MUDA mrefu nimekua nikijiuliza kwanini mchakato mzima wa
ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya katiba mpya ya Tanzania umekua na malumbano
mengi sana na pia zaidi ya asilimia tisini ya kinachozungumzwa kwenye mchakato wa
uundwaji wa katiba mpya ni maswala ya siasa tu. Lakini ukweli ni kwamba
watanzania tulio wengi hatufahamu kuwa katiba ya nchi ndio muongozo mkubwa sana katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanaishi kwa amani na pia
wanazilinda rasilimali za nchi kwa kutegemea katiba ya nchi. Na sio
kutumia asilimia zaidi ya tisini kujadili maswala ya siasa katika katiba maana mara
nyingi mchakato wa kukusanya maoni kwa ajili ya katiba mpya unaonekana kuegemea
sana upande wa
siasa kuliko kulenga matatizo mengi yanayoikabili jamii. Kuna mambo ambayo
kiukweli ukiyaangalia au kuyasikiliza utagundua kuwa watanzania wengi bado hatujafahamu
umuhimu wa katiba na hata tunapopata nafasi ya kuchangia mawazo utakuta tunachangia
masuala ya kisiasa tu.
Kwa mfano unakuta
kijana anapopewa nafasi ya kuchangia unamsikia akisema “Tunaomba katiba mpya itoe nafasi
kwa mgombea binafsi” Na mtu huyo hana kazi ambayo inampatia kipato cha
kumtosha kujikimu kwa maisha ya kawaida ya milo mitatu na kuishi kwenye nyumba
yenye umeme na maji na uhakika wa matibabu. Nadhani lingekua jambo la busara
kama kijana huyo angeweza kupendekeza katiba mpya itoe fursa kwa kila kijana
anapo hitimu elimu awezeshwe kupata ajira au kupatiwa mkopo wenye masharti
nafuu, au kuwe na sheria itakayowabana viongozi wa serikali kuweza kuiweka
mikataba wazi hususani mikataba kati ya serikali na wawekezaji inayohusiana na
rasilimali za nchi kama madini, mbuga za wanyama, gesi, na rasilimali nyingine
nyingi.
Wakati mwingine unakuta mwanamke anapata nafasi ya kuchangia
unamsikia akisema “Nafasi za wanawake ziongezwe bungeni ili kuweza kuleta usawa wa
wanaume na wanawake bungeni au nafasi za viti maalumu vipewe kipao mbele kwa
wanawake” Wakati mwanamke huyo elimu yake ni ya darasa la saba na hata
uwezekano wa yeye kupata nafasi hiyo haupo kabisa na yeye mwenyewe anafahamu
fika kuwa yeye hawezi kupata nafasi ya kwenda kuwakilisha bungeni. Nadhani
ingekeua jambo la busara kama angetoa mchango kwa kuomba katiba mpya iweze
kuondoa malipo kwa wakina mama wanapoenda kujifungua hospitalini, au katiba
mpya pia itoe nafasi kwa wakina mama ambao wapo nyumbani wanalea familia waweze
kuwa na mafao kutoka kwenye mshahara ambao waume zao wanalipwa ila kuwasaidia
pale ambapo mume anapofukuzwa kazi, anapostaafu au anapo fariki.
Na mlemavu anapata nafasi ya kuchangia mchakato wa katiba
mpya utamsikia anasema “Serikali itukumbuke na sisi walemavu tupewe nafasi bungeni ili tuweze kutetea na kuzisimamia haki zetu na misaada inayotoka kwa nchi wahisani” Wakati misaada ni mambo ambayo hayana uhakika
na pia misaada haitolewi kila siku au kila wiki, ila kuna maswala kama haki sawa katika sehemu
za ajira, haki za kulindwa wakati wa machafuko ama vita maana walemavu ndio
wahanga wakubwa sana wakati wa vita. Pia katiba mpya iweke bajeti kwa ajili ya
kununua vifaa kwa ajili ya walemavu mashuleni na pia zijengwe shule maalumu za
kutosha kwa ajili ya walemavu, tofauti na ilivyo sasa.
Mzee wa miaka zaidi ya hamsini anapata nafasi ya kuchangia
katika uundwaji wa katiba mpya utamsikia anasema “Katiba mpya itoe nafasi ya wazee
kuwa na bunge lake au wazee wapewe nafasi za viti maalumu bungeni” Wakati hata wakipewa hizo nafasi bado zitakua
ni chache sana na wala hazitaweza kukidhi matakwa ya wazee wote, wakati kuna
maswala ambayo endapo yatapendekezwa kuweka kwenye katiba mpya yatawasaidia
sana wazee kwa mfano mafao ya uzeeni yaboreshwe
na pia kwa wale wazee ambao hawakupata nafasi ya kuajiriwa nao wakifikizeeka
pia walipwe ili kupunguza utegemezi na pia kuwanusuru wazee na vifo visivyo vya
lazima kama kufa kwa njaa, kukosa matibabu, kuangukiwa na nyumba, n.k.
Hiyo ni mifano mchache tu lakini kuna mambo mengi sana ambayo yanatakiwa
kuwepo kwenye katiba mpya na sio kuzungumzia siasa tuuu. Wakati wanasiasa nao
wana nafasi zao za kuchangia kwenye mchakato wa katiba mpya.
By Joshua Fanuel
#teamKINGJOFA
No comments:
Post a Comment