Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, June 26, 2014

SERIKALI HAITAAJIRI MTUMISHI WA UMMA AMBAYE HANA SIFA YA UZALENDO

DODOMA serikali imesema kuanzia sasa haitaajiri mtumishi wa umma ambaye hana sifa ya uzalendo ikiwemo kupitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Makatibu Tawala wasaidizi wa sekretarieti za Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimali katika Wakala na Taasisi za Umma.


Balozi Sefue alisema serikali haiwezi kuendelea kuwa na watumishi wa umma ambao hawana uzalendo licha ya kuwa na sifa zingine zote za kuajiriwa. Alisema hata kama muombaji wa nafasi yoyote ya umma amekidhi vigezo vyote sifa pekee itakayoangaliwa kama nyongeza ni uzalendo kwa muhusika kupitia JKT kama sifa itakayompatia kipaumbele cha kuchaguliwa.


" Nawaombeni muelewe vyema kuwa kipaumbele hiki cha kupitia JKT kitumike tu ambapo sifa zingine zote za muombaji ziko sawa na si vinginevyo" alisema. Katibu Mkuu Kiongozi alisema katika ajira Sera, Sheria, kanuni na Taratibu zimeweka wazi miongozo ya kufuatwa kwenye kuajiri watu katika utumishi wa umma.


Alisema miongoni mwa miongozo hiyo ni uwazi katika kutangaza nafasi za ajira , usawa na haki wakati wa usaili na uajiri watumishi wa umma. Alisema pamoja na kuwepo kwa miongozo hiyo bado kuna malalamiko yanayosikika kuwa uwezi kuajiriwa kwenye Utumishi wa Umma sipokuwa kama unajulikana  au unatoa rushwa ya fedha au ngono.


"Tusipuuze hata kidogo malalamiko ya wananchi, bali tujichunguze na tuchunguzane ili kama mambo hayo bado yapo kwa pamoja tuazimie kuyakomesha kabisa kwenye Utumishi wa Umma." alisema.


Akizungumzia ajira za wastaafu, Katibu Ombeni alisema ataendelea kukataa maombi ya kuwaajiri kwa mikataba watumishi ambao sio adimu kawenye soko la ajira. Alisema licha ya serikali kuajiri watumishi kwa masharti ya mikataba  wapo baadhi ya waajiri wamekuwa wakiwasilisha maombi ya ajira za mikataba hata kwa nafasi ambazo zinaweza kujazwa kwa kupandishwa vyeo maafisa waliopo au kuajiri watumishi wapya.


Balozi Sefue alisema hali hiyo inatokana na baadhi ya waajiri kutokuwa na mipango ya kurithishana madaraka ambao ungetumika kuwaandaa watumishi mapema kwa kuwapa mafunzo ya kuwaongezea weledi na kuwawezesha kupata sifa za kujaza nafasi zinazoachwa wazi.


Alisema wakurugenzi hao wa utawala ni washauri wakuu wa Makatibu Wakuu wa Umma kwenye masuala ya utawala na rasilimali watu hivyo wakifanya vizuri utendaji wao hakutakuwa na lawama dhidi ya Utumishi wa Umma.


Kwa mujibu wa Balozi Ombeni wakurugenzi hao ni lazima kuzifahamu vyema Sera,Sheria, kanauni na taratibu  zinazohusu Utawala na rasilimali watu na kisha kuzizingatia. "Msipo zielewa vizuri kanuni na taratibu zenu mtawapotosha sana viongozi wenu wakuu kwenye Wizara, Idara na Taasisi zenu hivyo ni
muhimu kuzijua" alisema.

Aidha aliwataka viongozi hao kuhakikisha kuwa watumishi wa Umma nao wanazielewa Sera, Sheria, kanauni na taratibu hizo na kamwe wasifanye miongozo hiyo kuwa ni siri ya wachache.

No comments:

Post a Comment