KILIMANJARO jamii
imeshauriwa kuacha tabia ya kuwanyanyapaa watoto wenye ulemavu na
wenye utindio wa Ubongo na badala yake wa wapatie huduma muhimu sawa na wasio
na ulemavu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti
wa kikundi kinachojihusisha na kuwapitia Elimu wanawake walemavu na
watoto kiitwacho Songambele kilichopo mkoani Kilimanjaro na Arusha, Faustina
Urasa.
Urasa alitoa kauli hiyo
alipotembelea kituo kinacholelea watoto wenye mtindio wa ubongo cha Gabriella,
kilichopo mjini Moshi, na kutoa sare za nguo kwa ajili ya kujifundishia
mapishi, ambapo mafunzo hutolewa kituoni hapo.
Alisema kuwa, jamii imekuwa
haiwathamini watoto wenye ulemavu mbalimbali ikiwemo mtindio wa ubongo huku
wengine wakifikiria imani za kishirikina na kuwafungia ndani huku wengine wakiwanyanyapaa
wakinamama wanaojifungua watoto wenye ulemavu.
“Watu wamekuwa wakiwanyima haki za msingi watoto wanaozaliwa wakiwa na ulemavu au mtindio wa ubongo, na
kuwafanya kutokupata mahitaji yao ya msingi kama Elimu sasa imefika wakati
tunapaswa kutambua kuwa hilo ni tatizo kama matatizo mengine na tunachopaswa
kukifanya ni kuwahudumia bila kuwanyanyapaa” alisema Urasa.
Aidha Urasa alisema kuwa, Wanawake
wenye ulemavu, wamekuwa wakipata changamoto kubwa katika jamii, pindi wanapo olewa
kwa kutotambua haki zao za msingi hivyo kituo cha Songambele kimekuwa
kikiwaelimisha kujua haki zao pamoja na ujasiriamali ambapo wamekuwa wakitoa
mitaji kwa mmoja mmoja.
Urasa alisema kuwa, Familia
ambazo wanatoka watu wenye ulemavu wamekuwa wakiwachukulia kama mzigo, na
kuwatenga na jamii kwa kuwaficha ndani, hivyo ameiomba jamii kuungana kwa
pamoja na kupaza sauti ili kuhakikisha kuwa walemavu hawatengwi.
Pia alisema kuwa, Serikali imekuwa
na Sera ya watu wenye ulemavu, lakini jamii na baadhi ya viongozi wamekuwa hawaitekelezi,
hivyo ameiomba Serikali kuhakikisha inaingilia ili kuhakikisha kuwa
walemavu wanapata haki sawa.
Awali Mkurugenzi wa kituo cha
Gabriella, Brenda Shuma alisema kuwa, kutio chao kimekuwa kikiwahudumia
watoto mbalimbali wenye mtindio wa ubongo kwa kuwapatia elimu ya darasani kwa
vitendo pamoja na kuwafundisha masomo ya ujasiriamali, ambapo hufundisha
kufuga kuku, mbuzi, sungura, mapishi na ushonaji.
Alisema kuwa, changamoto kubwa anayokumbana
nayo, ni jamii kuwaficha watoto wenye mtindio wa ubongo, pamoja na kuwatenga
kwa kuwanyanyapaa, bila kutambua kuwa nao wanahaki ya kupatiwa elimu.
Changamoto nyingine ni uhaba wa
fedha kwa ajili ya kuwahudumia watoto hao, pamoja na kuwalipa watumishi wanao
wahudumia watoto hao kwani kituo hicho hakijafanikiwa kupata wafadhili.
No comments:
Post a Comment