Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, October 19, 2012

WABUNGE WATAKA MRADI WA UJENZI WA NYUMBA NHC UFIKE VIJIJINI..!

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) imetaka mpango wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu kufikishwa hadi vijijini ili wananchi wanaoishi katika maeneo hayo waweze pia kunufaika na nyumba hizo, badala ya mradi huo kujikita mijini peke yake.

Agizo hilo lililotolewa na Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe, ni kati ya maagizo kadhaa yaliyotolewa na kamati hiyo POAC katika kikao kati yake na bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya NHC, kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam jana.

Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alisema umefika wakati kwa NHC kufikisha vijijini mpango wake wa kujenga nyumba za bei nafuu, kwa kulenga zaidi vijiji, ambavyo wananchi wake wana kipato kinachowawezesha kumudu kununua nyumba za kuishi.

“Lazima tuwe rural plan. Haiwezekani shirika la umma likawa na plan ya mijini tu. Mchukue vijiji vyenye mazao ya biashara. Kwa mfano, Kijiji cha Kisorya (kilichopo Wilaya ya Bunda, mkoani Mara) kuna wavuvi wana kipato kikubwa kila mwaka. Ni vizuri mkaenda huko,” alisema Zitto na kuongeza:

“Vijana wanalalamika mnajengea matajiri, lakini wanaomaliza shule na wanaostaafu kazi hamuwajengei. Lazima mmbalance (muweke uwiano sawa). Wajengeeni matajiri mpate faida, lakini na watu wa hali ya chini pia.”

Mbali na hilo, POAC pia iliitaka bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya NHC kuwa makini katika eneo la manunuzi, ambalo ilisema linaweza kulitoa doa baya shirika hilo.

Pia iliitaka NHC kuepuka malipo ya kodi ya fedha taslimu kutoka kwa wapangaji, badala yake malipo hayo yafanyike kupitia benki ili kulinda mapato ya shirika.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema wamepokea maagizo hayo na kusema katika mwaka huu, watahakikisha mradi huo unagusa kila mkoa na kwamba, nyumba zao ziko katika madaraja matatu; la watu wa kipato cha kati, cha juu na cha chini.

Alisema katika NHC pia kuna mradi wa mwaka 2010-2015 uliopo katika mpango mkakati wa shirika, ambao umekwishaanza kwa wastani wa nyumba 3,000 kwa mwaka na kwamba, ifikapo mwaka 2015 mradi huo utafikisha nyumba 15,000.

No comments:

Post a Comment