Na Ally Kondo, Kuwait
Serikali ya kuwait imetenga kiasi cha
Dola za Marekani bilioni moja (1) kwa ajili ya kuzipatia nchi za Afrika
mikopo ya masharti nafuu katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Tangazo
hilo lililotolewa na Amir wa Kuwait ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano
wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Ushirikiano baina ya Nchi za
Afrika na Kiarabu (Third Afro Arab Summit), Sheikh Sabah Al-Ahnad
Al-Sabah wakati alipokuwa anatoa hotuba ya ufunguzi ya mkutano huo
nchini Kuwait siku ya Jumanne tarehe 19 Novemba, 2013.
Sanjari na kiasi hicho cha fedha, Sheikh
Al-Sabah alitangaza kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni moja (1)
kwa ajili ya kufadhili shughuli mbalimbali za utafiti zenye lengo la
kuibua fursa za maendeleo katika nchi za Afrika.
Sheikh
Al- Sabah aliwambia wajumbe wa mkutano huo kuwa, Mkutano wa Tatu wa
Afro Arab Summit unafanyika huku nchi nyingi za Afrika na Kiarabu
zikikabiliwa na changamoto za kisiasa na kiuchumi ambazo bila kupatiwa
ufumbuzi wa kudumu malengo yanaayowekwa katika mikutano hiyo
hayatafikiwa. Alisisitiza nchi za Afrika na Kiarabu kuwekeza katika
miradi itakayoimarisha ushirikiano wao akitolea mfano wa sekta ya
kilimo. “Endapo usalama wa chakula hautakuwa wa kuaminika katika nchi za
Afrika na Kiarabu, kutazifanya nchi hizo kuwa katika hali tete na
hatimaye kushindwa kukidhi matarajio ya wananchi wao. Sheikh Al-Sabah
alisikika akisema.
Aidha,
Amir wa Kuwait aliwaomba Wakuu wa Nchi kutumia mkutano huo kutafuta
suluhu ya kudumu ya mgogoro unaoendelea nchini Syria ambao athari zake
unaikumba kanda nzima ya Kiarabu. Alihitimisha hotuba yake kwa kulitolea
wito Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuishinikiza Israel
itekeleze Maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mamlaka ya Palestina.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti mwenza wa mkutano huo, Waziri Mkuu wa Ethiopia,
Mhe. Hailemariam Dessalegn alieleza kuwa nchi za Afrika haziwezi
kufikia mapinduzi ya kijani endapo hakutawekwa mkazo katika sekta za
nishati jadilifu, miundombinu na utalii. Hivyo, alisisitiza umuhimu wa
mkutano huo kubuni mwongozo makini wa ushirikiano utakaowezesha kufikiwa
kwa malengo hayo.
Mhe. Dessalegn alizihimiza nchi za Afrika
na Kiarabu kuongeza nguvu mara dufu katika mapambano dhidi ya uharifu
wa mipakani, ugaidi, uharamia pamoja na uhamaji wa kinyume cha sheria.
Aliweka angalizo kuhusu tatizo la uhamaji kwa kusema kuwa endapo
halitafanyiwa kazi vizuri linaweza kudhoofisha ushirikiano huo. Hivyo,
aliunga mkono pendekezo la kuunda Kamati ya Pamoja ya Wataalamu kutoka
nchi za Afrika na Kiarabu ili kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa
Afrika, Mhe. Nkosazana Dlamini-Zuma naye aliwahakikishia Wakuu wa Nchi
katika mkutano huo kuwa, Afrika imejizatiti kutekeleza yale yote mazuri
yatakayoafikiwa katika mkutano huo. Aidha, alihimiza umuhimu wa kuwekeza
katika elimu ili idadi kubwa ya vijana ambao ndio nguvu kazi na
wanawake ambao ni zaidi ya nusu katika nchi za Afrika wapate elimu bora
inayoendana na madadiliko yanayotokea duniani hivi sasa.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo
unaongozwa na Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais ambaye pia
amepangiwa kutoa hotuba.
|
No comments:
Post a Comment