Aprili 13, mwaka 1922, safari ndefu ya maisha ya Mwalimu Kambarage Nyerere iliyochukua miaka 77 na miezi 6 ilianza Mwitongo kijijini Butiama, kilomita takribani 30 kutoka mji wa Musoma, mashariki mwa Ziwa Victorialililoko kaskazini mwa Tanzania. Siku hiyo mvua kubwa ilinyesha. Mama Mgaya Nyang’ombe, aliyekuwa mke wa tano kati ya 23 wa Chifu Nyerere Burito wa Zanaki,
Alijifungua mwanae wa pili. Kwa desturi za kabila la Wazanaki, mtoto wa kike ama wa kiume aliyezaliwa siku ya mvua alipewa jina la KAMBARAGE (mzimu wa mvua).Kambarage alikuwa mtoto wa maskini kama walivyokuwa watoto wengine kijijini. Ingawa baba yake alikuwa Chifu (Mtemi), cheo hicho alichopewa wakati wa utawala wa Kijerumani hakikuwa na maslahi yoyote ya maana. Kwa desturi za makabila mengi, watoto walilelewa na kutunzwa na mama zao. Kwa hiyo, Mama Mgaya alijitegemea mwenyewe katika kuwalea wanawe 6 alioishi nao kwenye kibanda cha udongo, na paa la nyasi. Kambarage alipofikia umri wa kuelewa mambo, alimuhurumia sana mama yake na kumsaidia kazi kwa kadri alivyoweza.Eneo la Mwitongo lilikuwa na mandhari ya kupendeza ya kilima kidogo kilichozungukwa na vichaka na mawe.
Mtoto Kambarage alicheza michezo ya kujificha kwenye vichaka na kukimbiza pimbi na tumbili kwenye mawe. Alichunga mbuzi za mamaye na alipofikia umri wa kutosha, alienda na vijana wenziwe kuwinda porini. Pamoja kumsaidia mamaye alipata muda wa kuwa karibu na babaye na kujifunza utamaduni wa kizanaki.Siku moja, akiwa na miaka 10 baba yake alimtuma afuatane na mama yake wa kambo kwenda kwenye kijiji kingine kuhudhuria msiba wa jamaa wa mama huyo. Wakati wa kurudi walipewa mbuzi. Kambarage alimfunga kamba mbuzi na kumwelekeza njia. Mbuzi akagoma. Wakati wanakukurushana naye mzee mmoja akamwambia atamrahisishia kazi. Mzee yule akang’oa nywele kidogo kutoka kichwa cha Kambarage na manyoya kidogo toka kichwa cha mbuzi akachanganya na mizizi fulani, akatafuna na kumpa mbuzi akala. Yule mbuzi akamfuata Kambarage mpaka wakafika nyumbani Mwitongo bila kumsumbua!Akiwa na umri wa miaka 11 baba yake akamtolea Kambarage mahari kwa binti mmoja kijijini. Kwa desturi za Kizanaki mzazi alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo ili kuwa na uhakika kwamba hata akifa wanawe wa kiume watakuwa na uwezo wa kuoa.Kambarage hakutegemea kwamba angeliweza kupata nafasi ya kwenda shule kwa sababu baba yake alikuwa hana uwezo wa kuwasomesha wanawe wote. Hata hivyo, alidhihirisha kuwa na akili nyingi zilizo muwezesha kujifunza mambo haraka. Alijifunza kucheza bao kutoka kwa baba aliyependa kucheza bao na mama yake aliyekuwa hodari wa mchezo huo. Kila alipopewa nafasi ya kucheza bao na marafiki wa baba yake Kambarage aliweza kuwafunga! Akili alizozidhihirisha katika mchezo huo ndizo zilizomuwezesha kupata bahati ya kwenda shule. Mmoja wa wazee hao alimshauri Chifu Nyerere amuingize mwanawe shule kwa kuwa alionekana kuwa na akili sana. Ilimuwia vigumu Chifu kuamua lakini mwanawe mkubwa Edward Wanzagi alimshawishi akakubali.
Hatimaye, siku moja ya mwezi Aprili mwaka 1934, Kambarage akiwa na umri wa miaka 12 aliamka mapema kwa furaha kwenda kuanza darasa la kwanza katika shule ya Mwisenge, Musoma mjini. Kambarage aliingia shule akiwa hajui Kiswahili sawasawa. Hata hivyo, haikupita muda akajua Kiswahili, akili alizoonyesha kwenye bao zilidhihirika darasani pia. Ingawa wakati alipoanza shule alikuwa amechelewa kwa miezi mitatu, aliweza kuelewa mambo kwa kasi kuwashinda wengine walioanza mapema. Alipoingia darasa la tatu walimu waliamua kumrusha hadi la nne, akasoma masomo ya miaka minne kwa miaka mitatu tu. Mwaka 1936 alifanya mtihani wa nchi nzima wa kuingia darasa la tano, akawa mtu wa kwanza Tanganyika nzima. Alichaguliwa kuingia shule ya bweni Tabora ambayo ilikuwa na darasa la tano hadi la kumi.
