Hali ya
wasiwasi iligubika eneo kinapofanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilichoanza Dar es Salaam jana. Ulinzi
mkali wa walinzi wa Chadema (Blue Guard), uliimarishwa katika ukumbi wa
Ubungo Plaza kinapofanyika kikao hicho ambacho kinatarajiwa kumalizika
leo, huku kukiwa na maagizo yaliyoashiria kuwapo kwa mambo mazito.
Maazimio
ya kikao hicho yanasubiriwa kwa hamu na wafuatiliaji wa mambo ya siasa
nchini kwani kinafanyika katika kipindi ambacho chama hicho kikuu cha
upinzani nchini kinapita katika misukosuko na hasa ya malumbano baina ya
makamanda wake wa juu.
Maelekezo ya ulinzi - Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe aliwasili ukumbini hapo saa 5.20 asubuhi na
baada ya kuingia, wapiga picha waliruhusiwa kuingia kuchukua kumbukumbu
ya tukio hilo kwa dakika moja tu.
Waandishi wa habari hawakutakiwa kuingia na badala yake walielezwa kuwa wangepewa taarifa baadaye.
Wakati
wapiga picha wakiwa ndani, mmoja wa wajumbe wa mkutano huo alitoka na
kutoa maelekezo kwa walinzi wa Chadema akiwataka kuwa makini kutekeleza
kazi yao watakapopewa amri ya kumwondoa mjumbe yeyote mkutanoni.
“Kama
mkipewa amri ya kuondoa mtu ingieni na mtekeleze amri hiyo mara moja,”
alisisitiza mjumbe huyo na kuingia ndani haraka. Walinzi hao zaidi ya
10, walipokea maelekezo hayo kwa kutikisa kichwa kuashiria kukubaliana
na amri hiyo.
Kikao kufunguliwa - Kikao hicho ambacho kilifunguliwa dakika nane baada ya Mbowe kuwasili, kilipangwa kujadili mambo matatu jana.
Mmoja wa
wajumbe wa mkutano huo ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema
kingepitia taarifa za vikao viwili vya Kamati Kuu vilivyopita.
Suala
jingine ambalo lilipangwa kujadiliwa jana ni ushiriki wa Chadema katika
uchaguzi mdogo wa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Kiembesamaki,
Zanzibar na kupitia taarifa ya fedha.
Leo moto - Ajenda
zinazotarajiwa kujadiliwa leo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa
Kampeni ya ‘Movement For Change’ (M4C) na hali ya siasa.
Ajenda hiyo
inatazamiwa kugusa matukio ya hivi karibuni ndani ya chama hicho. Hayo
ni pamoja na malumbano kati ya Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho,
kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson
Mwigamba, kuvunjwa kwa uongozi wa Mkoa wa Mara na pia kuondolewa kikaoni
kwa Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda.
Zitto na Lema waliingia katika vita ya maneno mwanzoni mwa Novemba kuhusiana na masuala ya posho ya vikao.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Lema
alimtuhumu Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba anakataa posho za
vikao bungeni, lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika mbalimbali
ya kijamii nchini.
Lema aliweka
tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii Forum huku akisema suala hilo
halihitaji vikao vya chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na
hususan, mitandao ya kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao hiyo.
Akijibu hoja
hizo, Zitto alisema tangu siku nyingi alikwishapiga marufuku kwenye
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupokea posho kutoka taasisi
au mashirika yanayosimamiwa na kamati hiyo.
Alisema
tangu alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya
Umma (POAC), alipiga marufuku posho na pia aliwahi kuwashtaki Taasisi ya
Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) wabunge wanaochukua posho kutoka
taasisi za Serikali.
Zitto pia
alipata msukosuko mwingine baada ya kusambazwa ripoti inayoitwa ‘Taarifa
ya Siri ya Chadema’ iliyomtuhumu kuwa alikuwa anashirikiana na CCM na
viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa kuhujumu chama hicho.
Ripoti hiyo
inayodaiwa kuwa iliandaliwa na Idara ya Upelelezi ya Chadema, ilieleza
kuwa Zitto alikuwa akipokea fedha kutoka kwa maofisa wa usalama na
kuzisambaza kwa makada wengine wa chama hicho ili wafanye kazi ya
kukihujumu. Hata hivyo, Chadema kupitia kwa Mnyika ilitoa taarifa
kupinga vikali suala hilo.
CAG kukagua ruzuku - Pia,
Zitto aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama
vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na CAG. Chadema ilipinga vikali
madai hayo na kueleza kuwa imekuwa inatumia taasisi binafsi kufanya kazi
hiyo.
Suala
jingine linalotazamiwa kujadiliwa katika kikao hicho ni kusimamishwa kwa
Mwigamba na Baraza la Uongozi Kanda ya Kaskazini ambako kulizuka vurugu
kiasi cha kunyang’anywa kompyuta mpakato (laptop) baada ya kudaiwa
alikuwa anasambaza taarifa za kuhujumu chama hicho.
Suala lake linasubiri uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kama lile la kuvunjwa kwa uongozi wa Chadema wa Mara.
Pia kitendo
cha Baraza la Kanda ya Ziwa Mashariki kumtimua Shibuda kwa madai kwamba
halina imani naye nacho kina uwezekano mkubwa wa kujadiliwa.
Zitto na Mnyika wakosekana - Zitto na Mkurugenzi wa Uenezi wa chama hicho, John Mnyika walikuwa miongoni mwa wajumbe walioshindwa kuhudhuria jana.
Zitto yuko
na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) huko Sudan
Kusini na Mnyika pia yuko katika ziara ya kibunge Uturuki.
Kikao cha jana kilihudhuriwa na wajumbe 23 kati ya 32.
Chanzo - Mwananchi
Picha na Michael Jamson
No comments:
Post a Comment