Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, August 17, 2012

VITENDO VYA UPORAJI VYA TISHIA MAISHA YA WAKAZI WA ARUSHA...!

Ferdinand Shayo,Arusha.
Wakazi wa kata ya Ungalimited  mkoani Arusha wameilalamikia serikali ya mtaa huo kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya uporaji vinavyofanyika katika maeneo yao hali inayoathiri shughuli za biashara  na usalama wa mali zao.
Ni kufuatia kukithiri kwa vitendo vya uporaji vinavyofanyika kwa uwazi hata nyakati za mchana kwa wapita njia pembezoni mwa barabara ya Esso,Kona ya Nairobi ,Darajani na mtaa wa Makaburi ya baniani.Kukosekana kwa udhibiti wa matukio ya uporaji kumepelekea kushamiri kwa vitendo hivyo siku hadi siku.
Wakizungumza kwa sharti la kutokutajwa majina yao kwenye gazeti,wakazi wa eneo hilo na wafanyabiashara wameeleza kuwa viongozi wa mtaa wanayafahamu mambo hayo na wamekuwa wakiyafumbia macho hawachukui hatua jambo linalosababisha kuonekana kuwa wanakumbatia  vitendo hivyo.
“Hakuna mwizi anayeiba aliyetoka mbali na mtaa huo wezi wengi ni vijana ambao ni wenyeji wa eneo hilo,wengine ni watoto wa viongozi wa mtaa,jambo hili linatukosesha imani na viongozi wetu na kupelekea hisia kuwa wezi hao wanashirikiana na viongozi kwasababu wezi wamekuwa wakikamatwa na kuachiwa bila kuchukuliwa hatua za kisheria”
Wafanyabiashara wa eneo hilo wamesema kuwa vitendo vya uporaji vimekuwa vikiathiri biashara zao na kusababisha wateja kuwa wachache kwani vitendo hivyo vimekuwa vikiwatia hofu ,wamekuwa wakilazimika kuwahudumia wateja huku wakiwa makini kuwatahadharisha wasikwapuliwe vitu vyao kama simu,mikoba,pamoja na mali zao.
Pia wameeleza kutokuwa na imani na polisi jamii pamoja na Sungu sungu ambao baadhi yao wanadaiwa kuhusika na vitendo vya uhalifu na wameiomba serikali ichukue hatua madhubuti ya  kudhibiti vitendo hivyo ili kuhakikisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Makaburi ya Baniani Bwana Jumanne Abdallah  amekanusha  madai ya wananchi hao  na kusema kuwa si ya kweli “Tunapowakamata  wezi tunachukua hatua za kuwahoji,kuwakutanisha na walalamikaji,kujiridhisha kuwa tuhuma hizo ni za kweli kasha kuwafikisha  polisi.
“Tatizo mtu anayeibiwa anapopatiwa vitu vyake kutoka kwa muhusika,ukimwambia amchukue mtuhumiwa amchukulie hatua anakataa na kusema kuwa aoni haja ya kumpeleka polisi wakati ameshapata vitu vyake kwasababu hana muda huo.Hili  limekuwa likichochea vitendo hivi”
“Kwa eneo langu lina polisi jamii vijana wasiopungua kuni (10) wanaosaidia kudhibiti uhalifu mdogo mdogo mtaani kuanzia muda wa saa moja na nusu usiku,hili limepunguza uporaji wa simu na mikoba kwa kiasi Fulani,changamoto tunayokabilana nayo  ni wananchi kuwa na mwitiko mdogo wa kuchangia fedha kwa ajili ya kuwalipa posho vijana wanaojitolea kuwa polisi jamii”
Bwana Abdallah anaeleza changamoto nyingine ni walinzi kuwa wachache na wanaolindwa kuwa wengi,unapolinda mwizi asiibe mwizi naye anakulinda kuwa unaelekea wapi ili apate nafasi ya kuiba,Akijibu madai kuwa polisi jamii wa mtaa kudaiwa kuhusika katika vitendo vya uporaji amekanusha pia madai hayo.
Ameeleza kuwa vitendo hivyo vya uporaji vimekuwa vikichochewa na vijana  wanaotumia madawa ya kulevya pamoja na ukosefu wa ajira .Hivyo amewataka wananchi kuwa walinzi wa wenzao na kushirikiana kutokomeza vitendo vya uhalifu.

No comments:

Post a Comment