KIJANA KAMBARAGE
Mwaka 1937 Kambarage akiwa kijana wa miaka 15 alianza masomo ya darasa la tano akiwa na ari ya kusoma kwa bidii. Waalimu wake Tabora walimpenda kwa akili zake. Wanafunzi wenziwe nao walimpenda sana kwa sababu alikuwa mcheshi na mwema sana. Waliosoma naye waliwahi kueleza kwamba ingawa alikuwa akienda shule na fedha kidogo sana za matumizi, alikuwa radhi kutoa fedha zote alizokuwanazo kuwasaidia wanafunzi waliokuwa na shida. Pamoja na wema, alionyesha tabia ya kupenda kutetea HAKI. Hakukubali kuona uonevu uliokuwa ukifanywa na ma-kaka dhidi ya wanafunzi. Aliwahi kwenda kwa Mwalimu Mkuu kulalamika kuhusu adhabu ya kufungwa miguu na mikono aliyopewa mwanafunzi mmoja na kaka wa bweni. Kwenye kuamua shauri hilo Mwalimu Mkuu alimpendelea kaka na alimpa mwanafunzi huyo adhabu nyingine ya viboko. Kambarage aliamuriwa kumchapa, ilibidi amchape ingawa hakupenda kabisa kufanya hivyo! Hata hivyo, Kambarage hakuuacha msimamo wake wa kuwatetea waliokuwa wakionewa. Hatimaye, Waalimu waliamua kumpa naye cheo cha ‘Kaka’ lakini hiyo haikuwa dawa. Haikupita muda, alianzisha mgomo wa kupinga mtindo wa ma-kaka kupata upendeleo wa kujigawia chakula kingi kuliko wanafunzi wengine ingawa naye alikuwa kaka!Pamoja na kutetea haki za wanafunzi wenziwe, alidhihirisha uhodari wa kutetea kile alichoamini. Siku moja wakati wa kipindi cha majadiliano, mada ya “Tanganyika iendelee kuwa chini ya utawala wa Waingereza” ilikuwa ikijadiliwa. Katika kuchangia, bila woga wowote mbele ya Mwalimu Mkuu (Mwingereza) Kambarage alipinga kwa nguvu hoja ile na kuelezea waziwazi uovu mwingi uliokuwa ukifanywa na Serikali ya Uingereza katika kuitawala nchi kwa mabavu na kwa misingi ya ubaguzi wa rangi. Mwalimu Mkuu alimkatisha na kumwamuru akae chini asiendelee kuzungumza. Kambarage alihamaki na kuamua kutoka kwenda bwenini kubeba sanduku lake ili akapande gari moshi (treni) kurudi kwao Butiama! Ilibidi Mwalimu Mkuu atume watu kumshawishi arudi shuleni.
JULIUS KAMBARAGE
Akiwa shuleni Tabora Kambarage aliweza kubatizwa na kuwa Mkatoliki akajipa jina la ‘JULIUS’. Mwalimu aliwahi kusimulia kwamba ingawa alianza kuingia kwenye mafundisho ya dini akiwa shuleni Mwisenge, hakuweza kubatizwa kwa sababu mapadri walidhani kwamba angeweza kumrithi baba yake uchifu na hatimaye kuwa na wake wengi! Wamisionari walijaribu sana kumhubiria Chifu Nyerere Burito ajiunge na ukristo bila mafanikio. Mara nyingi mapadri walipomfuata kumhubiria aliishia yeye kuwahubiria wao! Kambarage aliweza kubatizwa baada ya baba yake kufariki mwaka 1942. Wasiwasi wa mapadri ulikuwa umeisha kwa sababu aliyerithi u-chifu alikuwa Edward Wanzagi.Baada ya masomo shuleni Tabora, Julius Kambarage alifanikiwa kwenda Chuo Kikuu cha Makerere. Akiwa huko kidogo kidogo alianza kujihusisha na mambo ya kisiasa. Alianzisha tawi la chama cha TAA kilichokuwa kimeanzishwa Dar es Salaam kama chama cha kutetea maslahi ya Watumishi wa Serikali waliokuwa wakinyanyaswa na kudhulumiwa na Wakoloni.
