Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Saturday, May 10, 2014

UFAFANUZI NA TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA DENGUE

  Aedes aegypti
UTANGULIZI:
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa  kwa umma juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue fever” hapa nchini.  Ugonjwa huu umethibitishwa  baada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es salaam kupelekwa kwenye maabara yetu iliyopo katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, Dar es salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya homa ya dengue mnamo tarehe Juni 12, 2013. Utafiti huu uliongozwa na jopo la wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikishirikisha program ya mafunzo ya Epidemiolojia yaani “Field Epidemiology and Laboratory Training Program” pamoja na manispaa ya Ilala.
Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao waliogundulika kuwa na dalili za ugonjwa huu  ni 20 na hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza maisha.

HOMA YA DENGUE:
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati  siku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue. Kwa wakati mwingine  dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa wakati wakipata homa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria ua la ili hatua stahiki zichukuliwe.
Virusi vya homa ya dengue vinaenezwa kwa binadamu  baada ya kuumwa na mbu aina ya Aedes. Mbu hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba. Viluwiluwi vya mbu hawa huweza kuishi katika mazingara ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu. Mbu hawa huwa na tabia ya kuuma wakati wa mchana.
Ugonjwa huu hauenezwi kutoka binadamu mmoja kwenda kwa mwingine. Homa ya dengue inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka.  Hakuna tiba maalumu ya ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na  dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu. Endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue
 
  KUANGAMIZA MASALIA YA MBU:
 •   Fukia madimbwi ya maji yaliyotuama  au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi  vya mbu kwenye madimbwi hayo
 •   Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
 •   Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu.
 • Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama.
 •   Funika mashimo ya maji taka  kwa mfuniko imara.
 •  Safisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.

  KUJIKINGA NA KUUMWA NA MBU:
 • Tumia dawa za kufukuza mbu “mosquito repellants”
 •   Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
 • Tumia vyandarua vyenye viuatilifu (hata kwa wale wanaolala majira ya mchana)
 • Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi

HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA WIZARA YA AFYA:
 • Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara kupitia Makatibu Tawala na Wakurugenzi.
 • Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani. Aidha uchunguzi wa ugonjwa huu utafanyika kwenye Mikoa na Wilaya zitakazoonekana kuwa na ongezeko la wagonjwa wenye homa.
 • Kutuma vipeperushi vya ugonjwa huu katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.
 • Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani wa  namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa atapatikana.
 • Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika hospitali 15 za mkoa wa Dar es salaam. Hospitali hizo ni pamoja na hospital ya Taifa Muhimbili, Hospitali zote 3 za manispaa ya Dar es salaam, kituo cha afya Kigamboni, Kituo cha afya cha Mbagala Rangi tatu, Dispensari ya Yombo Vituka, Kituo cha afya cha Mnazi mmoja, Dispensari ya Tabata A, Kituo cha afya cha Bochi, Kituo cha afya cha Mbweni, Hospital ya Mission Mikocheni, Hospitali ya TMJ, Hospital ya Regency na Hospital ya Hindu Mandal
 • Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara ili kuweza kuthibitisha  ugonjwa huu
 • Kufanya tathmini ya mazalio ya mbu ili kubaini ukubwa wa tatizo, jamii ya mbu wanaoambukiza ugonjwa, mazingira yao na jinsi ya kuwathibiti

HITIMISHO:
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu.

Ugonjwa huu si mpya. Mara ya kwanza kugundulika kuwepo kwa ugonjwa huu nchini ilikuwa ni Juni  2010 mkoani Dar es salaam ambapo idadi ya watu waliothibika kuwa na ugonjwa ilikuwa 40 na hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza maisha.

Wananchi mnashauriwa kwenda katika vituo vya tiba mara mnapoona dalili za ugonjwa huu.

Wizara inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini. Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huu.

No comments:

Post a Comment