Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, October 19, 2012

WAVUVI WATANO WAHOFIWA KUFA MAJI SENGEREMA..

Wavuvi watano kati ya saba wanadaiwa kufa maji baada ya kuzamishwa na watu wanaosadikiwa kuwa maharamia wanaodaiwa kushambulia mtumbwi waliokuwa wakiutumia kuvulia katika Ziwa Victoria, katika Kisiwa cha Meisome, Wilyani Sengerema, mkoani Mwanza.

Tukio hilo lilitokea katika usiku wa manane wa kuamkia jana, ambapo maharamia hao waliondoka na nyavu za wavuvi hao.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Karen Yunus, amethibitisha kupata taarifa ya tukio hilo.

“Mimi nipo mkoani Kilimanjaro kwenye msafara wa kusafirisha mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza kwa mazishi. Lakini nimewasiliana na OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) wangu kwa njia ya simu amekiri kuwapo kwa tukio hilo,” alisema Yunus.

Diwani wa Kata ya Meisome, Mtanzania Mazabari, aliwataja wavuvi waliokufa kuwa ni Revocatus Wisco, John Mayilla, Lwinamila na waliofahamika kwa jina moja moja la Rasi na Lwinamila.

Alisema wavuvi wawili walinusurika, ambao ni Thomas Lusana na Samson Nkelejiwa.

Wakielezea tukio hilo, wavuvi walionusurika walidai kuwa ‘maharamia’ hao wakiwa na boti waliwavamia wakati wakiwa ziwani wakivua na kuzamisha mtumbwi waliokuwa wakiutumia wenye namba MSR 1390.

Walisema walinusurika baada ya kuogelea na kutoa taarifa kwa wananachi, ambapo mbiu ilipigwa kwa ajili ya msaada.

Baada ya wananchi kufika eneo la tukio, walikuta mtumbwi ukiwa umezama na maiti ya mtu mmoja ilikuwa ikielea kutokana na kunasa kwenye mtumbwi.

Wavuvi waliozamishwa walikuwa wanatoka kambi ya Msufini na tayari juhudi za kuanza kutafuta miili ya wavuvi zilikuwa zikiendelea na tukio hilo.

Tukio hilo, ambalo limeripotiwa polisi, limezua hofu kubwa kwani ni la pili kutokea katika kipindi kisichozidi miezi mitano baada ya lile la kwanza kutokea Juni, mwaka huu, ambapo wavuvi watano walipoteza maisha wilayani humo.

No comments:

Post a Comment