MWALIMU JULIUS KAMBARAGE
Mwaka 1945 Julius Kambarage Nyerere alifaulu masomo yake na kupata Diploma ya ualimu. Akarudi kijijini Butiama na kumjengea mama yake nyumba kabla ya kwenda kuanza kazi Tabora. Uamuzi wake wa kutaka kuajiriwa kwenye shule ya misheni ya Mtakatifu Maria Tabora ni kielelezo kimoja cha msimamo wake kuhusu HAKI. Alikuwa amepokea barua mbili za ajira – moja kutoka Serikalini ikimpa nafasi ya kufundisha kwenye shule ya Sekondari ya Tabora na nyingine kutoka kwenye shule ya misheni ya Mtakatifu Maria (St. Marys). Barua kutoka Serikalini ilimweleza juu ya mshahara atakaopata na marupurupu ya malipo ya pensheni na kwamba shule za misheni hazikuwa na marupurupu yoyote. Julius hakupendezwa na utaratibu wa marupurupu ya walimu wa serikali na misheni kutofautiana. Akaamua kwenda kufundisha shule ya Sekondari ya misheni isiyo na marupurupu yoyote.Tabia yake ya kupenda haki iliendelea kujidihirisha katika shughuli mbalimbali alizofanya akiwa Tabora. Aliendelea kujihusisha na chama cha TAA akawa katibu wa tawi la chama hicho mjini Tabora. Alishiriki kwenye midahalo ya shule za Sekondari na hoja alizotoa zilivutia sana. Katika mdahalo mmoja uliokuwa na mada “Mali ni bora kuliko Elimu” Julius alipinga vikali hoja. Akasema kwamba alichagua kazi ya ualimu ili iwawezeshe watu kuelewa mambo na kwamba wakielewa wanakuwa na furaha, si kwa sababu wana mali. Unaweza kuwa mtu mwenye mali lakini huna furaha!Mwalimu Julius alikuwa na hamu sana ya kwenda ng’ambo kwa masomo ya juu lakini kutokana na msimamo aliokuwanao dhidi ya Serikali, wakoloni hawakutaka kumpa nafasi hiyo. Hatimaye kwa kutetewa na rafiki yake aliyekuwa padri wa kizungu (Father Walsh) aliweza kupewa scholarship na Serikali kwenda Chuo Kikuu cha Edinburgh kuchukua masomo ya historia na uchumi. Akalipenda sana somo la filosofia. Mawazo ya kuingia kwenye siasa yalianza kujengeka wakati huo. Akiendelea na msimamo wake wa utetezi wa haki aliweza kuandika makala mbali mbali. Mbili alizopeleka kwenye mashindano alipata zawadi ya kwanza. Makala moja ilihusu ‘kuonewa wanawake’ akielezea kuhusu unyonge wa wanawake katika maisha ya makabila nchini. Ya pili ilikuwa na kichwa cha habari “Matatizo ya Ubaguzi wa Rangi katika Afrika Mashariki”. Katika makala hiyo alisema Wazungu alikuwa anatawala kudumisha umaarufu wao kwa njia ya unafiki.... Bepari Mhindi alikuwa anapata chakula chake kwa wizi mtupu au ujanja-ujanja na unafiki... Mwafrika naye alikuwa mnafiki alijipendekeza kwa Mzungu wakati moyoni anapasuka kwa wivu na chuki!Alimaliza vema masomo yake huko Edinburgh na kuwa Mwafrika wa kwanza nchini Tanzania kupata Stashahada ya Juu. Aliporudi nyumbani alipokelewa na mchumba wake Maria Magige aliyemchagua mwenyewe si yule aliyetolewa mahari na baba yake. Ikambidi afanye tena zoezi la kujenga nyumba kwa ajili yake na Maria watakapofunga ndoa. Wanakijiji walimshangaa walipomuona msomi kama yeye akichanganya simenti na mchanga kufyatua matofali kwa ajili ya kujengea. Wasomi hawakupaswa kufanya kazi kama hizo! Julius na Maria walifunga ndoa tarehe 24 Januari 1953 kwenye kanisa Katoliki Musoma. Katika maisha yao ya ndoa waliweza kuwapatia watoto 7, watatu wa kike na wanne wa kiume.
