Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, September 22, 2014

WATANZANIA WASHAURIWA KUPANDA MLIMA KILIMANJARO ILI KUUTANGAZA UTALII WA NDANI

WATANZANIA wameshauriwa kuwa na tabia ya kupanda Mlima Kilimanjaro, ili kuutangaza utalii wa ndani, badala ya kuwaachia wazungu wenyewe kupanda mlima huo.

Hayo yalisemwa na Kamishna Mkuu Msaidizi wa Skauti Tanzania, Faustini Magige, wakati waliposhuka katika kilele cha mlima Kilimanjaro, walipopeleka ujumbe wa Amani.

Magige alisema kuwa, Skauti ni mtu wa kutengeneza amani pamoja na kuilinda amani ya nchi, hivyo katika siku ya amani duniani, inayofanyika kila mwaka Septemba 21. Mwaka huu ujumbe huo wa amani waliamua kuufikisha katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

“Ujumbe huu, wa amani duniani, tumelenga kwa kila mwananchi kuwa ni raia bora hasa katika familia zetu na tumeamua kuufikisha kileleni mwa mlima kilimanjaro, kwani ndio mlima mrefu kuliko yote Afrika,” alisema Magige.

Alisema kuwa kwa sasa nchi yetu, inajiandaa na Uchaguzi mdogo wa Serikali za Mitaa na ule uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwa, hivyo amewaasa wananchi kufanya uchaguzi huo kwa haki na amani bila kufanya maandamano yoyote yatakayochafua taifa letu.

Aidha Magige amewaasa vijana kujiunga na Skauti ili kunufaika na mafunzo hayo, pamoja na kuachana na kutumiwa na wanasiasa katika kuchafua amani ya nchi yetu iliyodumu kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Skauti aliye na umri mdogo wa miaka 18, na mwanafunzi wa kidato cha Nne katika shule ya Sekondari Lutengano, iliyoko mkoani Mbeya, Betody Ivo, alifanikiwa kuvunja rekodi, baada ya kupanda mlima Kilimanjaro hadi kileleni mwa mlima huo.

Ivo alisema kuwa, amefurahishwa kupanda mlima huu hadi kileleni na kufanikiwa kuweka rekodi ya kupanda mlima huo akiwa na umri mdogo.

“Kweli ninafuraha kupanda mlima huu hadi kileleni, na kufanikiwa kupata cheti, lakini tatizo kubwa nililokutana nalo ni hewa kuwa mbaya, hali iliyosababisha baadhi ya Skauti wenzetu kushindwa kupanda mlima huo na kurudia njiani” alisema Ivo.

Katika kampeni hizo za kupanda Mlima Kilimanjaro, Skauti wapatao tisa kutoka katika mikoa ya Dar es salaam, Mbeya, Pwani, Mwanza na wenyeji Kilimanjaro, walipanda ambapo watatu ndio waliofanikiwa kufika kileleni mwa mlima huo, na kufikisha ujumbe wa Amani.

No comments:

Post a Comment