KILIMANJARO wananchi katika manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro
wametakiwa kujitokeza kwenye zoezi la
uandikishaji wa wapiga kura kwenye
uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Disemba 14 mwaka huu.
Wito huo ulitolewa jana na Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika
Manispaa ya Moshi, Shaaban Ntarambe, wakati akizungumza na waandishi wa habari
jana ofisini kwake mjini Moshi.
Alisema wakazi wote katika manispaa ya Moshi wanawajibu wa
kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kujiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi
wa serikali za mitaa ili kuweza kutimiza haki ya kikatiba ya kupiga kura na
kuchagua viongozi wanaofaa.
Aidha alisema zoezi la uandikishaji wapiga kura linatarajiwa
kuanza Novemba 23 mwaka huu na kumalizika Novemaba 29 mwaka huu na kwamba vituo
vitafunguliwa saa 1:30 na kufungwa saa 10:00 jioni.
Aliongeza kuwa zaidi ya vituo 102 vitatumika katika zoezi
hilo kwenye kata zote 21 na mitaa yote katika manispaa ya Moshi na kwamba
halmashauri hiyo imejipanga vizuri kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.
Katika hatua nyingine Ntarambe alisema ulinzi wa wananchi
umeimarishwa katika vituo hivyo na kwamba wananchi wasiogope kujitokeza kwa
kuhofia hali ya ulinzi na usalama wao.
No comments:
Post a Comment