AWA KIONGOZI
Baada ya mapumziko yake Butiama Mwalimu Nyerere alienda kuanza kazi ya kufundisha katika shule aliyopangiwa ya Pugu Sekondari, Dar es Salaam. Mwaka huo wa 1953 akiwa Pugu alianza kujihusisha kikamilifu na shughuli za chama cha TAA. Aliitembea kwa miguu na wakati mwingine kwa baiskeli ya kua zima umbali wa maili 12 kwenda mjini Dar es Salaam kuhudhuria mikutano na shughuli za chama hicho. Haikupita muda akili na uwezo mkubwa aliokuwanao ulidhihirika akachaguliwa kukiongoza. Kutokana na uongozi wake mahiri chama cha TAA kikabadilishwa kuwa chama kamili cha siasa tarehe 7 Julai 1954, kikaitwa TANU.Chini ya uongozi wake baada ya kuanzishwa kwa chama cha TANU zilianza rasmi harakati za kupigania Uhuru. Pamoja na juhudi zote za Wakoloni kuchelewesha kupatikana kwa Uhuru hatimaye mwaka 1960 nchi ya Tanganyika ilifanikiwa kupata Serikali ya Madaraka. Desemba 9 1961 ikapata Uhuru kamili ,Mwalimu akawa Waziri Mkuu. 1962 nchi ya Tanganyika ikawa Jamhuri akawa Rais wa Kwanza wa Tanganyika Huru.Simulizi kuhusu uongozi uliotukuka miaka 24 wa Mwalimu Nyerere akiwa Rais wa Tanzania unahitaji makala nyingine nyingi. Hakuna maelezo mafupi yanayoweza kutosheleza historia ya uongozi wake. Itoshe kusema alikuwa kiongozi shupavu sana aliyepigania uhuru wa nchi yake na wa nchi zingine za Afrika. Alijishusha na kuwa pamoja na wananchi aliowaongoza – shida zao aliziona ni zake, zilimgusa na kumnyima usingizi! Akaondoa ubaguzi na kufuta matabaka ya walionacho na wasionacho. Akafuta ukabila na udini nchini. Watanzania wakaishi kidugu. Akafanikiwa kujenga AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO akiongozwa na dira ya MAENDELEO YANAYOLENGA WATU WOTE. Akafanya Tanzania ijulikane kuwa kisiwa cha AMANI duniani.
HITIMISHO
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipendwa na kuheshimika sana ndani na nje ya nchi. Mwaka 1985 aliamua kwa hiari yake mwenyewe kuacha uongozi wa Taifa ili apumzike. Alizunguka nchi nzima kuwaaga Watanzania. Kwa mapenzi makubwa wakampa zawadi za kila aina. Wananchi walionyesha wazi huzuni waliyokuwanayo kwa uamuzi aliouchukua. Walimuaga wakilia machozi!Yote aliyoyaanza tangu utoto wake yalifikia kikomo tarehe 14 Oktoba 1999 alipoaga dunia kwenye kitanda cha hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London alikokwenda kwa matibabu. Kabla hajafariki dunia aliwakumbuka Watanzania wake akasema: “Najua nitakufa sitapona ugonjwa huu. Ninasikitika kuwaacha Watanzania wangu, najua watalia sana. Lakini nami nitawaombea kwa Mungu.” Naam, Watanzania wake walilia sana walipopata taarifa za kifo chake. Mwili wake ulipoletwa nchini waliomboleza kwa uchungu mno. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizikwa kijijini kwake Mwitongo Butiama kwa heshima zote na wananchi wa Tanzania, na wa mataifa mbalimbali wakiwemo viongozi mashuhuri waliokuja kwa ajili hiyo.Ni dhahiri msingi wa yale yote aliyoyaamini na kuyasimamia utaendelea kudumu ndani ya mioyo ya kizazi chake, kizazi hiki na vizazi vijavyo kutokana na mchango mkubwa alioutoa akiwa Muasisi na Baba wa Taifa katika kujenga taifa la Tanzania. Huyo ndiye mtoto aliyezaliwa siku ya mvua na kupewa jina la mzimu wa mvua KAMBARAGE; mwana wa Chifu Nyerere Burito na Mgaya wa Nyang’ombe. Ni dhahiri, tarehe aliyozaliwa – 13 Aprili mwaka 1922, Mgaya hakujua kwamba alikuwa amejifungua mtoto ambaye angekuja kuwa kiongozi maarufu sana nchini na duniani, aliyewapenda binadamu wote na kuwatumikia Watanzania kwa moyo wake wote, akili na nguvu zake zote!
MUNGU Ailaze Roho yake Mahali Pema Peponi.Mwandishi wa makala hii, Anna Julia Mwansasu, Amepata kufanya kazi ofisi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
No comments:
Post a Comment