Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kusimamia ipasavyo fedha za miradi ya maendeleo, akionya kuwa Serikali ya Awamu ya Sita haitawavumilia wabadhirifu na watu wanaodai asilimia za fedha za miradi bila kufanya kazi.
Ameyasema hayo Oktoba 18, 2026, wakati akihitimisha ziara yake mkoani Iringa kwa kukagua ujenzi wa jengo la abiria na maegesho ya magari katika Kiwanja cha Ndege cha Iringa, unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 41.
Ameagiza kutathminiwa uwezekano wa kuweka taa zitakazowezesha ndege kutua na kuruka usiku, huku akisisitiza uzalendo na wajibu wa kila Mtanzania kuchangia maendeleo ya Taifa.
Aidha, amemtaka Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, kuhakikisha mkandarasi wa barabara ya mchepuo wa Iringa anarejea kazini ili kukamilisha mradi huo uliokwama licha ya Serikali kutoa fedha.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema Serikali imetenga takribani shilingi trilioni moja kwa ajili ya ujenzi na maboresho ya viwanja vya ndege katika mikoa 11 nchini.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa unatarajiwa kukamilika Mei 30, 2027, ukiwa na uwezo wa kuhudumia abiria 250,000 kwa mwaka na maegesho ya magari 80.

No comments:
Post a Comment