Bodi ya
Mikopo nchini, imeboresha mfumo wake wa makusanyo ya malipo ya mikopo
inayotolewa kwa wanafunzi na kufanikiwa kukusanya Sh. bilioni 20 mwaka
jana. Hayo
yalisemwa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru
Kawambwa, alipokuwa akifungua mkutano wa siku tatu wa Umoja wa Taasisi
zinazokopesha wanafunzi wa vyuo vikuu na elimu ya juu Barani Afrika
unaofanyika jijini hapa.
Alisema hali ya urejeshwaji wa mikopo ni nzuri kwa sasa kwani asilimia
61 ya fedha zinazokopeshwa zinarejeshwa na kusaidia kukopesha wanafunzi
wengine.Dk. Kawambwa alisema kuwa hali imekuwa tofauti na siku za nyuma.
Aidha, alisema mwaka wa fedha mwaka huu, serikali imetenga Sh. bilioni
326 kwa ajili ya kukopesha wanafunzi. “Lakini tunatarajia hata mwaka huu
mwishoni tutakuwa tumekusanya Sh. bilioni 20 na hii itaendelea kupanda
kwa sababu bado kuna watu hawajarejesha," alisisitiza.
Kuhusu kuwashtaki wanafunzi ambao walikopeshwa na kutorejesha pindi
wanapopata kazi, alisema hawapendi sana kupelekana mahakamani kwa sababu
inapoteza muda wa kufuatilia kesi, japo wapo baadhi wamepelekwa
mahakamani.
Aliwaomba wanafunzi na wafanyakazi waliosoma kwa mikopo hiyo, wakumbuke
kurejesha ili kuwezesha wenzao kupata nafasi ya kusoma elimu ya juu.
Naye
Mkurugenzi wa Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini, George
Nyatega, alisema kwa sasa Bodi hiyo inatoa mikopo asilimia 48 ya
wanafunzi wote wanaosoma elimu ya juu na wanaobakia wanajisomesha
wenyewe.
Alisema wanatamani kukopesha watu wengi zaidi lakini fedha walizonazo ni
hazitoshelezi na ndiyo maana wanasisitiza urejeshwaji wa fedha hizo kwa
waliomaliza.
“Tunajua malalamiko yapo mengi, lakini lazima yawapo kwa sababu wapo watu hawakidhi vigezo vyetu na fedha kuwa kidogo," alisema.
Kwa upande wake, Rais wa Umoja wa Taasisi zinazokopesha wanafunzi wa
Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu (Ahefa), Charles Ringera, alisema umoja huo
unalenga nchi zote za Afrika zijiunge ili wawafuatilie watu
waliokopeshwa kupitia bodi za kila nchi warejeshe fedha hizo kwa nchi
yoyote alipo kwa wakati huo.
Chanzo: Nipashe
No comments:
Post a Comment