanya matambiko yao na
kuwapa vijana imani ya kuapishwa juu ya kutetea na kulinda rasilimali za
Mtwara zisitoke bila wao kuridhia.
“Tumezungumza na wazee wa kimila na wakakiri kwamba walikwishafanya
matambiko yao na kutoa mbuzi wawili kama kafara, mbuzi mmoja alichinjwa
wakanywa damu na wa pili alipelekwa eneo lenye gesi na kufanya matambiko
yao.
“Katika matambiko yao walikubaliana kama mbuzi huyo akipiga magoti, basi
gesi hiyo haitatoka Mtwara na kama angesimama ingeashiria inatoka.
Wanasema mbuzi wao alipiga magoti.
“Pia tumeelezwa kwamba, vurugu hizo zilichochewa na taarifa zilizotolewa
na wavuvi wanaovua kina kirefu cha bahari kwamba, kuna meli imetia
nanga baharini na inavuna gesi na inaipeleka ng’ambo kupitia Nyambizi
yaani Sub-marine.
“Kutokana na hali hiyo, wananchi wa Mtwara walianza kuhamasishana mjini
hadi vijijini na kuwa na msimamo wao wa lugha ya kimakonde kama ‘AIYUKI’
yaani haitoki,” alisema.
Ubakaji
Sungusia
alisema wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Chuo cha Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Chuo cha Mtakatifu Augostine ni
miongoni mwa watu walioathiriwa.
Alisema wanafunzi hao walivamiwa na polisi wakiwa njiani wakienda mjini
kujifunza kwa vitendo ‘field’ na kufanyiwa vitendo hivyo vibaya.
Alisema licha ya wananchi wa Mtwara kushukuru askari wa Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) kurejesha amani, lakini wameendelea kuwa na
hofu kubwa.
CUF kukutana na Wanamtwara
Wakati
huo huo Chama cha Wananchi (CUF), kimeandaa kongamano kubwa kwa ajili
ya wananchi wanaotoka Mtwara na Lindi waishio jijini Dar es Salaam, ili
kujadili kwa uwazi tukio la Mtwara.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa Habari Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema kongamano hilo litafanyika
Juni 2, mwaka huu.
Alisema CUF imeamua kufanya kongamano hilo, baada ya kupokea malalamiko
kutoka kwa wananchi wakilalamikia hatua ya Serikali kutosikiliza kilio
chao.
“Baada ya majadiliano ya kina mawazo ya wananchi yatakusanywa kisha
kupelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Spika wa Bunge, Anne Makinda
ili waweze kuyachambua nao kwa nafasi zao na kuyachukulia maamuzi,”
alisema Mtatiro.
Alisema kuwa chama chake kinafanya hivyo kutokana na vyama vya siasa
kuzuiwa kufanya mikutano katika mikoa ya kusini katika kipindi hiki.
“Sisi vyama vya siasa hatuna mtutu wa bunduki, ila tunatoa elimu kwa
wananchi ni wapi tumeyumba kiuchumi na nini kifanyike katika kuiondoa
CCM madarakani,” alisema.
Chanzo - Mtanzania
No comments:
Post a Comment