KILIMANJARO Ugonjwa hatari wa dengue umedaiwa kuingia wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, ambapo watu wawili wamegundulika kuwa na dalili za ugonjwa huo, na hivyo wananchi wa wilaya ya Hai wametahadharishwa kuwa makini na kujikinga na mbu anayeeneza ugonjwa huo.
Tahadhari hiyo imetolewa na wataalumu wa afya wa wilaya ya Hai kufuatia kugunduliwa kwa watu wawili wakiwa na dalili za ugonjwa wa Dengue ambao umekuwa
tishio kubwa kwa wananchi wengi tangu ulipotangazwa kuingia nchini Tanzania na hususani katika mkoa wa Dar es salaam kuanzia mwanzoni mwa mwezi machi mwaka 2014.
Wakizungumza na waandishi wa habari madaktari katika hospitali ya Wilaya ya Hai Dokta Julius Massawe na Dokta Happynes Ndenshau walisema mpaka sasa kuna dalili za ugonjwa huo kuwepo wilaya Hai kutokana na watu wawili kusadikiwa kuwa na dalili za ugonjwawa Dengue.
Dokta Julius Massawe amesema watu hao wawili ambao wanasadikiwa kuwa walitokea jijini Dar es Salaam ambapo mmoja ni mkazi wa kijiji cha Narumu kata ya Narumu Mashariki na mmoja ni mkazi wa mtaa wa Kibaoni katika wilaya ya Hai wanasadikika kuwa na dalili za ugonjwa huo ila madaktari hao wanasubiri vipimo zaidi kutoka katika hospitali ya rufaa ya KCMC, ambapo wamepeleka damu ya watu hao kwa uchunguzi zaidi.
Dokta Massawe aliendelea kusema >> "kufuatia watu hao kuonesha dalili hizo za ugonjwa wa Dengue, ambao kwa sasa wamelazwa katika hospiali ya St. Jose ya mjini Moshi wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari mapema pindi wanapohisi kuugua ugonjwa huo kwa kufika katika hospitali ili waweze kupatiwa matibabu ya haraka."
Alifafanua kuwa wagonjwa hao wawili inasadikiwa kuwa walikuwa jijini Dar es Saalam kwa ajili ya kuwatembelea ndugu zao na waliporejea nyumbani kwao walianza kuumwa na kugunduliwa kuwa wanadalili za ugonjwa huo hatari wa Dengue.
Dokta Ndenshau alisema >> "Wanachofanya kwa hivi sasa ni kutoa elimu kwa madaktari na wauguzi na watu wengine, ili wanapobaini mtu mwenye dalili za ugonjwa huo ni vizuri akapelekwa hospitali mapema."
Asema kwa sasa hakuna tiba wala chanjo ya ugonjwa huo, hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya maambukuzi ya magonjwa yanayosababishwa na mbu.
Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuumwa kichwa, homa kali, upungufu wa damu na kupoteza maji mwilini, hivyo wananchi wametakiwa kuwahi kituo cha afya mara moja pindi wanapohisi dalili kama hizo, au dalili kama za malaria.
No comments:
Post a Comment